KikweteWakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjemin Mkapa, akiwa Tanga alisema kwamba dunia ingeshtushwa kama ingesikia kwamba Watanzania wamekiangusha chama kikongwe kama CCM.

Alisema kwamba CCM ni chama cha ukombozi kinachoendelea kuwakomboa Watanzania. Lakini ukitaka kusema kweli dunia imeshtushwa kusikia kwamba chama kikongwe kama CCM ambacho kimechokwa na wananchi kimeshinda uchaguzi. Ni katika mazingira hayo watu wengi huamini kwamba CCM imeshinda uchaguzi baada ya kuiba kura!

Madai kwamba CCM imeshinda uchaguzi baada ya kuiba kura yanatiliwa nguvu na mambo mengi. Kwa kuanzia inaonekana wazi kwamba CCM ilijua mapema kwamba isingeshinda uchaguzi huu.

Kwa hiyo, kwa mfano, baada ya uchaguzi kuwa ni wa kushindanisha vyama, CCM iligeuza kuwa wa kushindanisha wagombea. Kwa upande wa mambo yanayotilia nguvu madai kwamba CCM imeshinda kwa kuiba kura kuna mambo makubwa matatu.

Kwanza, CCM na Serikali yake hawajawahi kutumia nguvu kuhusika katika kuwakataza wapiga kura kusimama mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura kama ilivyotumia mwaka huu.

Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alikataza. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imeteuliwa na Rais nayo ilikataza. Nalo Jeshi la Polisi lilikataza.

Watu wanaendelea kujiuliza yote hayo yalifanyika kwa lengo la kulinda amani au kutoa nafasi ya kuibwa kura? 

Pili, Serikali ya CCM kupitia Jeshi lake la Polisi ilitumia nguvu kubwa katika kukamata kompyuta na simu za mkononi kuzuia matokeo ya uchaguzi yasikusanywe ingawa katika chaguzi za nyuma watu walikusanya matokeo bila matatizo.

Kwa kweli, kitendo hicho kilishangaza watu kwa sababu hatua iliyokuwa imechukuliwa na Serikali ilikuwa ni kutangaza matokeo. Haikukataza kukusanya matokeo.

Tatu, wananchi wanaendelea kuamini kwamba sababu ya Serikali kuzuia watu wake wasikusanye matokeo ilikuwa kuzuia wananchi wasijue wizi wa kura uliotokea. Ilibainishwa kwamba kura zilizotangazwa na Tume ya Uchaguzi zilitofautiana sana na zile ambazo wananchi walikuwa wakikusanya vituoni.

Kwa mfano, Tunduma; mbunge wa Chadema alipata kura 32,000, lakini mgombea urais kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa, alitangazwa kuwa amepata kura 6,000 ilileta picha kwamba watu wa Ukawa na mashabiki wao walikuwa wamempa mgombea ubunge kura 32,000 lakini walimkataa mgombea urais kwa kumpa kura 6,000!

Kwa hiyo, wananchi wanaamini madai kwamba mgombea urais kupitia Chadema na Ukawa alipata kura 32,000 sawa na zile alizopewa mgombea ubunge kupitia Chadema.

Biblia katika Mathayo 10:26 inatamka kwamba “hakuna neno lisilositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana.”

Basi, tukitaka kusema kweli, mwaka huu Watanzania walikuwa wamejipanga kuikataa CCM hata kabla Dk. John Magufuli hajateuliwa na chama chake kugombea urais.

Hii ni kusema kwamba Dk. John Magufuli angeweza kushinda kwa kishindo kama Watanzania wasingekuwa wamejipanga mapema kuikataa CCM.  Kwa kifupi, Watanzania hawakumpa kura Dk. Magufuli, hawakumkataa yeye bali waliikataa CCM.

Kwa kuwa katika kila uchaguzi CCM, imehusishwa na wizi wa kura basi Watanzania wanalikemea jambo hilo kwamba CCM imepona kwa kuiba kura. Hapa tuna kila sababu ya kukemea huu wizi unaoaminiwa kuwa unatokea kila mwaka wa uchaguzi. 

