Katika toleo la leo tumechapisha taarifa zinazoonyesha kuwa Serikali imechukua hatua ya kurekebisha kasoro zilizodumu kwa takriba miaka 20 katika sekta ya madini. Serikali imepeleka bungeni miswada ya sheria tatu zenye lengo la kupitia mikataba ya sasa ya madini na ijayo kuweka msingi wa nchi kufaidi rasilimali za taifa.

Hatua ya kupeleka miswada hii bungeni imekuja baada ya Rais John Pombe Magufuli kuwa ameunda Kamati mbili za kuchunguzi usafirishaji michanga nje ya nchi, michanga inayofahamika kama makinikia. Rais Magufuli amebaini mambo ya kutisha kupitia kamati hizo.

Imebainika kuwa tangu mwaka 2001 nchi imepoteza wastani wa Sh trilioni 108, ambazo kimsingi ni karibu mara tatu ya deni la taifa. Hii ina maana kuwa nchi ya Tanzania ingeweza kulipa deni linaloikabili, ikajenga miundombinu karibu nchi nzima na kubakia na “chenji”.

Rais Magufuli amesema mara kadhaa kuwa kwa sasa nchi ipo katika vita ya kiuchumi. Kwa yeyote aliyesoma historia ya dunia hii na kukumbuka masuala waliyopigia kelele wachumi waadilifu kama akina Walter Rodney kupitia kitabu chake cha ‘How Europe Underdeveloped Africa’ watakubalina na msimamo anaouchukua Rais Magufuli.

Sisi wa JAMHURI tunasema hatua ya kupitia mikataba ya madini na kulipa Bunge nguvu ya kuigiaza Serikali kufungua majadiliano kwa masilahi ya taifa katika mikataba ya sasa na iliyopita, tunasema tunaiunga mkono kwa asilimia 100.

Tunawaomba Watanzania tuungane katika hili kwani nchi yetu ipo katika vita ya kiuchumi. Inawezekana baadhi ya watu wana hofu ya Wazungu kuwa wakizuiwa kutunyonya watakasirika na kutunyima misaada, lakini sisi tunasema heri tunyimwe misaada kuliko kiwango hiki cha kuporwa madini yetu.

Hakuna siku, wala saa ambayo woga wetu utawafanya Wazungu waheshimu haki zetu. Kwa kuwa Rais Magufuli ameonyesha njia, tuungane pamoja kushinikiza mabadiliko ya mikataba hii kwa faida ya taifa letu.

Kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiyo hiyo hiyo iliyoiingiza nchi katika mikataba hii mibovu, ni hoja sahihi, ila haitusaidii kwa sasa. Hatua tuliyopo ni ya kupitia mikataba hii kuwanufaisha Watanzania na si vinginevyo. Watanzania tushikamane, tufaidi rasilimali za taifa letu.

Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri