Mjadala uliohusu vita dhidi ya uvuvi haramu ulitawala sehemu kubwa ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, bungeni jijini Dodoma, wiki iliyopita.

Pengine kabla ya kuendelea, ni vizuri tukafahamu kazi za mbunge. Mbunge ana kazi nyingi, lakini zilizo kuu kwa mujibu wa Katiba yetu ni kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria, na kuisimamia Serikali.

Lakini tunaweza kuzinyambua kazi hizo na kuona kuwa mbunge ana wajibu pia wa kushirikiana na wananchi wake katika kazi mbalimbali za kujenga taifa, kuisaidia Serikali ili iweze kuongoza vizuri, na pia kuhudhuria vikao vya Bunge.

Nimerejea kuzitambua kazi za mbunge baada ya kusikia mijadala mikali na yenye jazba kwa baadhi ya wabunge kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu pamoja na zana zake.

Wakati akihitimisha mjadala huo, Waziri mwenye dhamana, Luhaga Mpina, alitofautiana na wabunge waliokosoa hatua zinazochukuliwa na wizara yake kupambana na uvuvi haramu, hasa katika Ziwa Victoria pamoja na kudhibiti utoroshaji samaki na mazao yake nje ya nchi.

Akasema, “Mimi na wizara yangu tutahakikisha hili tunalisimamia kwa nguvu zote, hizi ni rasilimali za taifa na haziwezi kugawanywa kwa ukanda, rasilimali hizi zinapashwa kunufaisha nchi nzima kwa hiyo kama wizara inayosimamia sheria zilizopitishwa na Bunge hili tutahakikisha kwamba hakuna kabisa uvuvi haramu katika nchi yetu, hakuna mfanyabishara atakayejihusisha na kuuza wala kusambaza nyavu haramu, hakuna kiwanda kitakachochakata samaki wasioruhusiwa, hakuna mtu yeyote atakayevua kwa vyavu haramu wala kufanya biashara haramu ya mazao ya uvuvi. Ni lazima mali zetu tuzilinde kwa nguvu zote.”

Kwa dhati ya moyo wangu nampongeza Waziri Mpina. Tunahitaji mawaziri jasiri wa aina yake. Nampongeza si kwa sababu ya kuyasema haya bungeni, bali kwa kuwa huo ndiyo umekuwa msimamo wake hata nje ya Bunge.

Nchi hii tusipokuwa na viongozi wakweli na wenye misimamo ya aina hii, tutapoteza kabisa rasilimali zetu. Ukiwasikiliza wabunge kadhaa wanaokosoa mpango wa wizara katika kulinda rasilimali hizi unabaini kitu kimoja kikubwa ambacho ni UBINAFSI.

Sijafanya utafiti, lakini uzoefu unanifanya nishawishike kuwa huenda kwenye utetezi huu wabunge kadhaa ni sehemu ya tatizo la uvuvi haramu. Nasema sina hakika, lakini akili inanifanya nijiulize maswali mengi unapoona au kusikia utetezi wa jambo haramu. Nasema hivyo kwa sababu hata kunapotokea utetezi wa ufugaji holela, karibu wabunge wengi wanaotetea ni wadau wa hali hiyo.

Hapo juu nimeanza na kazi za mbunge. Sina hakika na idadi ya wabunge ambao kabla ya kwenda bungeni hukutana na wananchi kwa lengo la kukusanya maoni ya yepi wawakilishi hao wayapeleke bungeni kwa niaba ya wapigakura. Unaweza kujiuliza, haya yanayozungumzwa na wabunge huwa wametumwa na wapigakura wayaseme bungeni au ni maneno yanayotokana na hisia na misukumo binafsi? Hapa tutambue kuwa si kila mbunge ni mzalendo, maana bado napata shida kuamini kama kweli Mtanzania mzalendo anaweza kumshutumu waziri kwa jambo jema la kulinda rasilimali za nchi.

Kwa sababu hiyo hiyo, ndiyo maana nashindwa kuamini kama kweli kuna wananchi waungwana, wapenda nchi yao wanaoweza kumtuma mbunge bungeni kutetea maharamia na manabii wa uvuvi haramu. Kama kweli wapo wananchi wanaomtuma mbunge kuwasemea kwenye hilo jambo ovu, na mbunge naye akasimama bungeni kupaaza sauti kutetea uvuvi haramu, basi mbunge au wabunge wa aina hiyo ni janga kwa wapigakura wake na taifa zima.

Tumewasikia wabunge wakisema hawatetei uvuvi haramu na zana zake, bali wanapinga aina ya vitendo wanavyofanyiwa wavuvi na wananchi wengine wanaokutwa wakitekeleza makosa hayo. Mathalani, wanasema ni uonevu kwa wizara kuchoma nyavu (zilizozuiwa kisheria), badala yake wanashauri wale wenye kuzitengeneza au kuagiza ndiyo washughulikiwe. Haya ndiyo mawazo ya baadhi ya wabunge wetu! Kwao, anayetumia kisu kuua hana kosa, isipokuwa kile kiwanda kilichotengeneza hicho kisu! Kwao wao, anayeua kwa bunduki hana kosa, bali kiwanda kilichotengeneza silaha ndicho kinachostahili adhabu ya kufungiwa! Haya ni mawazo ya ajabu sana.

Wabunge wetu wanatambua kuwa kutojua sheria siyo kinga ya kuvunja sheria. Huwezi kutenda kosa halafu ukajitetea kwamba ulikuwa hujui kama sheria inazuia kosa hilo.