Kwanza, ni jambo la hatari kwa umoja na usalama wa Taifa wananchi wakiamini kwamba wanaendelea kutawaliwa na chama kilichoshindwa uchaguzi na ambacho wamekichoka.

Pili, ni aibu mbele ya mataifa ya nje chama kilichoshindwa uchaguzi kujidumisha madarakani kwa kutegemea kuiba kura na kulindwa na majeshi. Ubabe si sehemu ya utawala bora.

Tatu, ni jambo la hatari pia kuziba njia zote za wananchi kutafuta haki kwa kuwa waliotunga Katiba ya nchi mwaka 1977 walitaka CCM itawale milele, Tanzania walipanga hilo liwezekane kwa kupitisha sheria ya kukataza matokeo ya urais yasihojiwe mahakamani katika hali ya kujulikana mapema kwamba Tume ya Uchaguzi ingetumiwa kuiba kura. 

Njia ya kutafuta haki ikazibwa.  Lakini pia maandamano ni njia nyingine ya kidemokrasia ya kutafuta haki. Polisi wametumika vema kuziba njia hiyo ya halali ya wananchi kubainisha haki yao.

Ni katika hali hii kuna haja ya CCM na Serikali yake kukumbushwa kwamba nchi zote duniani zilizoziba mianya ya watu wake kutafuta au kupata haki, zimejikuta zimekaribisha ugaidi. 

Utawala wowote hauwezi kuzuia ugaidi kama unakandamiza haki za watu. Bila haki hakuna amani ni kauli ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alizoea kuitoa.

Lakini kuiba kura ni matokeo ya watu kukosa hofu ya Mungu. Ni matokeo ya kutaka kujipatia madaraka kwa nguvu ya shetani. Tukiangalia Biblia tunakuta kwamba kitabu hicho ni mkusanyiko wa vitabu vitakatifu visivyopungua 60.

Miongoni mwa vitabu hivyo vipo Waraka wa Paulo, Mtume kwa Warumi.

Katika Warumi 13: 1-7 Paulo Mtume anafundisha elimu ya uraia. Anaanza kwa kuandika kwamba “kila mtu na atii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.”

Basi kwa muda mrefu dunia iliendelea kuamini kwamba mamlaka yote hutoka kwa Mungu. Lakini, baada ya Yesu Kristo kujaribiwa na ibilisi jangwani, watu wanajua si kila mamlaka inatoka kwa Mungu. Mamlaka nyingine hutoka kwa shetani.

Katika Mathayo 4: 8-9 tunasoma kwamba ibilisi alimchukua Yesu Kristo mpaka mlima mrefu mno. Akamwonyesha milki zote za ulimwengu na fahari yake. Akamwambia, “Haya yote nitakupa ukianguka kunisujudia.”

Basi, ibilisi au shetani hutoa uwezo wa utawala kwa mtu au kundi lote la watu linaloanguka na kumsujudia. Chama chochote na Serikali yake lazima viheshimu hiyo haki. Viepuke kuiba kura, lazima watu wawe na hofu ya Mungu, kujipatia mamlaka kwa kuiba kura ni kumsujudia shetani.

Lakini hapa ni jambo la kutia faraja kuona uwezo mkubwa wa Mungu kupangua mipango mibovu ya mwanadamu. Kwa mfano, tunajua kuwa viongozi wakuu wa CCM kwa sababu zao binafsi hawakupenda Edward Lowassa apate nafasi ya kuwa rais. Kwa hiyo, walilikata jina lake mapema. 

Wakaleta kwenye vikao vyao vya uteuzi majina ya watu watano bila jina la Lowassa aliyeonekana kukubalika ndani na nje ya chama. Kwa hiyo, Mungu alitumia wajumbe wa Kamati Kuu na wa Halmashauri Kuu ya CCM wafuasi wa Lowassa kupangua majina ya watu walioandaliwa kupitishwa katika kinyang’anyiro hicho.

Walikuwa wafuasi wa Lowassa walioamua kuwaengua Bernard Membe na January Makamba kwenye mbio hizo. Kisha wakapanga kuwaengua Dk. Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali. Wakampitisha Dk. Magufuli. Ni muhimu hili lijulikane kwamba waliompitisha Dk. Magufuli ni wafuasi wa Lowassa waliotumia wingi wao kuwaadhibu viongozi wakuu wa CCM kwa kumwengua Lowassa kwa njia ambayo haikuendana na Katiba ya CCM.

