DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Baadhi ya wakazi wa Kigamboni wameiomba serikali kuangalia upya utaratibu wa mfumo wa kadi za kielektroniki kutumika wanapovuka bahari kwa kutumia pantoni.

JAMHURI limeelezwa na wananchi hao kwamba mfumo huo umeanza kutumika bila kuwapo elimu ya kutosha.

Mmoja wa wasafiri waliokuwapo upande wa Magogoni siku chache baada ya mfumo kuanza kutumika mwezi uliopita, Ibrahim Othman, anasema wamekumbwa na changamoto kadhaa kutokana na kutouzoea mfumo huo.

“Shida kubwa hutokea nyakati za asubuhi na jioni. Nyakati hizi huwa na wasafiri wengi, hivyo utakuta ni mashine mbili au tatu tu ndizo zinazofanya kazi. Ni shida kubwa,” anasema Othman.

Othmani anakiri kuwa mfumo wa kadi unasaidia kwa namna fulani, tofauti na tiketi za karatasi, isipokuwa waliouleta hawajaufanyia tathmini ya kutosha.

“Ukija asubuhi ndiyo utaelewa ninachosema, kwani utakuta msongamano mkubwa wa watu sehemu zote mbili; za tiketi za karatasi na mashine za kadi. Utagundua mara moja kuwa hauna faida kwa jamii,” anasema.

Mwanamke mmoja mtu mzima, Rose James, anasema kwa umri wake mfumo wa kadi ni adhabu kwani una usumbufu.

Anasema wengi wao wakishalipia kadi za kielektroniki huwa hawafahamu kama zina mwisho na ikiisha anatakiwa kulipa Sh 1,000 ili kuendelea kupata huduma.

“Mimi mara kwa mara hukumbwa na tatizo la kusahau. Sikujua kama kadi hii inatumika kama LUKU, kwa kweli kadi hizi kwangu si rafiki. Huisha bila taarifa huku nikiwa na fedha nyingine mfukoni,” anasema Rose.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Deo Fabian, akisema amewahi kuingiza Sh 1,000 kwenye kadi akitarajia kuvuka na pantoni mara tano, lakini baada ya safari mbili tu, fedha zikaisha kwenye kadi.

“Nilipokuja kwa mara ya tatu, kadi ikagoma. Ikaonyesha kwamba salio limekwisha na ninatakiwa kuongeza fedha!

“Watanzania wengi kipato chao ni cha chini, hivyo kulazimika kutoka kila siku lakini bado kipato hakitoshi. Kadi ikiisha uwezo wa kuweka Sh 1,000 haraka ni mzigo mzito. Ukiwa hauna fedha, labda umebaki na Sh 200 wanakataa kukuuzia tiketi, maana yake nini?” anahoji Fabian.

Anashauri mfumo uruhusu kuweka kiwango chochote cha fedha hata chini ya Sh 200 kuwasaidia wananchi wanyonge na kupunguza malalamiko kwa serikali.

Mmoja wa maofisa wa kutoka National Internet Data Centre (NIDC) anayesimamia mfumo katika kivuko cha Kigamboni, Simon Joseph, anasema mfumo ni mzuri na utapunguza foleni nyakati za jioni na asubuhi.

Anasema changamoto iliyopo kwa sasa ni upya wake kwa watumiaji ambao ni wananchi, na kwamba hiyo ndiyo sababu ya kuwapo kwa mwitikio mdogo.

“Baadaye watauzoea na kuelewa umuhimu wake tofauti na tiketi za karatasi. Tatizo kubwa hapa hatuna mashine za kutosha, ingawa wakati mwingine hulazimika kuongeza mashine moja,” anasema Joseph.

Pamoja na ugeni wa teknolojia hiyo eneo la Kivukoni, Joseph anasema unapendwa na wengi kwani umerahisisha huduma bila foleni na kuondoa msongamano.

“Ni rahisi sana kuutumia na anayeishiwa salio anaweza kuongeza kwa urahisi kwa kutumia simu ya mkononi,” anasema.

Mfumo wa kutumia kadi za usafiri katika vivuko vya Kigamboni umeanza kutekelezwa wiki kadhaa zilizopita ukilenga kuondoa mfumo wa tiketi za karatasi.

Kuhusu suala la elimu, anasema imeshatolewa kiasi cha kutosha na kwamba awali ilipangwa tiketi za karatasi kuondolewa Mei 15, lakini muda umesogezwa mbele.

Jitihada za JAMHURI kumpata Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Japhet Masele, ziligonga mwamba kwani hakuwapo ofisini kwake na hata alipopigiwa simu hakutoa ushirikiano.

Badala yake, Masele akasema atakuwa na mkutano na waandishi wa habari ingawa hakutaka kulialika gazeti hili.

“Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari wewe utaangalia na kusoma nilichozungumza kwenye mitandao ya kijamii. Au kama hautaridhika, nipigie simu jioni,” anasema Masele.

Hadi gazeti linakwenda mitamboni, Masele hakupokea simu. 

By Jamhuri