President Jacob Zuma addressing Investec Asset Management’s Global Investment Conference delegates in Cape Town.Picture: ESA ALEXANDER 05/07/2010

DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samsom Simbi

Kufikia mwaka 1960 baadhi ya nchi za Afrika zilikuwa zimepata uhuru na kuanza kujitawala zikiwa na jukumu kubwa la kutoa mchango wa hali na mali katika ukombozi wa Bara zima la Afrika.

Pamoja na mwaka huo kupewa jina la heshima la ‘Mwaka wa Afrika’, hatua mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa katika harakati za kulikomboa bara hilo kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Moja ya hatua kubwa iliyofikiwa Mei 1963 ni kuundwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) wenye jukumu la kuhakikisha Afrika inakuwa huru, yenye amani na kudumisha umoja miongoni mwa mataifa ya Afrika baada ya kutawaliwa na kunyonywa na mabeberu wa nchi za Magharibi kwa zaidi ya miaka 75.

Afrika Kusini ilitawaliwa na makaburu kwa muda mrefu sana kuliko nchi yoyote Afrika. 

Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wapigania uhuru wa Afrika, Nelson Mandela alifungwa jela kwa miaka 27 hadi alipoachiwa mwaka 1990.

Sababu kubwa ya kufungwa kwake ni msimamo wake madhubuti, akiwahakikishia kuwa mara tu atakapoachiwa huru ataendelea na harakati za kudai uhuru na haki za Waafrika.  

Kauli hii iliwakasirisha makaburu. Kwamba Mandela ana ujasiri na ubavu wa kuendelea kuwatetea wananchi wa Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi, kunyang’anywa ardhi, matabaka katika huduma za jamii kama elimu na afya na usalama wa raia.

Mandela alitolewa gerezani mwaka 1990 na akaendelea na harakati za ukombozi wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa dhahabu.

Hatimaye Afrika Kusini ilipata uhuru mwaka 1994 na Mandela kuwa Rais wa kwanza Mwafrika.

Akaitawala Afrika Kusini kwa miaka mitano na kuachia ngazi mwenyewe mwaka 1999.

Nchi ya kwanza kuitembelea baada ya kutoka gerezani Februari 1990, ni Tanzania, ambapo Machi 6, 1990, alihutubia taifa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam akikaribishwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Alifanya ziara hiyo kutokana na urafiki wake na Nyerere na kuthamini juhudi za kipekee za Mwalimu katika kusaidia ukombozi wa Afrika Kusini.

Rais Mandela alimuachia kijiti Thabo Mbeki aliyetawala kwa miaka tisa na miezi mitatu kabla ya kujiuzulu Septemba 2008.

Sababu hasa za kujiuzulu kwa Mbeki ni shinikizo la Halmashauri Kuu ya Chama (tawala) cha ANC. 

Pamoja na mambo mengine, alishutumiwa kwa kushindwa kusimamia au kutoa ushirikiano kwa Mahakama dhidi ya kesi ya msaidizi wake, Jacob Zuma, aliyekuwa akituhumiwa kwa ulaji rushwa katika mkataba wa ununuzi wa silaha uliohusisha Afrika Kusini na kampuni kadhaa za Ulaya.

Hata hivyo, Mbeki alikata rufaa na kushinda kesi hiyo Januari 12, 2009 ingawa suala la kujiuzulu kwake halikubatilishwa kwa mujibu wa sheria za Afrika Kusini.

Zuma aliyeonekana kuwa mpinzani akiwa Makamu wa Mbeki, alitumia hila na fitina dhidi ya Mbeki kwa kuwatumia wafuasi na viongozi wa juu wa ANC na washirika wake; Chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini (STACP) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Afrika Kusini (COSATU), kama mtaji na kummaliza kisiasa bosi wake, Mbeki.

Mbeki pia alilaumiwa na ANC kwa kushindwa kusimamia uchumi na uwekezaji, suala la ajira na kuonekana uchumi na biashara kuwaneemesha Wazungu na Waafrika wachache.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2009, Zuma alipigiwa debe na Julius Malema aliyekuja kufukuzwa uanachama baadaye na kuunda Chama cha EFF kilichoongoza kumdhalilisha Zuma bungeni miaka kadhaa baadaye.

Baada ya kufanikiwa kuingia madarakani, Zuma na wafuasi wake walimtenga Mbeki, wakitaka anyang’anywe kadi ya ANC; lakini hawakufanikiwa.

Kwa muda mrefu akiwa madarakani, Zuma aliandamwa na tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi, akishinikizwa kujiuzulu urais kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Thabo Mbeki.

