Toleo la leo ni toleo maalum la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Bajeti ya wizara hii imeeleza mipango mingi mizuri yenye lengo la kutatua migogoro ya ardhi nchini na kuwapa Watanzania haki ya kumiliki ardhi.

Wizara katika hotuba yake, imeeleza ufinyu wa bajeti unaoikabili wizara hii kutokana na fungu la fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kuwa finyu. Sisi tunapenda kuamini kuwa msomaji umesoma kwa kina maelezo ya waziri na wizara katika eneo hili.

 

Tumejaribu kufikiri kwa kina na kujiuliza jinsi gani nchi yetu inavyoweza kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja na kutatua migogoro ya ardhi. Ukisikiliza mjadala wa wabunge bila kujali itikadi za vyama, utaona kuwa wabunge wote wanalalamikia utaratibu wa upimaji viwanja.

 

Malalamiko ya wabunge ni dhidi ya watu wachache wenye uwezo wa kifedha wanaochukua mashamba makubwa ya ardhi, lakini hata kile kidogo walichonacho wanachi kuchukuliwa kwa guvu ya fedha. Tunawaheshimu Waziri Profesa Anna Tibaijuka na Katibu Mkuu, Patrick Rutabanzibwa.

 

Tunafahamu kuwa viongozi hawa wanao uwezo wa kufikiri na kuamua haraka wakaacha historia katika nchi hii. Kuna uwezekano mkubwa wizara hii kutumia Sheria ya Private Public Partnership (PPP) kuwahisha upimaji wa viwanja hapa nchini.

 

Wizara inaweza kutangaza mpango wa kupima viwanja, ikawajulisha wananchi gharama za upimaji na kuwapatia hati inayotambulika kisheria. Tunapenda kuihakikishia Serikali kuwa mradi wa aina hii ukiwa wa kweli usio wa ujanujanja, Watanzania watakuwa tayari kulipa hata Sh 1,000,000 kwa kiwanja.

 

Hati hizi zikishapatikana, wananchi watazitumia kupata mikopo kutoka benki mbalimbali, na hivyo kuondoa umaskini kwa kasi kubwa. Tunafahamu wapo watendaji wanaochukulia suala la ardhi kama ufalme wao. Wanakwamisha upimaji wakitegeshea rushwa.

 

Tunasema sasa wakati umefika. Watendaji wasiofanya kazi kwa malengo, waoneshwe mlango. Tuwapatie Watanzania hati za viwanja, huu utakuwa mwanzo wa kufuta umaskini, hasa ukitilia maanani kuwa dunia inakwenda kasi kuliko tulivyotarajia. Tubadilike.

Please follow and like us:
Pin Share