Machi 26 mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alitangaza uamuzi wa Serikali wa kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo.

Waziri Kagasheki alifanya uamuzi wa kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500 na kuliacha eneo la kilomita za mraba 2,500 litumiwe na wananchi kwa kufuata Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009.

Alisema eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori. Baadhi ya faida za uamuzi huo ni kwamba eneo hilo ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, ni mapito ya wanyamapori na kuna vyanzo vya maji maji. Kwa kifupi ni kwamba eneo hilo linachangia sana kuimarisha mfumo wa ekolojia wa Serengeti.

 

Uamuzi huo haukufanywa kwa kukurupuka, bali ulihusisha wataalamu kama Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na tume nyingi. Mwaka 2010 iliundwa Tume ya Waziri Mkuu ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara tisa, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro na wadau mbalimbali. Moja ya mapendekezo yake yakawa kupunguza eneo la Pori Tengefu la Loliondo bila kuathiri mapito ya wanyama na vyanzo vya maji.

 

Baada ya tangazo la Waziri Kagasheki, kumeibuka makundi ya watu kadhaa kupinga mpango huo mzuri. Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo yamekuwa yakiishi kutokana na mgogoro wa Loliondo, ndiyo yaliyo mstari wa mbele.

 

Mgogoro wa Loliondo ni wa muda mrefu, na sasa ni vema Serikali ifike mahali isikubali kuongozwa na NGOs ambazo kwa bahati mbaya, nyingi ni za wageni. Kuna habari zisizotiliwa shaka kwamba madiwani zaidi ya asilimia 60 wa Ngorongoro, ama ni waajiriwa wa NGOs au ni watu wanaofaidika moja kwa moja kutokana na vurugu za Loliondo.

 

Tanzania ni nchi huru. Inashangaza kuona kuwa fedha za wafadhili kupitia NGOs zinaelekea kuifanya nchi hii isitawalike. Baadhi ya wasomi katika eneo hilo wameamua kuifanya migogoro kama sehemu yao ya kujipatia mahitaji, yakiwamo ya kusomesha watoto wao katika shule ghali, huku masikini wengi wafugaji wakiachwa wakitaabika.


Serikali hii itakuwa ya ajabu kama itatishwa na kutishika kuhusu uamuzi huu wa kulinda utajiri huu mkubwa ambao Mungu ameijaalia nchi yetu. Wananchi wa Loliondo ni waelewa, tatizo ni hawa vinara wa migogoro wanaohamasisha vurugu na migogoro ya kila mara.

 

Uzushi huu wa kwamba kupunguza eneo hilo kutawaathiri wananchi, ni uongo na ghilba za NGOs ambazo lazima zikomeshwe sasa.


Hakuna serikali makini duniani ambayo inaendeshwa puta na NGOs. Wananchi wa Loliondo, Ngorongoro na Tanzania kwa jumla wanapaswa kuutambua uamuzi huu sahihi wa Serikali na kuiunga mkono kwa kupambana na wale wote wenye nia mbaya.


Mara zote tumesema wazi kuwa kwenye mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, hatutakuwa na suluhu na yoyote. Hatuwezi kushuhudia nchi ikiyumbishwa na watu wachache, na sisi tukakaa kimya. Lakini lililo muhimu ni kujiuliza, kwanini chokochoko nyingi zinakuwa na vimelea kutoka nchi jirani na kwa mashirika ya wafadhili?

 

Kwa hili tunasema Wizara ya Maliasili na Utalii isithubutu kurudi nyuma. Tupingane kwenye mambo mengine, lakini ya kitaifa lazima tuwe wazalendo ili tupambane na maadui wa umoja na maendeleo yetu.

1238 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!