Kama alivyo mfitini Mbeki, makamu wa Zuma, Cyril Ramaphosa, akaingia kwenye kampeni kuhamasisha kama si kushinikiza, Zuma aachie ngazi ili yeye apewe madaraka ya kuongoza nchi.

Ramaphosa alifanya kila linalowezekana kugombea urais wa Afrika Kusini, akionekana mwiba wenye sumu kwa Zuma, hasa alipokuwa mstari wa mbele kushinikiza hoja ya wabunge kutokuwa na imani na Rais.

Rais Zuma naye kwa kumfahamu vizuri makamu wake, alijiimarisha kwa kujiwekea ukuta imara wa kumlinda asijiuzulu hadi muda wake wa kuongoza utakapokwisha.

Juhudi za Ramaphosa na wapambe wake zilizaa matunda baada ya Zuma kushinikizwa kujiuzulu urais, akaridhia na kuachia ngazi Februari, 2018.

Baada ya Zuma kujiuzulu urais, makamu wake, Ramaphosa alichukua nafasi hiyo anayoendelea nayo mpaka sasa.

Hata baada ya kujiuzulu, Zuma aliendelea kukumbwa na misukosuko mbalimbali ikiwamo kufunguliwa mashitaka kwa kupokea rushwa na matumizi mabaya ya ofisi wakati wa uongozi wake.

Wafuasi wa Zuma, kwa nyakati tofauti, wameendelea kukana tuhuma hizo wakidai hastahili kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.

Juni mwaka huu, Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani kwa kosa la kuidharau mahakama baada ya kutofika kwenye mahojiano ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Zuma (79) hakuwapo kusikiliza Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ikitoa uamuzi na hukumu dhidi yake.

Jaji aliamuru Rais huyo wa zamani ajisalimishe mwenyewe ndani ya siku tano.

Zuma alishindwa kuhudhuria kwenye uchunguzi wa ufisadi uliongozwa na Naibu Jaji Mkuu, Raymond Zondo, Februari mwaka huu, kufuatia madai ya ufisadi wa kiwango cha juu uliofanyika wakati akiwa madarakani.

Amekana makosa hayo akidai Zondo ana chuki binafsi.

Siku hiyo ya hukumu, Jaji Sisi Khampepe, amesema: “Mahakama ya Katiba haiwezi kufanya chochote isipokuwa kuhitimisha kwamba Zuma ana hatia kwa kosa la kudharau mahakama.”

Uchunguzi wa ufisadi ulianzishwa na Zuma mwenyewe kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la wananchi kwenye kashfa hiyo muda mfupi kabla ya kuondolewa madarakani na ANC.

Hata hivyo, alitoa ushahidi mara moja tu; Julai 2019, kabla ya kupuuzia mialiko iliyofuata akitoa sababu za matibabu na maandalizi ya jaribio jingine la ufisadi.

Baada ya kuhukumiwa, Zuma alijitokeza hadharani kupinga hukumu hiyo akidai kuwa kufungwa akiwa na umri mkubwa wakati huu wa janga la COVID-19, ni sawa na kumhukumu adhabu ya kifo.

Pamoja na utetezi huo, Zuma alijisalimisha Kituo cha Polisi Jumatano ya Julai 25, 2021 na kuanza kutumikia kifungo chake katika Gereza la EstCourt, Jimbo la Kwa Zulu – Natal anakoishi.

Wakati Zuma akiwa gerezani, kumetokea ghasia katika majimbo ya Kwa Zulu-Natal na Gauteng, wafuasi wake wakiandamana na kuchoma magari, kupora maduka na kufunga barabara wakishinikiza kuachiwa kwa Mzulu huyo.

Rais Ramaphosa amewataka wananchi kuwa watulivu huku akiwaonya wanaotumia nafasi hiyo kupora na kuharibu miundombinu na mali watachukuliwa hatua kwa sababu vitendo hivyo huathiri uchumi.

Viongozi wengi wa Afrika wanatawaliwa na uchu wa madaraka na tamaa ya kujilimbikizia mali wakiwa madarakani. Wakati umefika sasa kwa viongozi wa namna hiyo kuelewa kwamba uongozi ni dhamana kwa ajili ya masilahi mapana ya nchi na wananchi wake.

Ofisa Mipango wa Taasisi ya Sema mkoani Singida, Jeremiah Masifia, amesema viongozi wanapaswa kuongoza kwa kuzingatia na kutii sheria za nchi.

0755985966.

By Jamhuri