MBEYA

Na Mwandishi Wetu

Mapinduzi katika kilimo yanayoendelea nchini yameungwa mkono na wazee wa kimila mkoani Mbeya, wakiamini kuwa sasa taifa limo katika mwelekeo sahihi.

Mbali na kilimo, mapinduzi hayo yamegusa pia sekta za uvuvi na ufugaji kwa miaka mitano mfululizo tangu kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Mmoja wa wazee hao, Chifu wa Wasafwa, Rodrick Mwashinga, anasema uwekezaji unaofanywa na benki hiyo kwa wakulima na wawekezaji wazawa unamfanya kuwa na imani kubwa.

“Wawekezaji wanatoka katika jamii yetu wenyewe. Hili ni jambo jema sana kwetu. Uwekezaji wa TADB unadhihirisha nia njema ya kutuletea maendeleo ya kiuchumi kupitia kilimo, mifugo na uvuvi,” anasema Chifu Mwashiga.

Anatoa wito wa kuendelea kupanua wigo wa utoaji mikopo kwa wazawa waweze kujenga viwanda vingi, hivyo kuongeza ajira, uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi na kuchagiza maendeleo ya Mkoa wa Mbeya na uchumi wa taifa zima. 

Chifu Mwashinga ameyasema hayo wakati TADB walipotembelea Kampuni ya Raphael Group Ltd inayoshughulika na kuzalisha, kuchakata na kuuza nafaka eneo la Nyanda za Juu Kusini.

Awali, akikabidhi matrekta kwa wakulima wa mpunga wa Mbarali mkoani hapa, Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, naye alisifu juhudi zinazofanywa na benki hiyo, akitoa wito wa kujitangaza zaidi kwa wakulima.

“Kazi mnayoifanya inaonekana. Mwenye macho hapaswi kuambiwa tazama,” anasema Profesa Mkenda.

Meneja wa TADB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Alphonce Mukoki, anasema uwezeshaji ni moja ya michango yao mikubwa katika kuboresha sekya ya kilimo.

Kampuni ya Raphael Group Limited imewezeshwa kupata mashine ya kisasa yenye uwezo wa kuchakata tani 80 za mpunga kwa siku; mashine ya kukausha mpunga na mashine ya uhakiki na utengaji wa rangi (madaraja) ya mchele.

“Tunaendelea kutimiza azima yetu kama muwezeshaji namba moja kwenye kilimo, mifugo na uvuvi,” anasema Mukoki.

Mbali na mashine, benki imeipatia kampuni hiyo mtaji wa uendeshaji na ununuzi wa mpunga na maharage kutoka kwa wakulima wadogo zaidi ya 13,000 wa Mbeya na mikoa jirani.  

Ni wazi kuwa ununuzi utakaofanywa na Raphael Group Ltd utaongeza tija kwa wakulima wa Nyanda za Juu Kusini.

Mukoki anasema wamejiwekea malengo kuwawezesha wakulima na wawekezaji wazawa kuchagiza mageuzi ya kilimo na kuleta maendeleo ya kijamii kiuchumi.

“Ni benki ya maendeleo na malengo yetu ni kuwawezesha wakulima na wawekezaji wazawa kuwa na teknolojia ya kisasa na mtaji wa kuinua biashara zao, kisha kuleta manufaa katika mnyororo wa thamani,” anasema.

Anaahidi kuwa malengo hayo yatatekelezwa sambamba na kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, elimu na mikopo nafuu kwa wazawa wanufaike na fursa zilizopo TADB.

“Siku zote tuko tayari na mstari wa mbele kuweka mazingira mazuri kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kunufaika kupitia vikundi vyao,” anasema Mukoki.

Meneja Mkuu wa Raphael Group Ltd., Lazaro Mwakipesile, ameishukuru benki hiyo kuwafikisha walipo kwa sasa kibiashara.

“Tunawashukuru kwa kutuwezesha kupata mashine hizi za kisasa. Hakika tunachakata mazao kwa wingi zaidi ya ilivyokuwa awali.

“Ziara ya wazee wetu ambao ni viongozi wa kimila imekuja wakati muafaka na elimu waliyoipata kwa kushuhudia uwezeshwaji huu ni chachu kwao kwenda kuwapa darasa wananchi katika maeneo wanakotoka,” anasema Mwakipesile.

Anasema kwa kushuhudia kwa macho yanayoendelea kiwandani hapo, kunampa imani kuwa watarejea makwao na kuwa mabalozi wazuri kwa wakulima kutambua manufaa na fursa za kibenki.

“Juhudi za TADB zinapaswa kuungwa mkono. Tunaiomba serikali iendelee kuiwezesha na mikopo nafuu kama hii ipatikane kwa wengi kwani itachagiza maendeleo kwenye kilimo, mifugo na uvuvi,” anasema.

Naye anaungana na Chifu wa Wasafwa na Profesa Mkenda kuitaka benki kutoa elimu kwa wakulima wengi zaidi, akisema: “Sisi tumefanikiwa kupitia nyinyi ila ninaamini kuna idadi kubwa ya wenzetu bado hawajui fursa zilizopo kwenu, sasa niwaombe tu mjikite kwenye kuwapa darasa watu wengi waweze kunufaika.”

Diwani wa Itezi, Shambwee Shitambala, ameishukuru Raphael Group Ltd na TADB kuwapa nafasi ya kwenda kujifunza kuhusu ushirikiano na uwekezaji walioufanya katika mnyororo wa thamani wa mpunga ambao umeleta manufaa kwa wakulima wa Mbeya na Nyanda ya Juu Kusini.

“Ushirikiano huu utautangaza mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla kama kitovu cha kuzalisha, kuchakata na kuuza mpunga,” anasema Shitambala.

Amewataka wakazi wa maeneo ya karibu kutumia mafanikio ya Raphael Group kama somo kusudi kampuni kama hizo zizaliwe kwa wingi na kuwa alama ya mafanikio kwenye ustawi wa kilimo.

Raphael Group Ltd., ni moja ya kampuni zinazoongoza Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika kuchakata na kuuza nafaka aina sita tofauti. 

Mpunga unachukua asilimia kubwa zaidi (asilimia 50) ya biashara ya kuchakata katika kiwanda hicho, ikifuatia na maharage (asilimia 20), karanga (asilimia 10) na mahindi (asilimia 5).

Benki inaendeleza jitihada za mageuzi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na kutekeleza kwa vitendo Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano uliozinduliwa na serikali ambao umezipa sekta hizi kipaumbele.

Hadi Juni mwaka huu, benki hii imekwisha kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 30 katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini; mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma na Songwe, katika minyororo ya thamani 18, ikiongozwa na mpunga, kakao, mahindi na kahawa. 

Viongozi wa kimila Mkoa wa Mbeya katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Raphael Group Ltd..jpeg_061204

By Jamhuri