Baada ya maelezo hayo, sasa tunaweza kuzungumzia sababu zilizofanya Watanzania kujipanga kuikataa CCM.

Kwanza, Watanzania wanaangalia CCM kama chama cha ukandamizaji na si chama cha ukombozi kama inavyoendelea kudaiwa. CCM, kama chama, inaonekana inaongozwa na watu waliotawaliwa na ubinafsi wasiojali watu wengine.

Wananchi wanajua fika kwamba ni chama cha TANU kilichokuwa chama cha ukombozi. Ni TANU iliyoikomboa Tanganyika (Tanzania Bara). Baada ya hapo TANU iliendeleza ukombozi wa wananchi kwa kuanzisha Azimio la Arusha mwaka 1967 lililokuwa na lengo la kuleta hali bora ya maisha kwa kila mwananchi, na TANU ilifanikiwa kutimiza lengo hilo. Wananchi walipata elimu bure, matibabu bure na maji bure.

Juu ya yote, Azimio la Arusha lilifuta matabaka. Mwaka 1977 ikazaliwa CCM. Mwaka 1991 CCM ilifuta Azimio la Arusha lililowakomboa Watanzania. Kuanzia wakati huo, Watanzania wamerejea tena kwenye matabaka aliyotuachia mkoloni. Watoto wa maskini wanapewa elimu duni na michango ya shule inayowaumiza wazazi haihesabiki.

Watoto wa wakubwa wanasoma nchi za nje na hapa nchini kwenye shule za watu binafsi wanakopewa elimu bora. Maskini Watanzania wana hospitali zisizo na dawa wala vitanda.

Wagonjwa wanalala sakafuni na wanaobahatika kupata vitanda wanalala wawili wawili. Wakubwa wanatibiwa nje ya nchi au hapa nchini katika hospitali za watu binafsi zinakopatikana dawa. Maskini Watanzania hawana maji wala umeme wa kuaminika. Wakubwa wana maji na umeme wa haraka.

Ni katika mazingira haya, mwaka huu Watanzania waliunga mkono juhudi za kutaka mabadiliko zilizoongozwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Mabadiliko wanayotaka wananchi siyo ya kupewa fedha za Serikali kama inavyopotoshwa. Ni mabadiliko ya wananchi kupata maji na dawa, watoto wao kupata elimu bora, michango ya shule kudhibitiwa na Serikali na kadhalika.

Kwa kuwa viongozi wa CCM na wa Serikali wamenufaika na hali mbaya iliyoendelea kuwakumba wananchi wameendelea kupinga wazo la mabadiliko.

Hata hivyo, wananchi wamefaidika na kauli za Rais Dk. Magufuli aliyoendelea kuitoa wakati wa kampeni kwamba yeye atawaletea Watanzania mabadiliko ya kweli.

Na wapo waliompigia kura kwa kuamini kwamba kweli ataleta mabadiliko. Hali ya wakubwa kuendelea kuishi maisha bora huku wanaowaongoza wakiendelea kuishi maisha duni, imefananishwa na utawala wa makaburu iliyowakandamiza na kuwabagua Waafrika.

Lakini watu wengine wamekwenda mbali zaidi, wanauona utawala wa CCM mbaya zaidi kuliko wa makaburu kwa sababu ni utawala wa Waafrika wachache walioamua kuwakandamiza na kuwabagua Waafrika wenzao. Ni katika hali hiyo tena Watanzania walijipanga kuikataa CCM, chama kilichojipambanua kuwa ni chama cha ukandamizaji.

Watanzania walijipanga kuikataa CCM pia kwa sababu CCM na Serikali yake vimejali zaidi maendeleo ya vitu badala ya kujali maendeleo ya watu. Ni kweli wamejenga na wanajivunia barabara. Lakini wameacha watu hawana maji wala umeme wa kuaminika. Ni kweli pia kwamba wamejenga shule. Lakini wameacha watoto wa maskini wakipata elimu duni na badala yake wanakaa sakafuni madarasani.

