Siku zote ubabe unagharimu

Jumapili Oktoba 25, 2015 tulikuwa na uchaguzi wa kihistoria hapa nchini. Nimeuita uchaguzi wa kihistoria kwa namna ulivyoendeshwa. 

 Baada ya Tume ya Uchaguzi kupuliza kipenga Agosti 22, 2015 kuashiria mwanzo wa kujinadi wagombea katika Uchaguzi, kampeni zilianza kwa kishindo.

 Haijawahi kutokea katika nchi yetu tukawa na uchaguzi usiotabirika kama huu wa mwaka 2015. Kampeni zilichukua muda wa siku 63. 

 Nchi hii imeshuhudia chaguzi nyingi kuanzia uchaguzi ule wa kihistoria tulioita uchaguzi wa Mseto, enzi za ukoloni mwaka 1958 mpaka huu uliofanyika Oktoba 25, 2015. Ni uchaguzi wa takribani mara ya 15. Tulianza mwaka 1958, 1959, 1960, 1962, 1965- 2015). Hivyo tunao uzoefu wa kutosha katika mambo haya ya uchaguzi. Tusijidharau, bali tuendeleze uzoefu wetu huo.

  Kumejitokeza tabia moja ninayoweza kusema ni ya ajabu kidogo. Baadhi ya vyama vya siasa hasa vya upinzani, vimekuwa na katabia ka kujigamba, kujitunisha na kujiamini kuwa chama chao kitashinda tu. Tabia hii imejitokeza kuanzia uchaguzi wa 1995. Katika uchaguzi wa mwaka ule Chama cha NCCR-Mageuzi, walijitokeza na sare za NCCR-Mageuzi na wakavaa na wakatamba barabarani kuwa Augustine Mrema ni “RAIS”, watashinda kwa kishindo.

  Ilipokuja siku ya uchaguzi, mimi ningali nakumbuka katika Wilaya ya Temeke, walimpa wakati mgumu sana aliyekuwa “Returning Officer” wa wilaya hii. Hapa Temeke kulitokea fujo na ghasia hata mabomu ya machozi yalipigwa maeneo ya Uwanja wa Taifa.

  Vijana wa NCCR-Mageuzi kwa imani potofu eti wamedhulumiwa ushindi, “Rais” wao hakuchaguliwa kwa sababu ya wizi wa kura wakageukia kufanya fujo pale ofisi ya wilaya. 

 Tume ya Uchaguzi ilipotangaza matokeo ya uchaguzi, ilitoa takwimu hizi; kati ya wapigakura waliojiandikisha 8,928,826, waliojitokeza na wakatumia ile haki yao ya kupiga kura walikuwa watu 6,846,681. Hii ni sawa na asilimia 77 ya wenye haki ya kupiga kura.

 Mgombea wa CCM alikumba kura 4,026,422 na yule “Rais” mtarajiwa wa NCCR-Mageuzi aliambulia kura 1,808,616 tu. Wagombea wengine kama mgombea wa CUF alitoka na kura 418,973 wakati mgombea wa UDP aliambulia kura 258,734.

  Kura zilizoharibika na zikaonekana ni 333,936. Hapo, upinzani waliojigamba na kutamba sana kwa sare na mabendera ya chama chao wakabaki kutweta kwa mshangao. Kimetokea nini hadi tushindwe vile? Walijiuliza! 

  Baada tu ya uchaguzi ule, NCCR-Mageuzi ilisambaratika. Wasomi kama akina Mabere Marando, Masumbuko Lamwai wakajiondokea. Leo, hii ni mzee James Mbatia tu, ndiye mwasisi aliyeng’ang’ania kukikumbatia chama kisife kifo cha mende hapa nchini.

 Kinajikongoja pamoja na mitafaruku kadhaa ndani ya chama hicho mpaka leo bado kinafurukuta angalau kugombea ubunge, lakini siyo urais. Wazo hilo la urais wana NCCR-Mageuzi wameshalisahau.    Katika uchaguzi huu wa Oktoba 25, 2015, Mheshimiwa James Mbatia amegangamala kule Vunjo hadi ameupata ubunge kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Anastahili pongezi kwa kuwa na msimamo usioyumba. Ana imani na itikadi ya NCCR-Mageuzi. 

  Nimeelezea uchaguzi wa 1995 kwa sababu ndiyo uliokuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi katika nchi yetu baada ya Serikali kuachana na ule ukiritimba wa chaguzi za chama kimoja. Kadhalika, yalikuwa matakwa ya wengi kuwa nchi hii sasa iwe na mfumo wa uchaguzi wa kimataifa wenye ushindani wa vyama kadhaa. Ndiyo demokrasia ya kweli haina mawaa. 

