Mimi ni Mtanzania ambaye kwa sasa nipo nchini Marekani nikijiendeleza  na kufanya shughuli mbalimbali kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

Mwaka 2008 nilikuja nyumbani (Tanzania) na kuelekea mkoani Mbeya kutafuta kiwanja cha makazi. Nilifanikiwa kupata kiwanja na kukabidhiwa hati miliki namba 12477 iliyotolewa Julai 10, 2008 na Msajili wa Hati Mbeya.

Mwaka jana nilirudi tena hapa nyumbani na kutembelea mkoani Mbeya kwa ajili ya kuangalia kiwanja changu.

Mhe. William Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) nilichokiona hapo kilinishangaza sana.

Nilikuta nyumba mbili zimejengwa ndani ya kiwanja changu, ndipo nikaamua kwenda katika ofisi za jiji la Mbeya kutoa taarifa za kuvamiwa kwa kiwanja hicho.

Mhe. Lukuvi katika ofisi za jiji hilo nilikutana ofisa mmoja ambaye badala ya kunisaidia akanijibu kwa kunikatisha tamaa  kwamba, “kazi ya kulinda kiwanja chako kisivamiwe ni yako mwenyewe.”

Jibu nililopewa na ofisa huyo limenikatisha tamaa sana, hivyo nikaamua kuondoka nchini na kurudi tena Marekani kuendelea na shughuli zangu.

Hata hivyo, nimekuwa nikifuatilia utendaji wako Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe Lukuvi na kuona kuwa ni Waziri unayejituma na kuwatetea wananchi wanyonge wanaodhulumiwa ardhi zao.

Nakuomba Mhe. Lukuvi unisaidie nipate haki yangu, kwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya `amewaruhusu’ watu wawili kuvamia kiwanja changu namba 210, kitalu KK, eneo la Itezi Mbeya.

Nimekuwa nikilipa kodi ya ardhi kila mwaka. Na imani kwamba nitapata haki yangu kupitia kwako Waziri Lukuvi au mtumishi yeyote wa wizara hiyo anaweza kunisaidia na kuokoa kiwanja changu kutoka kwa wavamizi hao.

Nimeamua kupitishia kilio changu kupitia gazeti hili la JAMHURI kwa sababu nimeona wanyonge wengi wakisaidiwa kupitia katika gazeti hili hapo Tanzania.

2854 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!