Rais Dk. John Magufuli, ameianza wiki yake ya kwanza ya uongozi kwa kuwapa faraja Watanzania.

Toleo lililopita tuliandika mambo kadhaa ambayo tuliamini Mheshimiwa Rais angeanza nayo.

Baadhi ya mambo hayo ni kuwashughulikia wakwepa kodi wakuu, kupigwa marufuku kwa safari za nje ya nchi, na utendaji kazi wa Wizara ya Fedha pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Tunashukuru kuwa Mheshimiwa Rais ameweza kuzikonga nyoyo za Watanzania wengi kwa hatua alizokwishachukua ndani ya saa chache tangu alipoapishwa.

Kama nilivyosema kwenye makala zilizopita, Rais Magufuli, si kiongozi wa kumweleza nini Watanzania wangependa kukiona au kukisikia kutoka kwake. Miaka yake 20 serikalini anajua mengi-mazuri na mabaya.

Sisi ambao tuko pembeni tunachopaswa kukifanya ni kumkumbusha na kumtia moyo. Hatuna sababu ya kumbeza Rais aliyepita, na wala huo si utamaduni wa Kiafrika, lakini tuna wajibu wa msingi wa kumsema kwa sababu, ama alishindwa kuongoza, au alipuuza mengi aliyoambiwa na wanaolitakia mema Taifa letu.

Wajibu huo wa kuyasema mambo yaliyoikwamisha nchi yetu kimaendeleo tutayasema kwa sababu ni wajibu weru halali kwani tunafanya hivyo kwa sababu ya mapenzi yetu kwa nchi yetu.

Rais Magufuli ndiyo kwanza ameanza. Atasikia mabaya kutoka kwa wale waliomtangulia; lakini kwa bahati nzuri atasikia mengi mazuri kutoka kwa maelfu kwa mamilioni ya Watanzania waliokuwa wamekatishwa tamaa na mtangulizi wake.

Sina sababu ya kurejea suala la safari za viongozi na watendaji nje ya nchi. Hili tumelisema sana. Mara kadhaa waliosafiri nje ya nchi wanaeleza fedha za um ma zinavyotumbuliwa. Ukitaka kukutana na viongozi wa Watanzania wanaosafiri, basi upite katika viwanja vya Heathrow, Dubai, Schiphol (Amsterdam), na kadhalika. Maofisa, viongozi wa Serikali, watumishi wa mashirika ya umma na wengine, wanapishana tu.

Misafara mingi ya mtangulizi wa Dk. Magufuli, watu walilala katika hoteli za nyota tano, au waliokosa, walilala hoteli za nyota nne! Japo hata mimi nina shauku ya kulala katika hoteli zenye hadhi hiyo, lakini kuna maana gani kufanya hivyo kwa uchumi huu tulionao? Kwanini wasaidizi wa rais, waandishi wa habari na watumishi wengine wasilale hoteli nafuu lakini zenye hadhi? Nani mwenye akili timamu anaweza kufurahia maisha ya fahari ilhali akitambua kuwa ameacha watoto wa Tanzania wakiketi chini kwa kukosa madawati?

Nani mzalendo anaweza kukubali kustarehe kiasi hicho ilhali akitambua wajawazito wanalala wawili katika kitanda kimoja, na wengine hawana kabisa vitanda? Nani anaweza kutushawishi hata tushindwe kuamini kuwa shida zinazoipata jamii yetu ni shida zinazosababishwa na aina hii ya matumizi mabaya ya fedha za umma?

Rais Magufuli, kwa uamuzi wake wa juzi wa kupiga marufuku utitiri wa safari za nje, Watanzania wameburudika mno; na kwa hakika wanamwombea kwa Mungu aizidi kusonga mbele. Nimeperuzi kwenye mitandao ya kijamii na kusoma baadhi ya wachangiaji wakisema akiendelea hivyo, hawana sababu ya kuendelea kuwa wapinzani! Mimi nasema waendelee kuwa wapinzani, lakini kwa upinzani wenye hoja kwa sababu kupitia kwao Rais atapata mengi ya maana na hivyo atapaswa ayafanyie kazi.

Nimesikia wengine wakisema aongezewe ulinzi kwa sababu atagusa maslahi ya majizi wengi waliyokubuhu. Pale aliposema “Watanzania mniombee”, bila shaka yeye mwenyewe alilijua hilo. Ulinzi imara unatoka kwa Mungu.

Wapo wanaomtaka Rais aende mbali zaidi. Ahakikishe kila wizara na idara zinakuwa na magari ya pool. Wanatoa mfano wa maofisa wanaohudhuria vikao vya Bunge Dodoma. Wanahoji, kuna ulazima gani kila ofisa kuwa na Land Cruiser au Nisan? Kwanini wasisafiri kwa basi maalumu, na wakishafika Dodoma walitumie hilo moja? Hapo kuna pointi muhimu. Rais Magufuli lisikie hilo pendekezo.

