DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Asasi za kiraia nchini (AZAKI) zimependekeza suala la uwazi wa mikataba ya sekta ya uziduaji kuwa mojawapo ya vipaumbele vya serikali wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Tatu unaotekelezwa sasa.

Pendekezo hilo lilitolewa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Azaki yaliyofanyika jijini Dodoma wiki iliyopita – mbele ya waziri mmoja na manaibu waziri wawili waliokuwa wamehudhuria maadhimisho hayo na kushiriki katika mjadala kuhusu mchango wa sekta za uziduaji na viwanda kwa maendeleo ya nchi.

Akiwakilisha Azaki mbalimbali za masuala ya uziduaji, Mkurugenzi wa Asasi ya HakiRasilimali, Racheal Chagonja – ambaye pia alikuwa mmoja wa waongozaji wa mjadala huo, alisema usiri wa mikataba ya sekta ya uziduaji ni miongoni mwa masuala yanayoikosesha serikali na wananchi haki ya kufaidi mapato yao.

Kwa mujibu wa Chagonja, endapo mikataba ya sekta ya uziduaji ingewekwa wazi na kujadiliwa kwa kina, serikali ingeweza kupata mikataba mizuri zaidi na yenye faida kwa ajili ya kufanikisha maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta hiyo.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoamini katika uwazi na tumesaini mikataba mbalimbali ya kutambua hilo. Huko nyuma, mheshimiwa waziri uliwahi kuahidi kwamba mikataba itakuwa wazi kuanzia mwaka 2019 lakini hilo halijatokea bado. Tunaomba hilo lifanyike kwa masilahi mapana ya nchi yetu,” amesema Chagonja.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko, alikuwa akimsikiliza Chagonja wakati akizungumza; akiwa amesindikizwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe. Mada katika tukio hilo ilihusu ni kwa namna gani sera za serikali zimeweza kuvutia wawekezaji kuja nchini na wakati huohuo yenyewe ikifaidika na utajiri wa maliasilia uliopo nchini.

Mjadala kuhusu uwazi ulichagizwa pia na hoja kutoka kwa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyetoa maelezo kuhusu mgodi wa madini ya nickel ulioko Kabanga ambao umeuzwa kwa kampuni moja kwa gharama ambazo zinatia shaka.

Katika maelezo yake, Zitto amesema ingawa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutafuta madini katika eneo hilo ulitumia kiasi cha dola za Marekani milioni 250, kampuni iliyouziwa ilipewa mgodi huo kwa gharama ya dola milioni nane tu.

“Hili ni eneo moja ambalo inabidi liangaliwe kwa kina. Utafiti peke yake umegharimu kiasi cha dola milioni 250 halafu mgodi unauzwa kwa dola milioni nane tu. Hapa kuna kitu na sasa kuna haja ya kubaini ni akina nani hasa wako nyuma ya umiliki wa mgodi huu kwa sasa,” anasema Zitto.

Akizungumza katika mkutano huo, Biteko amesema ni kweli kwamba suala la uwazi ni muhimu katika mikataba ya sekta ya madini na jambo hilo linafanyiwa kazi kwa sasa ingawa tayari kuna mambo yako hadharani.

Amesema taasisi kama TEITI zilizoko nchini zimeanza kutimiza majukumu yake mbalimbali ya kuweka uwazi katika sekta hiyo na kwamba muda si mrefu suala la uwazi katika madini litakuwa si suala kubwa tena.

“Kupitia TEITI tayari taarifa mbalimbali kuhusu mapato ya sekta ya madini hapa nchini zinawekwa wazi. Tumewahi kutoa ahadi huko nyuma kuhusu uwazi na ninaamini kwamba tunakokwenda mikataba hii itawekwa wazi kwa kila mtu kuiona,” amesema Biteko.

Mjadala huo ulihudhuriwa na wawakilishi mbalimbali wa asasi za kiraia waliokuwa Dodoma, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, wawakilishi kutoka jamii ya wahisani, wataalamu wa sekta mbalimbali za uchumi na maendeleo na waandishi wa habari.

Waziri Biteko aliueleza mkutano huo kwamba ana matumaini makubwa kuwa ifikapo mwaka 2026, mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa utafika asilimia 10 – kama ilivyoelezwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Amesema kwa sasa mchango huu unafikia asilimia saba na kwamba kwa mipango iliyopo, kuingia kwa wawekezaji na ushirishwaji unaoendelea wa wananchi katika mnyororo wa thamani, mambo yanakwenda kuwa mazuri zaidi.

Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa, alihoji ni kwa “miujiza” gani Biteko ataileta katika wizara hiyo kufikia mchango huo wa asilimia 10 ilhali tangu mwaka 2016, ukuaji haujawahi kuzidi asilimia moja kwa mwaka.

Kwa upande wake, Byabato alisema sekta ya nishati itakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa sababu ya miradi mikubwa inayotekelezwa na inayopangwa kutekelezwa kuanzia sasa hadi mwaka 2026.

Akizungumza kwa mifano, alisema Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) peke yake utatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 1,000 kwa Watanzania pamoja na mapato mengine katika mnyororo wa thamani.

Amesema Novemba 8, mwaka huu, serikali kupitia wizara yake inaanza rasmi mazungumzo ya kufufua mradi wa gesi wa Lindi, maarufu kwa jina la LNG ambao ulionekana kukwama katika miaka ya karibuni.

Wachangiaji mbalimbali waliozungumza katika mkutano huo walisema serikali haitakiwi kurudia makosa ya nyuma ambako miradi mikubwa ya sekta ya nishati na madini ilifunguliwa mpaka kufungwa pasipo kuwa na mikakati kabambe ya uwezeshaji wazawa (Local contents).

Serikali ilishauriwa kuhakikisha Watanzania wanafaidika kwa kupata ajira, kutoa huduma mbalimbali zinazoendana na shughuli za kwenye migodi na mashapo ya gesi pamoja na kufungamanisha sekta ya uziduaji na sekta nyingine za uchumi hapa nchini.

Kwa upande wa Kigahe, anasema ukuaji wa sekta ya viwanda katika miaka ijayo kutategemea sana ukuaji wa sekta ya uziduaji, kwa sababu zana nyingi za viwandani ni matokeo ya malighafi kutoka sekta ya uziduaji.

340 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!