Wazee amkeni, simameni mseme

Ubaguzi katika nchi yetu umeanza kushamiri. Hatuhitaji mwalimu wa
kutuweka darasani kutufundisha kulibaini tatizo hili.

Kauli zinazotolewa na baadhi ya watawala (siyo viongozi), akiwamo Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, zimeanza kuzaa matunda. Sote tunatambua kuwa AMANI ni zao la HAKI. Kama hakuna haki, amani haiwezi kumea na kustawi.

Kuna mambo tunapaswa kuyazungumza kwa uwazi bila kujali tofauti zetu
za kiitikadi. Tanzania kwetu iwe ndiyo alfa na omega. Hivi vyama vya
siasa havikuwapo, vimekuwapo, na bila shaka yoyote vitapita, lakini
Tanzania itabaki.

Yaliyotokea Kinondoni ni cheche mbaya katika dumu la mafuta ya petroli.
Kutulia au kuenea kwake kutatokana na namna tunavyojipanga kukabiliana
na aina hii ya hatari inayotunyemelea.
Mwanafunzi mdogo kabisa wa mwaka wa kwanza ameuawa wakati polisi
wakidhibiti wanachama wa Chadema waliokuwa wakienda kudai haki yao
katika ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni. Polisi
wamemuua binti asiyekuwa na hatia; binti ambaye wazazi au walezi wake
walikuwa na matumaini ya kumwandaa asome ili baadaye awe na tija kwao
na kwa Taifa.
Tunaweza kuwalaumu polisi kwa kumuua huyu binti. Tunaweza kuwalaumu
walioandamana na hata kuwafanya polisi watumie risasi za moto kujeruhi
na kuua. Tunaweza kusaka wabaya wote kwenye tukio hili, lakini ukweli
ni kuwa tatizo hapa si polisi wala Chadema.
Ndiyo; tunaweza kusema tatizo ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la
Kinondoni ambaye kwa kujisikia kwake, aliweza kuona busara ya kutowapa
viapo mawakala wa Chadema. Tunaweza kumlaumu kwanini hakuwapa viapo
mawakala wa Chadema kama alivyofanya kwa wenzao wa CCM. Je, uamuzi wa
msimamizi huyu ni utashi wake tu wa kibinadamu au ni utekelezaji wa
mbinu zilizobuniwa na wakuu wake wa kazi ili kujitwalia ushindi hata
kama ni kwa kumwaga damu?
Kilichofanywa Kinondoni ni ubaguzi. Ubaguzi huu wa waziwazi hauwezi
kuwa na mwisho mwema, si kwa Kinondoni pekee, bali hata kwa nchi nzima.
Tunapanda mbegu mbaya. Kinachofanywa sasa na watawala hakina tofauti
na kile tunachokipata kwenye simulizi za chanzo cha ukimwi. Wale
walioingia maabara kutengeneza virusi vya maradhi hayo walidhani
waathirika wangekuwa weusi pekee, lakini matokeo ya ubunifu huo haramu
tumeyaona hata kama walioumia zaidi ni weusi.
Kama kuna kundi la watawala/viongozi wanaodhani kuwa dhambi hii
inayoundwa ni mahsusi kwa ajili ya wapinzani pekee, wanajidanganya.
Kama wapo wanaodhani kuwa Tanzania itaongozwa au kutawaliwa na upande
mmoja tu wa wanasiasa, hao ni wa kuonewa huruma. Daima hakuna
kisichobadilika, isipokuwa mabadiliko pekee.
Chama Cha Mapinduzi ambacho mimi ni shabiki wake, hakiwezi
kujihalalisha kwa mbinu na hila kwa imani kuwa kitaendelea kuongoza
milele.
Binadamu, kama walivyo bakteria na virusi, wana desturi ya kujenga
usugu. Kama si hivyo, basi leo tungekuwa na aina moja ya dawa ya
kutibu malaria. Hatuna dawa moja ya kuutibu ugonjwa huo kutokana na