Wapo wanaoamini kuwa “kufukua makaburi”, kwa maana ya kuanza kuhoji nani kafanya nini wakati wa uongozi uliopita, si jambo jema. Hofu yao ni kwamba anaweza kuibua visasi.

Mimi si kati ya wanaoamini hivyo. “Kufukua baadhi ya makaburi” ni jambo la lazima. Kwa mfano, hivi karibuni kuna kampuni imetajwa sana kwenye ukwepaji kodi ya mabilioni ya shilingi. Wenye kampuni hiyo kwa kutambua kuwa Dk. Magufuli, atakuwa Rais, wamejitangaza mufilisi! Wanaowafahamu wanasema hiyo ni danganya toto kwa sababu wapo kwa staili na majina mengine. Wamesoma alama za nyakati na kutambua kuwa Dk. Magufuli hatakuwa na simile na watu walioliumiza au wanaoliumiza Taifa.

Hiki wanachokifanya hakina tofauti na mtu aliyeua watu, lakini baada ya kutambua kuwa atashitakiwa na hatimaye kuadhibiwa, akaamua kubadili jina. Mtu hawezi kukwepa hukumu inayotokana na uhalifu wake eti kwa sababu tu kabadili jina au kajizulia kifo!

Vyombo vya dola makini vinapaswa kufuatilia na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kuamuriwa walipe kodi zote walizokwepa wakati wakifaidi pepo waliyopata chini ya Serikali ya Awamu ya Nne.

Kama kina Mzee Daniel Yona na Basil Mramba, wamefungwa kwa makosa waliyotenda wakati wa uongozi wa Awamu ya Tatu, hawa wengine wanusurike kwa vigezo vipi?

Kuwashughulikia hao si kulipiza kisasi wala “kufukua makaburi”, isipokuwa ni kuonyesha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuufanya utajiri wa Tanzania uwe kwa ajili ya Watanzania. Madikteta na majizi wa Afrika, wakiwamo kina Sani Abacha wa Nigeria na Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire, walipofariki dunia, ukwasi wa wananchi wao waliouficha ulirejeshwa kuwanufaisha wananchi. Hakuna aliyesema kufanya hivyo ni “kufukua makaburi” na kwa maana hiyo ni kuhatarisha amani na utulivu.

Pia hapa kwetu hatuwezi kuwafumbia macho watu wanaojulikana wazi kuwa wameliibia Taifa kwa kiwango cha kusababisha adha kubwa kwa wananchi. Wala hatupaswi kusubiri wafe ndipo tuhoji na kuzitaifisha mali zao. Hao wanapaswa wachukuliwe hatua za kisheria ili warejeshe mali walizowaibia Watanzania.

Rais Magufuli ni jasiri. Sifa hiyo pekee inatosha kumtofautisha na mtangulizi wake aliyeamini ili awe kiongozi mzuri, basi lazima apendwe; na yeye amfurahishe kila aliye karibu yake au familia yake.

Kuna watu wamepata vyeo katika Serikali kwa sababu walijipendekeza kwake au kwa watu wa karibu na familia yake. Kuna ndugu waliokosa nafasi za ubunge wakapewa ukatibu wa chama kama njia ya kuwapoza. Uongozi wa chama na nchi ukawa ni mali ya kifamilia. Watanzania hawatarajii kuliona chini ya Rais Magufuli.

Kiongozi anayetaka kumfurahisha kila mtu, huyo hawezi kuongoza. Kiongozi mzuri ni yule anayeyatazama na kuyalinda maslahi ya walio wengi. Achukiwe na wezi 10, lakini apendwe na Watanzania milioni 10.

Siku za mwisho mwisho za uongozi wa Mheshimiwa Kikwete, tumeona uteuzi ambao si rahisi kuuelezea. Siku moja kabla ya kuondoka madarakani aliendelea kuteua!

Uteuzi huu unaweza kutafsiriwa kwa namna nyingi. Unaweza kuwa ni mpango wa kulipa fadhila. Unaweza kuwa ni upendeleo kwa ndugu, jamaa na marafiki zake. Unaweza kuwa ni mpango wa kumkomoa Dk. Magufuli ili asijue pa kuanzia. Katika hali ya kawaida wananchi hawakutarajia kuona wala kusikia uteuzi wa wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, wakuu wa mashirika ya umma na viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali.