  Pili, sijui wangapi bado tunakumbuka kuwa uchaguzi wa mwaka 1995 ulifanana kinamna na ule uchaguzi wetu wa kwanza katika nchi hii mwaka 1958. Nasema ulifanana kwa maana chaguzi hizi mbili zilifanyika katika awamu mbili. Mwaka 1958 ulifanyika uchaguzi awamu ya kwanza katika majimbo 5 tu ambayo yalikuwa Nyanda za Juu, Magharibi, Mashariki, Tanga na Kaskazini. Kwanza ulifanyika Septemba 8 mpaka 10, 1958. Awamu ya pili uchaguzi ulifanyika kuanzia Februari 9 na kumalizika tarehe 17/2/1959. Huu ulihusisha majimbo ya Dar es Salaam, Kusini, Ziwa Mashariki, Ziwa Magharibi na Jimbo la Kati. 

 Kumbe mwaka ule 1995 uchaguzi ulifanyika katika tarehe mbili tofauti. Mara ya kwanza ulifanyika Oktoba 29 na mara ya pili ulifanyika Novemba 29 ndiyo maana hapa nimesema chaguzi hizo zimefanana kwa namna zilivyoendeshwa tu, na siyo vinginevyo. 

 Nisingependa kuelezea uchaguzi wa 2000 kwa vile haukuwa na mvuto wa ushindani wa kinyang’anyiro cha urais kama ilivyokuwa mwaka ule 1995 na mwaka 2005, 2010 na hata mwaka huu wa 2015. 

  Mwaka 2005 tukawa na Uchaguzi Mkuu tena wenye jazba na ushindani mkubwa. Huu ulikuwa na mtazamo wake. Kikalenda, uchaguzi ule ungefanyika mwezi Oktoba, lakini kutokana na sababu zisizotarajiwa (kifo cha mgombea mmoja wa chama fulani) ulisogezwa mbele hadi Desemba 14, 2005.

 Safari hii mvutano mkubwa ulikuwa kati ya chama tawala CCM na Chama cha Wananchi (CUF). Hapo kinyang’anyiro cha mwaka ule kilijikita kati ya mgombea wa CCM na yule mgombea wa CUF. Dar es Salaam palishindia kwa vituko.

 Maeneo ya Zakhem huku Temeke mgombea urais kwa tiketi ya CUF alishaitwa “Rais”. Kuna siku risasi zilivurumishwa kule Zakhem hata mgombea urais na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ilisemekana, walinusurika katika patashika ile. Tunamshukuru Mungu.

 Jambo ninalokumbuka wazi ni madai ya CUF kwamba Tume ya Uchaguzi haikuwa huru na hivyo wanahofia kupokonywa ushindi wao uliokuwa dhahiri mwaka ule. Ilifika wakati wana-CUF wakitembea na ‘mijisu’ (visu) mikubwa mikubwa yenye mipini ya rangi nyekundu na bluu.

 Wakati huo vijana wa CUF wakaibuka na neno “NGANGARI” yaani kusimamia imara kura zao zisiibwe. Hapo ndipo Polisi wakataka kuonesha wao ndiyo pekee wenye jukumu la kulinda watu na mali zao katika nchi hii. 

  Kama sikosei Mkuu wa Polisi siku zile akaja na neno “NGUNGURI” kwa kuonesha iwapo vijana wa CUF wataendelea na madai yao ya kulinda kura zao watapambana na wanausalama, wana NGUNGURI kuwadhibiti hao vijana wa CUF. Uchaguzi wa mwaka 2005 ulifanyika tarehe 14 Desemba huku Bara wakati kule visiwani ulifanyika tarehe 30 Oktoba. 

 Tume ya Uchaguzi ilipotangaza matokeo yalikuwa hivi;-

Mgombea wa CCM alipata kura 9,123,952 huku yule “Rais” mtarajiwa mgombea wa CUF pamoja na majigambo na mbwembwe nyingi aliambulia kura 1,327,125. Ndugu yangu wa Chadema, mwasisi wa kaulimbiu “People’s Power”, akaangukia kura 668,756 tu. Tangu uchaguzi ule ndugu huyo hana hamu tena ya kugombea huo urais.

