Wastaafu 638 wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), wanaoidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 23 za mapunjo ya mafao yao kwa zaidi ya miaka 20 wamemwomba Rais John Pombe Magufuli kufuatilia madai hayo.

Watumishi hao waliostaafishwa kazi mwaka 1996, wameieleza JAMHURI, kuwa Serikali imekuwa ikiwazungusha kuwapa haki zao bila sababu za msingi licha ya fedha zao za mafao kutolewa na wafadhili Shirika la Misaada la Norway (Norad).

Mwenyekiti wa Kamati ya wastaafu hao, Rashid Mohamed, anasema Serikali imeshauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwalipa wastaafu hao madai yao ili kumaliza mgogoro huo lakini wameendelea kuzungushwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Mohamed anasema fedha za mafao yao zilitolewa na wahisani lakini kilichojitokeza inaonesha baadhi ya watu wachache waliokosa serikalini walinufaika na fedha hizo na hicho ndiyo chanzo cha kuendelea kuzungushwa.

Madai wanayoidai Serikali ni fedha za kujikimu Sh milioni 1.8 kwa kila mmoja walizoahidiwa na mfadhili wa zoezi la kuwapunguza kazi, lakini uongozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ukawalipa Sh 600,000 kila mmoja.

Kutokana na malipo hayo  kila mmoja anadai  malikimbikizo ya Sh 1,200,000. mbali ya fedha hizo pia iliamriwa kila mmoja kulipwa Sh 72,000 kwa muda wa wiki mbili za kusubiri malipo yao lakini hakuna aliyelipwa.

Madai yao mengine ni malipo ya pensheni ya PPF yalifanyika makato yasiyokuwa na maelezo kutoka kwenye malipo ya wadai ambako zaidi ya Sh milioni 163 hazikulipwa kwa walengwa.

Anasema kiasi hicho cha fedha zao za PPF wanachodai kililipwa wakati wao hawapo kazini na kukwapuliwa na wajanja wachache chuoni na Hazina, na kwamba madai waliyonayo yanatofautiana kabisa na yaliyokuwa mahakamani.

‘‘Mkataba wa kupunguzwa kazi watumishi hao ulipaswa kuanza Juni 28, 1996 lakini kwa sababu ambazo hazieleweki ulianza kutumika baada ya siku tatu wakati wao hawapo kazini,’’ anasema Mohamed.

Kutokana na madai ya uongozi wa Chuo hicho kuwa mkataba ulianza Juni 30, 1996, anasema madai hayo hayana ukweli wowote kwani siku hiyo ilikuwa ni Jumapili, kwa maana hiyo huo ni mkataba feki.

Anasema katika mkataba huo ‘feki’ unaeleza kuwa wastaafu hao walilipwa Sh 600,000 ikiwa ni malipo yao ya mabati na saruji, jambo ambalo limekanushwa na wastaafu hao. 

Kwa mujibu wa Twaha Issa Taslima wa Kampuni ya Uwakili ya Taslima aliyekuwa akiwatetea wastaafu hao katika kesi ya madai Namba 299 ya mwaka 1997, anasema mkataba wa hiyari wa Agosti 14, 1995 uliosainiwa na Profesa Massenge, na kuthibitishwa na aliyekuwa Ofisa Tawala wa Chuo, Jaka, kila mmoja wao alistahili kupata malipo ya bati na saruji, lakini wastaafu hao hawakupata.

Katika barua yake yenye kumbukumbu namba TLC/WAST/2 ya Aprili 22,  2006, Taslima anasema kila mmoja alistahili kulipwa nauli Sh 326,220 sawa barua ya Profesa Mshana ya Oktoba 2,  2002, hakuna kilichofanyika hadi sasa.

Taslima aliutaka uongozi wa Chuo kulipa madai ya wastaafu hao ndani ya siku 14 tangu walipopokea barua hiyo ambayo nakala zake zilitumwa kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wakati huo agizo hilo nalo likapuuzwa.

Kesi waliyoifungua Mahakama Kuu, Namba 299 ya mwaka 1997 ilitolewa uamuzi na Jaji Ihema ambapo madai yao yalitupiliwa mbali.