Rais Magufuli, asipate kigugumizi. Kama alivyosema pale Uwanja wa Uhuru siku akiapishwa; yeye ndiye Rais wa Tanzania. Yeye ndiye mwenye uamuzi wa kuunda timu anayoamini itamsaidia kutekeleza yale aliyowaahidi Watanzania. Asisite kupangua uteuzi uliofanywa na mtangulizi wake kwa hofu ya kumuudhi! Hatutaki watu wafikie hatua ya kusema “afadhali ya Kikwete”.

Wananchi waliposema wanataka mabadiliko hatakumaanisha wanataka mabadiliko ya mchuzi au nguo. Walitaka mabadiliko ya uongozi kuanzia kwenye aina ya hao wanaoteuliwa.

Walitaka mabadiliko ya kuona watendaji wa umma wanabadilika na kuwaona wananchi ndiyo waajiri wao wakuu. Wametaka mabadiliko ya kuona mtu anayeteuliwa kushika wadhifa fulani, kweli anaipata nafasi hiyo kwa sababu anaimudu, na si kwa sababu ni rafiki au mfunga viatu vya mtoto wa rais.

Wanataka mabadiliko ya kuona uongozi haupatikani kwa njia ya udalali, kwa maana ya yule anayejipendekeza au anayeahidi kurejesha fungu, anapewa nafasi!

Nimesema tangu awali kuwa wajibu wetu wananchi sasa ni kumsaidia Rais Magufuli kadri inavyowezekana.

Miongoni mwa mambo tunayopaswa kumsaidia ni kumtajia watu tunaodhani hawafai kuwamo kwenye uongozi. Haya tunayasema si kwa sababu tuna wivu au ugomvi, la hasha! Tunayasema kwa sababu kama raia wa nchi hii, tuna wajibu halali wa kushiriki kuijenga nchi yetu – kwa ushauri na kuonya-kila mmoja kwa kadri ya mahali alipo.

Sisi tulio kwenye uandishi mchango wetu muhimu kwa sasa ni kumweleza Rais madudu yaliyofanywa na yanayofanywa na watu ambao kwa wazi kabisa sasa hivi wanaonekana kujiependekeza ili waingie kwenye uongozi, hasa Baraza la Mawaziri.

Pengine leo nihitimishe kwa kumuomba Mheshimiwa Rais afanye jambo muhimu kama lile alilolifanya katika Wizara ya Fedha. Bila shaka kwenye mipango yake bado amenuia kuzuru wizara nyingine.

Siwezi kuianza Jumanne ya leo vema bila kumwomba Mheshimiwa Rais afanye ziara katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Takwimu zinaonesha kuwa utalii kwa mwaka 2013 ulichangia pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 18; na kutoa ajira za moja kwa moja 466,830 na zisizo za moja kwa moja kwa watu 1,338,000. Idadi hii ni asilimia 10 ya ajira zote nchini kwa mwaka 2014. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Utalii ndiyo chanzo nambari moja cha mapato ya fedha za kigeni, ambako mwaka 2014 uliingizia Taifa dola bilioni 2 za Marekani.

Idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Idadi ya watalii mwaka 2011 ilikuwa 867,994 lakini mwaka 2014 idadi hiyo ilipanda hadi watalii 1,140,136.

Tanzania ni miongoni kwa nchi tano katika Bara la Afrika zenye fursa ya kuimarika kwa utalii wake katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Mataifa mengine ni Botswana, Cape Verde, Namibia na Afrika Kusini.

Wizara ambayo inachangia pato ya Taifa kwa asilimia 18 si ya kufumbiwa macho hata kidogo. Bahati mbaya, hii wizara kwa miaka miwili imekabidhiwa viongozi wakuu hatari. Ikafikia hatua kukawa na utatu-hatari (Lazaro Nyalandu, James Lembeli na Peter Msigwa). Ukiona watu wanaopaswa kuibana Serikali wanaungana -lao likawa moja, hapo ujue kuna kitu kisicho cha kawaida.

Mheshimiwa Magufuli asikubali kamwe Wizara ya Maliasili na Utalii inayoingizia Serikali mapato ya asilimia 18 ikaangukia mikononi mwa wezi na wahujumu uchumi. Leo mmoja ameanza kujitapa hata anajiona ana sifa za kuwa Waziri Mkuu! Huyu ni kati ya wengi ambao muda walistahili wale wanahojiwa kwa kuliumiza Taifa. Ushahidi wote wa wizi, uvunjaji wa kanuni, sheria na uonevu uliofanywa na Nyalandu na genge lake tunao. Tupo tayari kuuwasilisha Ikulu. Kama Katibu Mkuu Kiongozi yuko tayari, na atuite tumpatie leo. Hapa ni Kazi tu. Hatuna muda wa kupoteza.

1495 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!