usugu wa vimelea vya maradhi hayo.
Wananchi wanapozoea kupigwa mabomu (kwa uonevu) wanajenga usugu.
Wanaposhambuliwa kwa risasi hata kama hapakuwa na ulazima wa
kuzitumia, watazizoea na utafika wakati hawatahofu milio ya bunduki
wala risasi zake. Polisi wanapoona njia pekee ya kukabiliana na
‘maandamano’ wasiyoyataka ni kutumia bunduki, utafika wakati hata
mizinga haitafaa kitu kuwatawanya watu waliokwishakata tamaa.
Mamlaka za utawala zijiweke kando na mpango wowote uwao wa kuwajengea
usugu wananchi wake. Usugu huu unaweza kufika mahali kukakosekana
kinga au tiba ya kuukabili.
Watoto wadogo wanapoona dada zao, kaka zao, mama zao, majirani au
rafiki zao wakiuawa hawawezi kukua katika misingi ya kuwafanya
waipende dola. Watajenga chuki ambayo matokeo yake ni kuwa na Taifa
lililogawanyika kwa misingi ya ubaguzi.
Nchi hii imeshakuwa na watawala wengi kwa nyakati tofauti tangu zama
za kabla na baada ya ukoloni. Leo hawapo. Ulimwengu huu umeshakuwa na
watawala hatari na wenye nguvu ambao leo hawapo. Wanaosoma historia ya
dola ya Roma wanashangaa ilikuwaje wababe hao wakaondoka kwenye ramani
ya dunia. Wanaojua kanuni ya historia hawawezi kushangaa matokeo hayo!
Wamarekani watakuwa watu wa ajabu sana kuamini kuwa ubabe wao utadumu
milele. Wanaoamini hivyo wanajidanganya. Hatima ya maguvu yao ya
kiuchumi na kijeshi ipo tu hata kama ni kwa miaka 100 ijayo, lakini
bado tamati yao ipo tu. Hii ni kanuni ya historia isiyotokana na
utashi wa mtu au kiongozi.
Kama ulivyo utaratibu wa kubadili mboga, kuna wakati binadamu huwa
kama ‘kichaa’ akililia mabadiliko hata kama ni hatari kwake. Kuna
wakati binadamu hulazimika kubadilika kwa sababu ya kutaka mabadiliko
tu bila kujali, au kuzingatia matokeo ya mabadiliko hayo. Wale Walibya
walioungana na mabeberu kumng’oa mwanamapinduzi wa kweli, Muammar
Gaddafi, walifanya hivyo licha ya kupewa mahitaji yote ya kibinadamu.
Kwao, walichopata hakikuwa muhimu isipokuwa mabadiliko tu. Wapo
wanaojuta leo kama vile wasemavyo Waswahili ‘ningejua huja baada ya
tukio’.
Basi iwe ni wananchi wenyewe wanaoamua kufanya hivyo, na isiwe kwa
viongozi wa dola kuwalazimisha kuukana upendo na amani. Pamoja na
ukweli wa yote tunaoweza kuusema, amani na upendo miongoni mwa
Watanzania si kitu tu kilichojitokeza chenyewe kama wale wanasayansi
wanaopenda kusema ‘nature’. Hakuna nchi au jamii iliyojijenga kwa
mfumo wa ‘nature’. Hakuna. Mwonekano wa jamii yoyote ni matokeo ya
uhunzi uliofanywa na watangulizi.
Tanzania ipo hapa ilipo kwa sababu wapo watu waliojitahidi kwa hali na
mali kufifisha mipango yote ya ubaguzi, upendeleo, dhuluma na uonevu
wa kila aina. Tulipoitana ‘ndugu’, hatukuitana hivyo kwa bahati mbaya,
bali ni kutokana na misingi ya makuzi iliyowekwa na wazee wetu.
Amani ni zao la haki. Nchi inakuwa na amani kama wananchi wake wanaona
wanatendewa haki. Haiwezekani katika mazingira haya ya watu wa chama
fulani kutendewa tofauti na wa chama kingine kukawapo amani. Huu ni
