Rais Jakaya Kikwete alipoamua kuleta suala la Katiba mpya kupitia ilani yake ‘mbadala’, wapo waliomshangaa.

Nakumbuka niliandika makala iliyosema, “Nitakuwa wa mwisho kuishabikia Katiba mpya”. Hiyo haikuwa na maana kwamba sikutambua wala kuthamini matamanio ya Rais wetu kuwaachia Watanzania Katiba nzuri!

Kwangu mimi, tatizo la nchi hii si Katiba kama watu wanavyotaka tuamini. Tatizo ni ubinafsi na ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa viongozi wetu. Shida za nchi hii zinasabishwa na viongozi wabovu waliojaa tamaa. Katiba ni kisingizio tu!

Ukisikiliza michango mibovu ya wabunge katika Bunge Maalum la Katiba, utajua ninachokisema hapa.

Watu wazima wanapopinga elimu ya mbunge walau ianzie kidato cha nne, tatizo hapo si ukosefu wa “katiba nzuri’, bali ni ubinafsi na ujima wa kimawazo uliowajaa baadhi ya Watanzania, hasa wana CCM wanaoamini bila chama hicho kufanyiwa mbinu za kuendelea kuwa madarakani, hawana maisha mengine! Kwao CCM ni maisha yao, na maisha yao ni CCM!

Watu wenye maono walishasema elimu ya kidato cha nne ndiyo iwe elimu ya msingi! Kuendelea  kwao kung’ang’ania darasa la saba litambuliwe, hiyo ina maana hawataki kidato cha nne kiwe ndiyo elimu ya msingi katika Tanzania!

Sababu wanazotoa ni dhaifu. Eti wanasema kumnyima darasa la saba haki ya kugombea ni kumnyima haki yake ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa!

Haki za binadamu au za kidemokrasia zina ukomo. Kwa ukomo huo, ndiyo maana majambazi au wahalifu wengine walio magerezani hawapigi kura. Kama ni haki, basi siku ya upigaji kura masanduku yapelekwe pale Milembe (hospitali ya afya ya akili) ili wale ndugu zetu nao wapate haki ya kuwachagua madiwani, wabunge na rais wanayemtaka. Hilo halifanyiki kwa sababu haki zina ukomo wake.

Kama ni haki, na kama kweli wabunge hawa wanaamini demokrasia haina mipaka, basi kwanini wang’ang’ane kuweka umri wa mgombea urais? Kwanini isiwe miaka 18? Kama mwenye umri wa miaka 18 anapiga kura kumchagua rais, kwanini huyo huyo asiwe na haki ya kupigiwa kura ya kuchaguliwa kuwa rais? Kwanini iwe kinyume? Imekuwa kinyume kwa sababu haki au demokrasi ina mipaka yake. Haki ni kama ndevu. Haiwezekani kila jinsi ikawa na ndefu kana kwamba hii ni jamhuri ya samaki!

Moja ya kazi kubwa ya mbunge ni kutunga sheria. Wabunge wengi wanapotaka tuendelee kuwa na watu wenye ujuzi mdogo kielimu, hasa ubunge, maana yake wanataka ujinga utumike kama mtaji wa CCM kudumu madarakani. Hiyo haikubaliki, na kamwe haitakubalika.

Uchumi wa gesi, mafuta; uchumi wa madini, uchumi wa ulimwengu wa sasa unahitaji watu wenye weledi na elimu ya kutosha. Kutaka wabunge wetu wa darasa la saba wakutane kujadili mambo na wabunge wa Uingereza au Marekani katika masuala ya kiuchumi, ilhali tukijua hao wa ughaibuni ni wasomi na wazalendo kutuzidi, tunajidanganya.

Elimu ya darasa la saba ilikuwa muhimu wakati ule ambao Tanzania haikuwa na wasomi kwa maana hiyo ikawa mbunge awe na sifa ya kujua kusoma na kuandika. Hili naomba niitwe mchochezi! Naomba popote litakapoonekana, Watanzania walipinge kwa hoja na ikibidi kwa kura hata kama ni mwaka 2016 au 2020!