Waziri Mpina na timu yake wanatekeleza sheria zilizopitishwa na Bunge. Wenye mamlaka ya kubadilisha sheria ni wabunge hao hao. Kama wanaona sheria za kulinda rasilimali za nchi hazifai ni wao hao hao wanaopaswa kubadili sheria. Bahati nzuri sheria zetu zinaruhusu mbunge kuwasilisha muswada binafsi wa sheria au mabadiliko ya sheria. Pamoja na kuwapo fursa hiyo, hatujamsikia mbunge au wabunge wanaopeleka mapendekezo ya kubadili sheria ili makokoro yaruhusiwe kuua samaki awaye yeyote popote alipo.

Badala yake wanachofanya ni kumvizia waziri awasilishe hotuba kisha wapate muda wa kumshambulia. Kama kinachofanywa na waziri ni kibaya, kwanini hawamwondolei hiyo sheria?

Ndugu zangu, sisi baadhi ya Watanzania, na nadhani Waafrika wa leo kwa ujumla wetu, moja ya sifa zetu mbaya ni ubinafsi. Tumekuwa wabinafsi kiasi cha kutufanya tusione wala kukubali kuwa kuna maisha mbele. Tumekuwa wabinafsi kwa kiwango cha kutupofusha hata tusiweze kuona kuwa kuna kizazi kinachokuja baada yetu sisi. Tumekuwa watu wa kuamini kuwa maisha ni leo tu, na ni kama tunasema hao wajao – wakute vipo au havipo – hiyo ni shauri yao! Tunaweza kuwapuuza Wazungu kwa baadhi ya mambo, lakini kama lipo jingine jema la kujifunza kwao ni hili la kuishi kwa namna ya kuandaa maisha bora kwa kizazi kijacho.

Kuwa na huruma na wavuvi haramu na zana zao ni ubinafsi mbaya. Wapo baadhi yetu wanaotaka waachwe wavue kadri wanavyoweza ili wafaidi wao leo! Hawana habari kabisa na kizazi kijacho. Wanadhani wanao pekee ndiyo wenye haki ya kufaidi urithi huu. Mababu na mabibi zetu kama wangekuwa na roho mbaya namna hii, sisi leo tusingeambua kitu. Mababu zetu walitumia ndoana, wakavua samaki wakubwa na kuwaacha wadogo waendelee kukua na kuzaliana. Sisi leo tunataka turuhusu makokoro ili tupate samaki zaidi –huku tukijifanya hamnazo kwamba mbinu hiyo inamaliza samaki wote.

Hatuna budi kuishi kwa kuheshimu mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho. Uvuvi haramu umeleta janga kubwa mno nchini. Wapo maharamia wanaotumia mabomu na sumu kuua samaki. Wapo wanaotumia makokoro kuvuruga matumbawe na sehemu zote za mazalia ya samaki. Kuwatetea watu wa aina hii kunahitajika moyo usio wa upendo kwa nchi yako. Sidhani kama kuna mbunge Mtanzania anaweza kuwa upande wa maharamia hawa.

Uvuvi haramu una athari nyingi. Unasababisha upungufu wa samaki na kwa maana hiyo unasababisha upungufu wa protini kwa wananchi. Protini inapopungua hiyo inakuwa njia ya kupata maradhi. Kupungua kwa samaki kuna athari kiuchumi kwa wavuvi na wananchi. Badala ya kumpinga waziri, tuungane kumuunga mkono ili mapambano haya yalete tija kwa wananchi na kwa taifa. Hatuwezi kupambana na umaskini kwa kutetea uvuvi haramu.

Mbunge anayedhani wajibu alionao ni kutetea wananchi wanaovua kwa mbinu haramu, huyo ni adui wa wananchi. Badala ya kulalamika kuchomwa nyavu, atumie nafasi yake kukutana na wapigakura kuwaeleza athari na adhabu zinazowakabili wavuvi haramu.

Tunapaswa kumuunga mkono Waziri Mpina kwa sababu anachofanya kina manufaa mapana kwa taifa, na kwa kweli anatekeleza kazi aliyotumwa na wabunge kupitia sheria walizotunga. Msimamo wa wabunge endapo utashinda maana yake tutakuwa tunajenga na kudumisha tabia mbaya ya kuwaandamana viongozi wanaotekeleza sheria kadri ya viapo. Mpina hakuapa kuhakikisha samaki wanatoweka. Aliapa kuhakikisha analinda rasilimali hii ili ilete tija kwa wananchi na taifa.

Kutafuta kupendwa na wananchi kwa kutetea uvunjifu wa sheria si kulitendea haki taifa, na hasa kwa kizazi kijacho ambacho kina haki sawa ya kufaidi rasilimali hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Wajibu wetu ni kulinda utajiri huu kwa nguvu zote. Tutakuwa viumbe wa ajabu kuona tukimaliza samaki wote kwa uvuvi haramu na badala yake sasa tukawa waagizaji wa samaki kutoka ughaibuni.

Wakati mwingine tunapotukanwa na Wazungu tusilalamike maana kuna mambo tunayofanya yasiyolingana kabisa na uwezo wa akili za binadamu wa karne ya 21. Tunapowaonea huruma wavuvi haramu kiukweli tunakuwa hatuwaonei huruma wananchi. Hongera Waziri Mpina na timu yako inayosimamia rasilimali hii adhimu. Kwa kuwa mnatenda yaliyo mema kwa manufaa ya kizazi cha leo na kijacho, msiogope. Mungu yuko upande wenu maana kwenye maandiko ya uumbaji sijaona mahali Mungu akituagiza tuteketeze mema aliyotupatia. Mungu awabariki sana.

2507 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!