DODOMA

NA MWANDISHI WETU

Watanzania 60 wameukana uraia na hivyo kuwa raia wa mataifa mengine, Bunge limeambiwa.

Wakati Watanzania hao wakiukana Utanzania, wageni 135 wameomba na kupewa uraia wa Tanzania katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, mwaka huu; idadi ambayo ni ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2016/2017.

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Watanzania hao 60 walijipatia uraia wa mataifa mengine kama ifuatavyo: Australia (2), Botswana (4), Canada (3), India (4), Kenya (4), Lesotho (1), Norway (9), Sweden (1), Uganda (2), Uingereza (1), Ujerumani (19) na Zimbabwe (3). Katika kipindi kama hcho kwa mwaka 2016/17 Watanzania 35 ndio walioukana uraia wa Tanzania.

Kwa sababu hiyo, watu hao wamepoteza hadhi ya kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357 Rejeo la 2002.

Hayo yamo kwenye hotuba ya Dk. Nchemba, mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. HOTUBA KAMILI INAPATIKANA Uk. wa 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16 na 17.

Amesema wageni walioomba na kupewa uraia wa Tanzania kwa kipindi hicho na idadi yao kwenye mabano ni kutoka Burundi (4), Cameroon (2), China (1), Greece (1), India (83), Jordan (1), Kenya (1), Korea (1), Lebanon (2), Rwanda (2), Sierra Leone (1), Somalia (4), Uganda (2), Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (6), Yemen (23) na Zambia (1).

Dk. Nchemba pia amezungumzia marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Tanzania ya Uraia, Tangazo la Serikali Na. 427/2017 kwamba imetoa punguzo la ada ya uraia kutoka dola 5,000 za Marekani hadi Sh 2,000,000. Punguzo hilo la ada linawahusu waliozaliwa Tanganyika kabla na baada ya Uhuru ambao wazazi wao hawakutambulika kuwa raia wa Tanganyika kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya Tanganyika Sura Na. 512 ya mwaka 1961.

“Vilevile, Kanuni imejumuisha watu waliongia nchini Tanganyika kabla na baada ya Uhuru na kuendelea kuishi nchini kwa kipindi chote pamoja na watu waliozaliwa nje ya Tanzania kwa wazazi ambao ni raia kwa Tanzania kwa kuridhi. Hivyo, natoa rai kwa watu hao kurekebisha hadhi yao ya uraia ili kukidhi matakwa ya Sheria,” amesema Dk. Nchemba.

Usalama wa Makundi Maalum

 

Waziri Nchemba asema katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2017 hadi Machi, mwaka huu wazee/vikongwe 117 waliuawa, kati ya hao wanawake 26. Mkoa wa Tabora uliongoza ukifuatiwa na Songwe, Rukwa na Kagera.

Matukio hayo yalitokea katika mikoa ya  Arusha (6), Dodoma (1), Geita (9), Iringa (1), Kagera (10), Katavi (3), Kigoma (1), Mara (2), Mbeya (7), Morogoro (2), Mwanza (9), Njombe (5), Rukwa (10), Shinyanga (3), Simiyu (5), Singida (6), Songwe (12) na Tabora (25).

Amesema katika kipindi hicho, matukio mawili ya kujeruhiwa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa katika mikoa ya Morogoro na Tabora.

“Watuhumiwa 100 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Natoa rai kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo hivyo viovu vinavyokiuka haki za binadamu. Jeshi la Polisi litaendelea kudhibiti na kuzuia mauaji ikiwemo ya makundi maalum na kuendelea kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kwa umma ili kuacha mila na imani potofu,” amesema.

Katika katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, mwaka huu matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji 86 yalitokea na kusababisha vifo vya watu 44, kati yao wanawake wanne. Watu wengine 75 walijeruhiwa. Watuhumiwa 129 walifikishwa mahakamani.

Ununuzi wa Sare za Jeshi la Polisi

Dk. Nchemba amesema taratibu za ununuzi wa sare na vifaa vingine vya kijeshi kwa kutumia viwanda vya ndani zinaendelea baada ya Kiwanda cha 21st Century kilichopo Morogoro kuthibithisha uwezo wa kutengeneza vitambaa bora vya kushona sare.

Amesema Jeshi la Polisi linakamilisha mkataba wa ununuzi wa jozi 15,000 za viatu (buti jozi 10,000, viatu vya kawaida –‘staff shoes’ jozi 5,000) kutoka Kiwanda cha Viatu cha Jeshi la Magereza Karanga, Moshi.

Kwa upande wa kuimarisha doria, misako na operesheni maalumu na za kawaida, amesema Jeshi la Polisi limepokea magari 172 aina ya Ashok Leyland yakiwa ni sehemu ya ununuzi wa magari 777 kutoka nchini India.

“Magari hayo yatagawiwa katika Mikoa, Vikosi na Wilaya za Kipolisi. Pia, Jeshi la Polisi limepokea pikipiki 10 aina ya Tongba kutoka kwa wadau wa usalama wa Mkoa wa Dar es Salaam. Pikipiki hizo zimesambazwa katika Vituo vya Polisi katika kanda maalumu ya Dar es Salaam kwa kazi za doria za kuzuia makosa ya usalama barabarani,” amesema Dk. Nchemba.

INAENDELEA Uk.9

1203 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!