Unapowasikia watu wazima wakijadili kuwa na Katiba inayotaka kiongozi anayepewa zawadi (rushwa) ya dhahabu, hata kama ni kilo 100; iwe mali ya kiongozi aliyepewa zawadi hiyo, moja kwa moja mwenye akili utajua nchi hii imepigwa laana! Kwao, kiongozi kupewa mali nyingi na za thamani kadri inavyowezekana, halafu akazifaidi yeye na familia yake, hilo si jambo la kuwasumbua vichwa Watanzania. Walituletea rushwa kwa mgongo wa takrima, sasa wanaleta rushwa kwa sura ya zawadi za viongozi! Wananchi kataeni mapendekezo haya mabaya.

Unapotazama runinga na kuwaona watu wanaohaha waitwe waheshimiwa wa Bunge Maalum la Katiba, wakikataa kama masuala ya ‘uadilifu’ kuwekwa kwenye Katiba, na badala yake eti itungiwe sheria, ujue hapa kinachowahangaisha hawa wakubwa ni kuhakikisha wanaendelea kutapanya mali za Watanzania bila kuhojiwa! Uadilifu kuwekwa kwenye Katiba kuna dhambi gani?

Tena basi, ukiwaona watu wenye umri wa kustahili kuitwa wazee au ajuza wakipambana kwa nguvu zote kupinga uteuzi wa rais kuthibitishwa na Bunge, hakika ujue hapa tunahitaji ukombozi mwingine! Huu tulionao si ukombozi, isipokuwa ni mifereji inayotiririsha kasumba mbaya za uongozi wa kibabe wa watu waliopofushwa na upendeleo na kubebana.

Tumeona Waziri Mkuu akithibitishwa na Bunge, lakini sasa tunaambiwa Jaji Mkuu au Naibu wake kuthibitishwa na Bunge ni kutaka kupunguza hadhi ya mhimili wa Mahakama! Eti Jaji Mkuu au naibu wake hawana sababu ya kuthibitishwa na Bunge ambalo ndicho chombo cha juu cha uwakilishi wa wananchi. Kama wanapinga jaji na naibu wake kuthibitishwa na Bunge kwa kigezo kuwa hao ni wa mhimili mwingine (Mahakama), kwanini wakubali/wamekubali waziri mkuu ambaye ni wa mhimili mwingine (Serikali), athibitishwe na Bunge ambalo ni mhimili tofauti?

Kama wanapinga jaji kuthibitishwa na Bunge, iweje wawe tayari kukubali ushindi wa rais kuhojiwa mahakamani, au wabunge kuwa na mamlaka ya kumuondoa rais madarakani kupitia kura ya kuwa au kutokuwa na imani naye? Hivi watu wazima wakiingia kwenye ule ukumbi, nini huvuruga akili zao?

Kenya tumeona waomba ujaji mkuu wakipambanishwa kwa maswali yanayorushwa ‘live’ kupitia runinga na redio. Nafasi kama ya Mkuu wa Jeshi la Polisi inaombwa! Watu wanafanyiwa usaili! Hii inawafanya wanaopitishwa kujiona ni watumishi wa umma kwa sababu kazi hizo hawazipati kwa busara au hekima ya rais wa nchi. Mambo mazuri kama haya kwanini wabunge wa Tanzania hawayataki?

Kumetolewa hoja nzuri za kutaka mawaziri wasiwe wabunge. Zipo sababu nyingi, lakini baadhi ni kwamba hatua hiyo inampa wigo mpana rais kuweza kuteua watu wenye uwezo badala ya kumuwekea wigo wa mawaziri kutoka bungeni pekee.

Faida ya pili ni kujaribu kuleta uwajibikaji. Tumeona wabunge ambao ni mawaziri wakipendelea majimbo na hata mikoa yao. Wanafanya hivyo si kwa bahati mbaya, bali kwa kulenga kujijengea mazingira mazuri ya kuchaguliwa tena kwenye ubunge ili waendelee kuwa mawaziri.

