Katika maendeleo ya nchi na jamii msingi wa utawala wa sheria ndio hasa huleta ulinganifu kwa aliyenacho na asiyenacho. Hivyo ni msingi huo pekee haki huonekana imetengendeka.

Kumekuwepo na kilio hasa kutoka kwa wanyonge pindi wanapoona hawajatendewa haki na mamlaka husika. Kilio kikubwa  kimekuwa kikielekezwa kwa Jeshi la Polisi. wamekuwa wakituhumiwa na wananchi kuwapatia ulinzi baadhi ya watu wasio wema.

Lawama na shutuma hizo zimekuwa zikitajwa katika migogoro ya ardhi, ambapo wenye ukwasi wamekuwa wakitumia vyombo vya dola katika kuzima haki za wanyonge.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Murilo Jumanne, ameonesha kwamba zama zimebadilika na Polisi wanafanya kazi kwa weledi, hasa lilipokuja suala la ‘amri’ ya kumwondoa Jaji Joseph Warioba katika nyumba ya serikali alimopanga kama walivyo wapangaji wengine.

Mbali na kupokea maombi ya kuwapeleka askari kusimamia kumwondoa mpangaji, kutoka kwenye kampuni ya udalali ya Yono, bado kamanda wa Polisi, hakuangalia kwamba maombi hayo yanaihusisha taasisi ya Serikali na mpangaji wake, yeye akaomba amri ya Makahama, ili awaruhusu askari kwenda kutoa ulinzi wakati wa kumwondoa Jaji Warioba.

Kitendo hicho, kinapongezwa kwa dhati kabisa na gazeti la JAMHURI, huku tukisisitiza kwamba umakini huo wa kuomba nyaraka muhimu kama amri ya Mahakama iwe ni chahu kwa viongozi wengine wa Jeshi la Polisi nchini, kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawatendea haki wananchi wenzetu bila kuangalia mamlaka na madaraka waliyonayo.

Shauri la Jaji Warioba na Wakala wa Majengo ni miongoni mwa mashauri mengi yaliyoko Mahakamani yakisubiri uamuzi, lakini ‘wahuni’ wamekuwa wakipitia mlango wa nyuma na kutumia mabavu kwa kuvishirikisha vyombo vya dola.

Sisi JAMHURI tunasema ni wakati mwafaka kutii na kufuata misingi ya utawala wa sheria kwa yeyote awaye. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima na kutengeneza jamii inayoheshimiana na kuheshimu utawala wa sheria.

By Jamhuri