Waziri Lugola maliza sakata la Lugumi

Ni miaka miwili na nusu sasa tangu
Watanzania walipoanza kusikia kuhusu
sakata la Kampuni ya Lugumi Enterprises
kushindwa kufunga vifaa vya kuchukulia
alama za vidole kwenye vituo 108 vya
Polisi, kama mkataba wa kampuni hiyo na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
ulivyotaka.
Jambo hilo liliibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof.
Juma Assad, katika taarifa yake ya ukaguzi
ya mwaka wa fedha 2011/2012.
Jambo hilo limewahi kupapaswa na mhimili
wa Bunge na kutoa maelekezo kwa Serikali
kulifanyia kazi tangu Agosti 2016, mpaka
leo hakuna kilichofanyika. Katika kipindi cha
miaka miwili na nusu ya utawala wa Rais
John Magufuli, mawaziri wawili wa Mambo
ya Ndani ya Nchi wamepita bila kumaliza
mjadala wa sakata hilo.
Mawaziri hao ni Charles Kitwanga pamoja

na Dk. Mwigulu Nchemba, ambao kwa
nyakati tofauti wameiongoza wizara hiyo,
huku sakata la Lugumi likiendelea kufukuta
bila kumalizwa, kwa ama jamii kuambiwa
hapakuwa na jambo lolote ama wahusika
kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Sakata hilo limeibuliwa upya Julai 2, mwaka
huu na Rais John Magufuli, baada ya
kumwapisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Kangi Lugola. Wiki kadhaa baadaye
waziri huyo ameonyesha kuhitaji kukutana
na mmliki wa Kampuni ya Lugumi
Enterprises, Said Lugumi.
Ni matumaini yetu kwamba mkutano huo
utakuwa ni wenye manufaa kwa pande
zote; mosi, kuhakikisha teknolojia hiyo ya
alama za vidole inafungwa katika vituo
vyote ili kukidhi matarajio ya kununua
teknolojia hiyo, lakini kama kumekuwa na
ulaghai ni wakati sahihi hatua stahiki
zikachukuliwa kwa masilahi mapama ya
Tanzania.
Kitendo cha Said Lugumi, ambaye ndiye
mmiliki wa Kampuni ya Lugumi Enterprises,
kusema yuko tayari kukutana na waziri

katika mazingira yoyote yatakayoonekana
yanafaa, ni mwanzo mzuri katika kuelekea
kukamilisha na kufunga kabisa mjadala
huo.
Rai yetu kwa Waziri Lugola ni kuhakikisha
sakata hilo analishughulikia na kulimaliza
kwa uwazi kama ambavyo ameahidi katika
mkutano wake na wanahabari. Lakini pia
wananchi wanasubiri kuona kama yeye
atakuwa tofauti na watangulizi wake, ambao
sakata hilo lilikuwa sawa na mfupa mgumu
usiolika.