Vilevile ni kweli kwamba wamejenga hospitali, lakini wameacha watu bila dawa na baadhi ya wagonjwa wanalala sakafuni. Halafu akinamama wanaotaka kujifungua hujinunulia vifaa vya uzazi.

Kwa hivyo, Watanzania walijipanga kuikataa CCM na katika juhudi zao za kutafuta mabadiliko, walitafuta utawala wa chama kingine ambacho kingejali maendeleo ya watu badala ya utawala wa CCM ulioweka mbele maendeleo ya vitu.

Bei ya vyakula haikamatiki na hasa baada ya kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Nne. Kwa hiyo, Watanzania walio wengi hupata mlo mmoja kwa siku na wengine hulalia maji. Kwa hiyo, Watanzania walijipanga kuikataa CCM ili wapate chama ambacho Serikali yake ingejali maisha yao kwa kudhibiti bei ya vyakula. 

Serikali ya CCM imeua viwanda vilivyojengwa na Serikali ya TANU, kwa hiyo vijana wengi hawana ajira. Lakini wakati huo huo wananchi wanajitafutia ajira kama wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga), Mama Lishe na Bodaboda.

Serikali ya CCM imewasumbua, imewanyanyasa na imewapora vitu vyao na fedha zao na kuwaacha hawana uwezo wa kurejesha mikopo. Hii ilikuwa ni sababu nyingine ya Watanzania kujipanga kuikataa CCM. 

Halafu japokuwa alama ya CCM ni jembe na nyundo, CCM na Serikali yake haikujali wakulima wala wafanyakazi. Alama hiyo imebaki kuwa mapambo tu. Wakulima wameendelea kukopwa mazao yao na walipodai malipo wamesumbuliwa. Vile vile, wakulima wamepangiwa bei ya mazao na wanunuzi kwa kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia vyama vya ushirika.

Na kwa upande wa wafanyakazi, walimu, madaktari na wauguzi ama hawakupewa haki zao au wamecheleweshewa haki zao. Kwa mfano, mtu anapandishwa daraja lakini hapewi malipo yanayolingana na daraja lake.

Hizi zilikuwa sababu za wakulima na wafanyakazi kujipanga kuikataa CCM, wakati huo huo Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia maliasili ya nchi na uchumi wa Taifa.

Madini ya tanzanite ambayo hupatikana Tanzania tu yamenufaisha zaidi wananchi wa Kenya, Afrika Kusini na India kuliko Watanzania wenyewe.

Wanyamapori wa Tanzania wamesombwa usiku kupitia viwanja vya ndege vinavyolindwa. Ujangili Tanzania umepoteza asilimia 63 ya tembo wote nchi katika miaka hii minne.

Mikataba mibovu ya madini na vitalu vya wanyamapori vimenufaisha zaidi wageni na wakubwa kuliko wananchi. Fedha za umma zimeibwa katika halmashauri za wilaya zisizopungua 70 na hakuna aliyechukuliwa hatua. Hizi zilikuwa sababu nyingine za Watanzania kuikataa CCM.

Halafu, kuna masuala sugu ya rushwa na ufisadi ambayo kila mtu anaamini kwamba utawala wa CCM hauwezi kuikomesha rushwa na ufisadi. Mambo hayo yamekuwa ni sehemu ya uhai na maisha ya CCM.

Kwa upande wa rushwa si kama tu CCM imeendelea kutoa rushwa ya khanga, fulana na kofia kwa wanachama wake ili waipigie kura, bali pia CCM, kupitia wabunge wangi, iliwahi kupitisha sheria iliyoruhusu kutoa rushwa kwa wapigakura (takrima).

Licha ya sheria hiyo kufutwa na Mahakama, bado rushwa inatumika katika kusaka kura. Kwa kuwa chama tawala kimehusishwa na utoaji rushwa, matokeo yake yamekuwa wananchi kukosa haki polisi na mahakamani.

Lakini pia Tanzania imedhalilishwa kutokana na kukithiri rushwa nchini. Na kwa upande wa mafisadi ndani ya CCM mtu haitwi fisadi mpaka ahame CCM. Akiendelea kubaki CCM, fisadi huendelea kuonekana mtu safi sana.

