Nianze kwa kuwapongeza Watanzania kwa namna ambavyo tumejipangia maisha ya uongozi na kuwa mfano mzuri wa kuigwa barani Afrika, tunatoa fundisho kwa wengine kwa kupitia mifano halisi, rais anaondoka madarakani akiwa na furaha tele moyoni na kumkabidhi mwenzake kijiti cha urais kwa moyo mkunjufu kabisa.

Nawapongeza marais wastaafu wote; naanza na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye siku alipomwachia madaraka Ali Hassan Mwinyi, alikaa mbali na mtawala mpya na kumpa heshima ya rais katika Uwanja huo wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Kila mtu alishangaa na kumuona kama vile Mwalimu ameacha kitu kikubwa sana katika maisha yake.

Iliwachukua watu muda kukubaliana kwamba Rais wa Tanzania ni Alhaj Mwinyi. Eti Mwalimu aliondoka Ikulu na kwenda moja kwa moja Mwitongo kupumzika, alikuwa akilima shamba lake la mahindi na kufuga ng’ombe wa maziwa aliopewa na jeshi letu la wananchi.

Baada ya muda tulizowea na kukubali kuwa Julius kaondoka madarakani na kwamba Rais ni Mwinyi almaaruf kwa jina la Mzee Ruksa, naye pia kwa mtindo uleule alimkabidhi nchi mzee wa Ukweli na Uwazi kwa mtindo uleule wa kupokezana vijiti. Ni uwanja wa Uhuru alipotua mzigo kwa mwenzake naye akarejea Tandika kupumzika.

Mkapa naye baada ya Kikwete kuapa, aliteremka ngazi na kuondoka huku akisema anajisikia fahari kwenda kupumzika baada ya kuitumikia Serikali yake ya Awamu ya Tatu kwa nguvu zake zote. Alishuka ngazi kutoka katika kile kidimba kama raia wa kawaida kabisa na hakuondoka kwa mbwembwe zozote pale uwanjani, amekuwa akionekana mitaani kama ilivyo kwa Mzee Mwinyi, wanashiriki masuala ya kijamii kama wananchi wengine lakini kizuri zaidi wamekuwa watiifu kwa Serikali iliyopo madarakani na hakuna anayevunja sheria kwa kigezo cha kuwa rais hapo awali.

Wiki jana, Kikwete naye akiwa na sura ya bashasha ya ajabu kaja mwenyewe Uwanja wa Taifa kukabidhi madaraka huku kavaa suti yake na kaambatana na mkewe kukubali kutoka Ikulu, lakini ni huyu huyu Kikwete kama ilivyokuwa kwa Mkapa, Mwinyi na Nyerere, ndiye aliyezunguka nchini kumnadi mpokezi wake wa kiti cha urais pasi na kutaka kuendelea kubaki madarakani. Kuna kitu kikubwa cha kujifunza hapa.

Wakati Kikwete akija kuachia ngazi ya juu kabisa nchini kimadaraka, walikuwapo viongozi mbalimbali kutoka nchi jirani ambao wengi wao walifanya kazi na Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete lakini bado wapo, hawa wangekutana na mpiga debe mmoja wa CCM angewananga vizuri sana, viongozi hawa wengi wao walikuwa wakijaribu kudadisi demokrasia yetu katika kipindi hiki cha kampeni na walisahau kuwa wao wapo na bado watakuwapo hata awamu ya Magufuli itakapokwisha.

Sina hakika walikuwa na mpango gani na Taifa letu, labda kutuingiza katika migogoro ya amani ama kutafuta uhalali wa kwao kuwapo madarakani kwa sisi kuwa kigezo cha uhalali wao, mimi nasema washindwe na kamwe Tanzania haitakuwa kama wao na hata wakiwekeza fedha katika vurugu sisi tutazijua na tutazitumia bila kujali watumiaji wana akili gani, sisi uongozi wetu ni miaka kumi kikatiba na tunamchagua kiongozi kwa kura na busara yake. Tanzania kwanza vyama baadaye.

Sasa tumeingia katika awamu nyingine ya ‘sasa kazi tu’. Hii ni awamu ambayo mimi nilikuwa nikiisubiri kwa hamu, inanikumbusha awamu ya kwanza ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Tanzania kumiliki rasilimali zake, Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Tanzania ya usawa na haki, Tanzania ya kila mtu kuwa sehemu ya maendeleo.

Inanikumbusha Tanzania yetu ya kufanya kazi na siyo biashara kuwa mfumo wa maisha, Tanzania ya nguvukazi kama kaulimbiu, Tanzania ya kilimo na Tanzania ya uhujumu uchumi, Tanzania ya kujitegemea, Tanzania ya kiongozi mkali lakini mwenye hekima, Tanzania ya demokrasia ya kweli na siyo demokrasia ya kutegea kazi na kuendeleza vijiwe ambavyo ni mwanzo wa uvunjifu wa amani.

Inanikumbusha Tanzania ya uzalendo, nahisi itafika, Tanzania ya kuheshimiana, Tanzania ya kujituma, Tanzania ya kazi chini ya John Pombe Magufuli. Wengi wana matumaini na wewe hata mimi nina matumaini na wewe, hebu ioneshe dunia kwa niaba ya wale wachache waliokuja siku ile unaliyoapa.

Waoneshe hata wale ambao kidemokrasia hawakukupigia kura kwa misingi na itikadi zao. Nasikia wewe ni tingatinga lakini mimi nakuona kama role model wangu kiutendaji.

 

Wasalaamu

Mzee Zuzu 

Kipatimo.

By Jamhuri