TABORA

Na Moshy Kiyungi

Ukitazama ghafla jukwaani unaweza kudhani kuna mtoto wa shule aliyepanda kuimba na kunengua, lakini kumbe ni mwanamuziki maarufu wa dansi nchini, Khadija Mnoga.

Umbo lake dogo na sura yenye bashasha muda wote, sambamba na umahiri wake stejini, vimempa umaarufu mkubwa na kupachikwa jina la ‘Kimobiteli’.

Khadija ni mwimbaji mzuri sana wa muziki wa dansi na taarabu, ambaye awali alipanga kuingia kwenye sanaa hiyo baada ya kuzaa.

“Nilihofia kujikuta nikizeeka bila kuwa na mtoto kutokana na pilikapilika nyingi za muziki. Kwa hiyo baada ya kupata mtoto wa kwanza, alipomaliza kunyonya nikamkabidhi kwa mama yangu,” anasema.

Khadija, mzaliwa wa Mwananyamala, Dar es Salaam, alisoma Shule ya Msingi Mwongozo iliyopo Kinondoni na kuhitimu darasa la saba mwaka 1995, kisha akajiunga na Sekondari ya Navy, Kigamboni.

Akiwa shuleni alipendelea zaidi michezo na hakuna aliyedhania kuwa baadaye angekuja kuwa mwanamuziki.

Kipaji cha sanaa ya uimbaji kilianza kujitokeza alipojiunga na kikundi cha Chipukizi cha CCM, Mwananyamala, mwishoni mwa miaka ya 1990, kilichokuwa kikimiliki kwaya.

“Ni hapo ndipo nilipojitambua kuwa nina kipaji cha kuimba, kwa kuwa watu wengi walivutiwa sana na uimbaji wangu,” anasema.

Kikundi hicho kilikuwa kikifadhiliwa na diwani mmoja wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Bwana Ndege, hivyo kupata mialiko katika shughuli nyingi za CCM.

“Watu waliovutiwa na uimbaji wangu walikuwa wakinituza hadi Sh 100,000 katika onyesho moja,” anasema. 

Anasema wenzake wakaanza kumshawishi ‘apande ngazi’ na kujiunga na kikundi kikubwa zaidi kuliko kwaya hiyo ya chipukizi.

Alipomwambia mama yake kwamba anajiamini na ana uwezo wa kuimba kwenye bendi ya muziki, mama yake hakumuunga mkono wala hakumkatalia.

Siku chache baadaye, mpiga ngoma wa kwaya ya chipukizi akampa taarifa kwamba kuna bendi inahitaji mwimbaji wa kike.

Mara moja akaenda kwenye mazoezi ya bendi hiyo na anasema: “Wala hata sikuuliza ni bendi gani.

“Safari yangu ikanifikisha karibu na mataa ya Fire. Hapo nikakutana na Shikamoo Jazz! Kumbe hao ndio walikuwa wakihitaji mwimbaji wa kike.”

Shikamoo ni bendi iliyoanzishwa mwaka 1994 ikiwa na wanamuziki wastaafu kama Salim Zahoro, Kapteni John Simon na Majengo Selemani.

Wakongwe hao walikuwa wakifanya mazoezi nyumbani kwa Waziri Nyange, Buguruni.

Wazee hao walikigundua kipaji cha Khadija na kumpa malezi mazuri wakifahamu kuwa nyimbo zao nyingi hazifahamu.

“Wakawa wakinipa nauli kila siku ya kwenda na kurudi mazoezini, na pesa kidogo ya kujikimu,” anakumbuka Kimobiteli.

Hata kabla ya kupanda jukwaani na Shikamoo Jazz, tayari viongozi wa Young Star Taarab ‘Wana Segere’ wakapata taarifa za kuwapo kwa binti mdogo mwenye sauti nzuri ambaye amejiunga na wazee.

Mbinu zikafanywa za kumnasa kiaina Khadija.

“Kwanza walinikaribisha nikawatembelee. Nikaenda na kuambiwa wao huimba nyimbo za taarabu. Kwa kuwa nina asili ya Zanzibar, kwenye taarabu nilijisikia nyumbani zaidi,” anasema.

Akaingia kwenye mazoezi, vyombo vikapangwa na wenyeji wake wakamuuliza ni wimbo gani wa taarabu anaweza kuimba.

Khadija akaimba wimbo uliokuwa maarufu Zanzibar wakati huo, wenye maneno haya:

“Nafanya kwa raha zangu kwetu sigombwi, na nikigombwa napewa pipi, napewa pesa na Mobitel.”

Siku hiyo hiyo akapokewa rasmi kundini na kuambiwa ajiandae kupanda stejini usiku wa siku hiyo kuanza kazi.

“Mara yangu ya kwanza kupanda stejini nikaimba wimbo ule ule nilioimba kwenye mazoezi. Kwa kuwa wimbo huo una neno ‘Mobitel’, mashabiki wakanipachika jina la ‘Kimobiteli’,” anasema huku akicheka.

Huo ndio ukawa mwanzo wa safari yake kimuziki iliyompitisha katika bendi za African Stars ‘Twanga Pepeta’, Extra Bongo, Mchinga Sound, Double M Sound na African Revolution ‘Wana TamTam’.

Kibao cha ‘Mgumba’ kilichotungwa na Muumin Mwinjuma wakiwa African Revolution, kilitendewa haki na Khadija Mnoga ‘Kimobiteli’ kwa uimbaji mahiri wenye hisia kali na kumfanya kuwa mmoja kati ya waimbaji bora kabisa wa kike wa muziki wa dansi nchini.

Kwa sasa Kimobiteli anafanya kazi ya muziki katika Bendi ya Sayari Stars.

“Mimi nipo jamani wala sijapotea. Nipo Sayari Stars pamoja na akina Rogart Hegga ‘Katapila’, Badi Bakule, Emma Chocolate na wengine wengi tu,” anasema.

Bendi hiyo ina makazi yake Manzese Tip Top, Dar es Salaam.

Siku za nyuma Khadija Mnoga alionekana kwenye Tamasha la 38 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni (TaS-UBa), lililofanyika Bagamoyo, akishirikiana na bendi ya John Kitine (JKF), inayomilikiwa na gwiji wa muziki wa dansi nchini, Kitine.

Fadhila, mdogo wake Khadija, ni mwimbaji wa taarabu wa G5 Modern Taarab, kundi lenye makazi yake Mtoni kwa Azizi Ally.

Kimobiteli anaamini kuwa kuporomoka kwa muziki wa dansi nchini kumesababishwa na baadhi ya vituo vya redio kutopiga muziki huo mara kwa mara tofauti na ilivyokuwa awali.

Anasema wakongwe wa dansi, Sikinde na Msondo, wanaoendelea na muziki huo hadi leo hata wao wananyimwa nafasi ya muziki wao kusikika kwenye baadhi ya vituo vya redio.

“Hiki ndicho chanzo cha kushuka kwa soko la muziki wa dansi, ingawa mashabiki wake bado wapo wengi tu,” anasema.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba 0767331200, 0784331200 na 0713331200.

429 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!