Baada ya madai yao kutupiliwa mbali na Mahakama, walipeleka malalamiko yao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyofafanua kuwa madai ya mapunjo yaliyopelekwa mahakamani ni tofauti na ambayo yapo Serikalini na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, hayakuzungumzwa mahakamani.

“Hivyo hayakuwa sehemu ya kesi iliyotupiliwa mbali na Mahakama Kuu,” imeeleza sehemu ya barua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Julai 11, 2011 yenye kumbukumbu namba J/C.60/3274/17  kwenda kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha iliyosainiwa na Abraham Senguji.

Barua hiyo imeeleza kuwa madai ya wastaafu hao yamepitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Katibu Mkuu, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kama ilivyojulikana wakati huo na Desemba 5, 2008 Katibu Mkuu Kiongozi alitoa maagizo kwamba madai yao yachunguzwe kwa umakini, uwazi na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.

Pamoja na kupendekeza kuundwa kwa kamati ndogo ya kuhakiki madai ya wastaafu hao kama ilivyopendekezwa katika kikao cha Desemba 28, 2008, iliamuliwa wastaafu hao walipwe madai yao kama walivyoomba na mgogoro huo ufungwe.

Katika barua yake ya Agosti 1, 2011 Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaeleza kuwa kamati hiyo ndogo iliyoundwa na Serikali ilishatoa mapendekezo yake kwamba wadai walipwe mapunjo yao ili mgogoro huo ufungwe rasmi, lakini hakuna kilichofanyika baada ya uamuzi huo.

Wastaafu hao wamedai tangu kutolewa kwa maelekezo ya Mwanasheria Mkuu na Kamati ndogo iliyoundwa na Serikali jumla ya madai yao haieleweki kwa uwazi kutokana na uongozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuzuia vocha zao za malipo.

Machi 14, mwaka huu walimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi wakimkumbusha kutokulipwa mapunjo ya mafao yao kutokana na kupunguzwa kazi mwaka 1995 hadi 1997 na kujibiwa kwamba hakuna nyaraka zinazothibitisha uhalali wa madai ya mapunjo ya mafao yao.

‘‘Hivyo basi, msimamo wa awali wa Serikali uliotolewa kupitia barua mbalimbali mlizoandikiwa bado uko pale pale, Wizara inashauri kwamba mna haki ya kuwasilisha madai yenu mahakamani endapo mnaona hamkuridhika na malipo yaliyokwishafanyika,’’ inaeleza sehemu ya barua ya iliyoandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Servacius Likwelile.

Kutokana na majibu hayo ambayo wameyaita kwamba yana lengo la kudhurumu haki zao, Aprili 13 mwaka huu, walimwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi wakilalamikia majibu hayo ya Dk Likwelile na kwamba wana mgogoro na Serikali zaidi ya miaka 20 wakizungushwa kulipwa haki zao licha ya kupitia sehemu mbalimbali na suala hilo kupatiwa ufumbuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini Wizara ya Fedha imekuwa kikwazo.

Wanasema licha ya kufikisha madai hayo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi mbalimbali za Serikali hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kuhakikisha mgogoro huo unafikia mwisho.

Afisa Habari wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaya, anasema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alikwisha toa maelekezo kwa wastaafu hao hivyo ni muhimu wakayatekeleza.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa wastaafu hao anasema inapaswa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kulipa madai hayo waliyopunjwa kwa makusudi, pia kuongeza malipo yao ya wastaafu ya kila mwezi kutoka Sh 50,000 hadi 100,000 kama yalivyoongezwa na Serikali mwaka uliopita.  

Awali walifikisha madai yao kwa Katibu Mkuu wa CCM, ambako katika barua yake ya Juni 28, 2013 anaeleza kuwa madai yao ni ya msingi kwa kuwa idadi ya waliokuwa wamestaafishwa mwaka 1996 ni 265 waliotengewa zaidi ya Sh bilioni 1.7. 

Anasema uamuzi ya Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu na Utumishi walitoa Sh bilioni 1.4 kulipa mafao ya wastaafu 265, badala yake wakaongezwa wastaafu wengine 638 na kufanya idadi mpya kuwa 903 na kulipwa kiasi hicho cha fedha.

3807 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!