ubaguzi ambao yeyote awaye – awe wa chama cha Upinzani au wa chama
kinachotawala – anapaswa kuupiga vita.
Tutende mambo kwa kuweka akiba tukiamini kuwa ‘leo ni mimi, kesho ni
wewe’. Tuijenge Tanzania katika misingi ya gwaride ambako aliyeko
mbele sasa anaweza kuwa nyuma pindi inapotolewa amri ya kiongozi wa
gwaride.
Kama tumeridhia kujenga nchi ya kidemokrasia, kwanini tuhofu uchaguzi
ulio huru na wa haki? Kwanini Msimamizi wa Uchaguzi apendelee? Kwanini
walio na viti vingi wang’ang’ane kwa gharama ya damu kutwaa kiti
ambacho hata kikitwalia na upande mwingine hakiwezi kuwa na athari kwa
chama tawala?
Kwanini turuhusu polisi watumie silaha za moto kujeruhi na kuua watu
wasio hata na manati? Haya yanayofanywa na polisi mchana tumeyaona
yalivyo mabaya; je, yale wanayoyatenda mbali ya kamera na macho ya
Watanzania yanafananaje? Maguvu yote haya kwa maskini, makabwela
wanyonge ya nini? Huruma imewaishia Watanzania kiasi cha vijana wa
nchi hii kuwapiga raia wao bila huruma? Polisi wameishiwa na risasi za
plastiki na kusaliwa na za moto pekee?
Je, Tanzania tumeishiwa na statesmen? Kama wapo mbona hawasimami kukemea hatari hii inayolinyemelea Taifa?
Kule Manyara kuna kiongozi kasema hataki kuwaona madiwani wa upande
ule mwingine. Wazee wa Taifa wamenyamaza. Je, wanakubaliana na kauli
hizi za kibaguzi? Kama hawakubaliani nazo, kwanini hawazikemei na
kuzilaani? Je, uchama una maana gani kuliko utaifa? Je, hali hii
tuliyonayo sasa inatushawishi kuendelea kuamini katika demokrasia ya
ushindani wa vyama vingi vya siasa?
Watanzania wenye mapenzi mema na nchi yao wanapaswa kujitokeza
kuyalaani haya ya ubaguzi na mauaji yanayoanza kuota mizizi nchini
mwetu. Kukaa kimya maana yake ni kuyabariki. Dhambi hii ikishastawi
haitatuacha salama. Hebu tuwe wamoja kama watoto wa familia moja.
Turejee kuishi kwenye misingi iliyojengwa na wazee wetu – ya amani na
upendo. Tupingane na aina zote za ubaguzi hasa huu wa kiitikadi ambao
unakuja kwa kasi ya ajabu.
Tuamini kuwa waliopo madarakani leo, kesho wanaweza kuwa nje ya nafasi
hizo. Tujiwekee akiba njema ya baadaye kwa kuhakikisha haki
inatamalaki katika Taifa letu.
Inawezekana wakawapo wanaodhani kwa kuua au kuonea wanaufurahisha
uongozi wa juu wa Taifa letu. Wanajidanganya. Kama wanafanya hivyo kwa
kujipendekeza wajue damu zinazomwagika bila hatia zitawaumiza. Kwa
kulisema hili najiepusha kuwa sehemu ya wale watakaohukumiwa kwa
ukimya wao. Tumsaidie Rais Magufuli kwa kuyamekea haya.

 

Bado nauliza, Tanzania tumeishiwa na ‘statesmen’? Kama wapo, mbona wako kimya kana kwamba hawana redio, televisheni wala hawapati magazeti? Wazee wakemeeni wasimamizi wa uchaguzi. Wakemeeni viongozi wabaguzi. Wakemeeni watendaji wanaoivuruga nchi kwa kujipendekeza kwa wakubwa.  Wakemeeni polisi wamwaga damu. Wakemeeni wachinja Watanzania wasio na hatia.
Kemeeni maovu yote. Mkifanya hivyo huenda wahusika wakawasikia maana
maneno ya wazee ni dawa. Tushirikiane kuijenga Tanzania yenye usawa.