Matokeo ya mfumo huu yameyafanya majimbo yasiyokuwa na mawaziri yabaki nyuma kimaendeleo. Busara ikaonekana kwamba kuwa na mawaziri ambao hawajipendekezi kwa wapiga kura kutaleta ufanisi na kusambaza maendeleo kwa uwiano nchini kote. Hili wabunge wetu wengi, kama waliologwa, hawalitaki!

Wanataka mawaziri watoke miongoni mwa wabunge. Wanataka rais aendelee kuhangaika kuli- circle humo humo bungeni hataka kama kabaki na ‘pumba’. Wanataka hata kama rais kabaki na wabunge wote wabovu, basi atafute ‘mbovu kiasi’. Haya ni maajabu ya Tanzania.

Lakini kabla sijahitimisha, nirejee kile nilichokigusia mwanzoni mwa makala hii. Rais Kikwete alipoamua kuanzisha utaratibu wa kuwapatia Watanzania Katiba mpya, inawezekana alikuwa na nia njema, lakini kwa bahati mbaya, ama yeye, au wasaidizi wake, hawakuwa na utashi wa kuileta Katiba hiyo.

Imekuwa kawaida ya watu walio Ikulu au madarakani kuamini kuwa wana akili kuliko maelfu kama si mamilioni ya Watanzania wengine wasiokuwa na sauti.

Kwa mfano, kupitia gazeti hili hili tuliandika hivi, “Katiba mpya haipatikani”. Awali, tulionekana kama waganga wa kienyeji! Wakubwa walio Ikulu hawakutaka kusoma maudhui kujua kwanini tumediriki kusema hivyo. Hata tulipoandika ya ujangili, nchi haikutikisika isipokuwa pale yalipoandikwa kwa kimombo katika gazeti la Daily Mail la Uingereza.

Tulisema hivyo kwa sababu kadhaa, lakini kwa ufupi tu ni kwamba Katiba isingewezekana bila kuanza na kura ya maoni ya aina ya Muungano ambao Watanzania wanautaka. Kufanya hivyo lilikuwa jambo muhimu hata kama lingetafsiriwa kuwa ni uhaini. Kura ya maoni ingerahisisha sana kwani hilo lingemalizwa kabla ya utaratibu wa kuandika Katiba kuanza.

Pili, tukasema lilikuwa kosa kubwa kwa Rais Kikwete kuiacha Zanzibar ‘ijitangazie uhuru’; ilhali yeye akiwa kimya akishuhudia uvunjaji Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulio wazi. Mwaka 1984 hilo lilipojitokeza, Rais wa wakati huo alilizima haraka.

Rais Kikwete alipowaita waandishi wa habari Ikulu (wakati huo akiwa bado anawapenda), aliulizwa swali hilo, lakini majibu yake yakawa kwamba “kama Zanzibar wameridhiana na kurejesha utulivu, kulikuwa na ubaya gani?” Hakujua alichokiita ‘utulivu’ kilikuwa ni maambukizi ya maradhi mabaya ya kuivunja nchi ambayo hapa yalipofika, hakuna tiba ya kuyaondoa! Matokeo yake Tanganyika sasa inadaiwa kila kona hata ndani ya CCM yenyewe.

Wale walio nje ya Ikulu na Serikali walishauri, lakini kwa sababu walio nje ya vyombo hivyo ‘hawana akili’ kama waliomo ndani, wakapuuzwa. Matokeo yake ndiyo haya ya kushindikana kupatikana kwa Katiba licha ya mabilioni kutafunwa.

Haya niliyojaribu kuyaeleza hapa ndiyo yanayonirejesha kwenye hoja yangu ya kwamba “Nitakuwa wa mwisho kuishabikia Katiba mpya”. Kama kweli Katiba yenyewe iliyotumbua Sh bilioni 100 za Watanzania ndiyo ya aina hii tunayoletewa, heri tuendelee na Katiba yetu ya mwaka 1977.

By Jamhuri