Yeye yuko tayari kuwapigia debe wengine waombe urais mradi asiondolewe kwenye uenyekiti wa Chadema maana inasemekana ni kiti cha urithi kutoka baba mkwe wake aliyewahi kutamka, hatavumilia kuona watu wasiojulikana wanaongoza chama chake.   Kati ya wapigakura milioni 15 wa mwaka ule 2005, ni wapiga kura 11,365,477 tu waliojitokeza kutumia hiyo haki yao ya kumchagua rais wa nchi yetu. 

  Hapa tena ubabe na majigambo ya wapinzani hayakuleta ushindi tarajiwa. Wakabaki kuelekeza lawama zao kwa Tume ya Uchaguzi eti haikuwa huru. Wamedhulumiwa kura zao. Lakini tofauti kati ya mshindi wa CCM kwa kura milioni 9 kwa zile milioni 1 za CUF ni wizi wa namna gani huo wa kukumba mamilioni yote hayo? Upinzani wanapaswa kukaa na kujiuliza inatokeaje?

 Kadhalika, wasishabikie kutumia vijana kutoa vitisho kwa wapiga kura. Kwa hofu ya ubabe wa mabaunsa wao, wapiga kura wanasema, kama utawala wenyewe ni wa namna ya hawa wanaotutisha, wenye fujo na wagomvi, afadhali tuipigie kura hiyo hiyo CCM yetu tuliyoizoea! Kwa mtazamo hasi namna hiyo CCM wanapata kura hata kutoka kwa wapinzani. Hili nalo liangaliwe. 

 Katika uchaguzi wa mwaka 2010 ndiyo mambo yalizidi kukorogeka. Hapa upinzani walikamia kuiondoa CCM Madarakani. Wakawa na mbinu mpya. Hii ilikuwa kulalamikia Tume ya Uchaguzi iundwe upya na upinzani washirikishwe. Hiki ni kichekesho, maana yake uundwaji wa Tume hizi unafanyika kwa mujibu wa Katiba.

 Rais hakurupuki tu kuteua wajumbe wa Tume fulani. Hilo wazo shirikishi la upinzani ni kwa mamlaka gani? Waombe au hata wadai haki wasiyostahili kikatiba? Hakuna andiko linalompa mamlaka rais wa nchi ati ashirikiane na upinzani katika uteuzi wowote ule kwa kazi za madaraka. Dai namna hiyo ni ulalamishi usiokuwa na msingi. 

  Mwaka 2010 tulijiandikisha wapiga kura 20,137,303 lakini tuliojitokeza kupigia kura kwa rais wa Jamhuri, wabunge na madiwani tulikuwa watu 8,626,283 tu. Wengine wale 11,511,020 kwa nini hawatumia hiyo haki yao ya kuchagua viongozi wao? Mimi sijui na wala sitaki kujua.

  Hisia yangu, waliogopa vitisho vya wapinzani. Wakaamua kubaki majumbani ambako maisha yao ni salama. Ndiyo sababu hawakujitokeza kwa wingi. Kumbe ubabe una matokeo hasi kama hilo la kutokujitokeza kwenda kupiga kura kwa kuogopa au kupwelea kudundwa na wahuni. 

  Kulikuwa na visingizio na matamshi ya uongo mengi kutoka upinzani. Uvumi na uzushi vilitawala. Nakumbuka kuna wakati mgombea urais kutoka Chadema alivumisha kuna kontena kutoka Afrika Kusini limekamatwa Tunduma linaleta karatasi za kura tayari imepigwa upande wa CCM. Mwisho wa siku, ilithibitishwa lile lilikuwa ni kontena la vipodozi mali ya mfanyabiashara fulani tu.

  Kulikuwa na vitisho vya mauaji au kupigwa wakati wa uchaguzi ule. Fujo na vitisho namna hii wananchi wanaogopa sana kujitokeza na kupigia kura wapinzani. Lakini matokeo yakitangazwa upinzani wanakuwa mstari wa mbele kulalamikia Tume na vyombo vya Serikali.  

  Uchaguzi ulifanyika Oktoba 31, 2010 na Tume ya Uchaguzi ikaja na matokeo namna hii pale Ukumbi wa Karimjee. Kama sikosei, viongozi wa Chadema hawakuhudhuria matangazo ya pale Karimjee. 

  Mgombea urais wa CCM alipata kura 5,276,827, yule mgombea wa Chadema alibahatisha kupata kura 2,271,491. Huku ndugu yangu Mnyamwezi wa Tabora anayejaribu mara ya tatu kutafuta huo urais wa nchi kwa tiketi ya Ngangari-CUF alibaki na kura 695,667 tu chini kabisa ya zile alizopata mwaka ule 2005.

 

>>ITAENDELEA