KATAVI

Na Walter Mguluchuma

Familia zenye watoto wenye ulemavu zimehamasishwa kuwapeleka shule watoto hao waweze kutimiza ndoto zao badala ya kuwachukulia kama laana.

Akizungumza katika kikao maalumu na wazazi wa watoto wenye ulemavu, Ofisa Maendeleo wa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Mpanda, Joshua Sinkala, amesema watoto hao wanastahili kupata haki ya elimu sawa na wenzao.

“Kuna baadhi ya wazazi huwachukulia watoto hawa kama laana na kuwafungia nyumbani badala ya kuwapeleka shuleni. Hii ni kinyume cha haki za mtoto na za binadamu,” anasema Sinkala.

Mratibu wa Elimu Jumuishi Manispaa ya Mpanda, Jeremia Kikoti, amesema ulemavu ni suala la kawaida na watoto wenye ulemavu ni sawa na wengine na kwamba wana haki kushiriki katika masuala mbalimbali.

“Jamii haipaswi kuwatenga. Wakitengwa wataishi maisha yasiyo na furaha,” anasema Kikoti.

Anasema katika Mradi wa Elimu Jumuishi unaotekelezwa kwa awamu ya pili katika Manispa ya Mpanda, upo katika shule za msingii nne ambazo ni Azimio, Kivukoni, Shanwe na Nyerere.

“Tangu utekelezaji wake ulipoanza umekuwa na mafanikio kwa kuwaunganisha watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu kusoma pamoja tofauti na ilivyokuwa awali,” anasema.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Azimio, Beno Mahema, anasema shuleni hapo kuna wanafunzi wenye elemavu wa aina mbili; wasioona na ulemavu wa kutosikia wanaosoma kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba.

“Kuna wazazi wanaoshindwa kuwasafirisha watoto wao kuja shuleni na kusababisha watoto kukosa baadhi ya vipindi,” anasema Mwalimu Mahema.

Anaitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wazazi kushindwa kununua betri za mashine  za kusaidia usikivu na kusababisha ufundishaji wa watoto wenye ulemavu wa kusikia kuwa mgumu.

Mwalimu Emable Kabale wa Shule ya Msingi  Nyerere, anasema shule hiyo ina watoto 27 wenye mahitaji maalumu.

“Mpango wa elimu jumuishi umesaidia kuondoa tatizo la kubaguliwa watoto wenye ulemavu. Ukifika shuleni kwetu wala hauwezi kuwatofautisha watoto hao kwa jinsi wanavyoshirikiana darasani na hata michezoni.

By Jamhuri