Kwa hiyo, ndani ya CCM bado wako mafisadi wa EPA, rada na Tegeta Escrow. Bado ni jambo la kubahatisha kutegemea kwamba ufisadi utakomeshwa nchini na rais kutoka CCM.

CCM ina tabia sugu ya viongozi wake kulindana. Kwa hiyo, rais kutoka CCM anaweza kuwa safi lakini baadaye anageuka kuwa mla rushwa, fisadi, mbinafsi kwa kuwa hiyo ndiyo tabia sugu ya mfumo wa utawala wa CCM.

Watanzania wanawajua watu waliochotewa mamilioni ya fedha za Tegeta Escrow kutoka Benki ya Mkombozi, lakini Serikali ya CCM imeendelea kuwaficha na kuwalinda watu wa Ikulu waliochotewa mabilioni ya fedha hizo kutoka Benki ya Stanbic.

Basi, tabia ya Serikali ya CCM ya kuwalinda wala rushwa na mafisadi ni sababu nyingine iliyofanya Watanzania kujipanga kuikataa CCM.

Watanzania wanaamini kwamba rais kutoka CCM hawezi kupambana na rushwa wala ufisadi kwa kuwa maovu hayo yamekuwa ni sehemu ya utawala wa CCM.

Kwa ujumla, Watanzania walikuwa na sababu nyingi za kujipanga kuikataa CCM baada ya kuona kwamba CCM, kama chama tawala, imeshindwa kutawala kwa ujumla.

Kutawala ni kudhibiti uhalifu, kuwapa watu huduma bora za jamii, na kuwapa raia haki zao. Serikali ya CCM imeshindwa kufanya hayo, lakini pia Watanzania walijikuta wamejipanga kuikataa CCM baada ya kuona kwamba chama hicho tawala kimeshindwa kusimamia Serikali yake.

Serikali ya CCM, hasa ya Awamu ya Nne, haikuwa sikivu na ilijiona iko juu ya chama chake. Kwa mfano, chama tawala kilipotaka mawaziri mizigo waondolewe, Serikali iliwatetea na kudai kuwa walikuwa watu safi. Yote hayo ni matokeo ya mtu mmoja kuwa kiongozi wa chama pia wa Serikali.

Mwisho, sisi sote tunajua kazi ngumu inayomkabili Rais John Magufuli katikati ya nchi ambayo Serikali iliyomaliza muda wake iliboronga karibu kila kitu.

Rais Magufuli ana kazi ngumu ya kurejesha imani ya wananchi iliyopotea juu ya CCM. Hapa isisitizwe tena kwamba katika uchaguzi uliopita wananchi hawakujipanga kumkataa Dk. Magufuli, walijua kuwa ni mtu mzuri, lakini wananchi wamekata tamaa kiasi cha kuamini kwamba rais kutoka CCM hawezi kuleta mabadiliko kwa kuwa mfumo wenyewe unatoa nafasi kwa rais kuwa naye mla rushwa, fisadi na mbinafsi.

Hivyo ndivyo wanavyoamini wananchi. Ni katika mazingira hayo, Watanzania walikuwa wamejipanga kumchagua Lowassa, mfuasi na mcha Mungu na mvumilivu aliyechafuliwa sana bila kujibu neno. Kwa ujumla Watanzania wanamwangalia Lowassa kama mzalendo na mwenye mapenzi ya kweli kwa Watanzania. 

Ikumbukwe kwamba hakuna kiongozi wa Tanzania aliyejali tatizo la watoto wa maskini waliokuwa wakirudi nyumbani kwa maelfu baada ya kumaliza elimu ya msingi, alikuwa Lowassa aliyesimamia kwa ufanisi mkubwa ujenzi wa shule za sekondari za kata. 

Hii ni kusema kwamba Watanzania wamekata tamaa kabisa na matokeo ya uchaguzi kila mtu anayetarajia kwamba Dk. Magufuli ataongoza safari ya mabadiliko ambayo Lowassa hakupewa nafasi ya kuongoza.

1832 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!