Bunge la Uingereza kulipata kuwa na Mbunge aliyeitwa William Wilberforce. Kila aliposimama bungeni kuzungumza, alidai kuwa utumwa ukomeshwe. Ndipo sheria ya kukomesha utumwa katika makoloni ya Uingereza ikapitishwa mwaka 1807.

Nami nafuata mfano wake. Nimeamua kuiandama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hadi hapo Serikali itakapoinyoosha.

 

Nina sababu nne za kuiandama wizara hii. Kwanza, naijua vizuri wizara hii. Nilikuwa mwalimu, nilikuwa mkuu wa shule (headmaster), nilikuwa Mtanzania wa kwanza kupelekwa nchi za nje na Serikali ya Mwalimu Nyerere kwenda kuchukua mafunzo ya uandishi na uchapishaji vitabu (Uingereza), nilikuwa Afisa wa Vitabu wa kwanza mzawa Wizara ya Elimu, na tangu mwaka 1994 naendesha semina za walimu Dar es Salaam na mikoani. Kwa hivyo, nimeendelea kufuatilia kwa karibu utendaji wa wizara hii. Hakika naijua.

 

Pili, naendelea kuiandama wizara ya elimu kwa sababu ndiyo wizara inayoongoza Tanzania kwa uozo.

 

Tatu, naiandama wizara hii kwa sababu viongozi wake si wasikivu, ni wakaidi kupindukia. Wameendelea kuendesha masuala ya elimu kibabe bila kujali maoni ya wadau wa elimu wakiwamo walimu. Nne, viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wameshikilia kwamba hawawezi kujiuzulu kwa sababu yoyote ile kana kwamba ni watu safi sana. Hapa naanika ukweli wa mambo.

 

Nikumbushe tu kwamba mwaka jana kabla Bajeti ya Elimu haijasomwa bungeni, niliandika kwenye gazeti la RAI makala tatu nikizungumzia kwa undani uozo wa wizara ya elimu. Lakini hayupo mbunge aliyetumia makala hizo kuibana wizara. Leo, baada ya wanafunzi wa kidato cha nne kufanya vibaya  mitihani yao, tunasikia kelele zinazotaka Waziri wa Elimu na wasaidizi wake wajiuzulu. Na wamegoma kujiuzulu. Hawahusiki moja kwa moja na matokeo hayo.

 

Lakini nimeamua kulitangazia Bunge viongozi na watendaji wakuu wa wizara walivyovuruga elimu kwa kiasi kikubwa, kwa kugeuza shule za umma kuwa dampo la vitabu vibovu. Na vitabu hivyo ni kwa ajili ya watoto wa maskini.

 

Katika mwendelezo wa semina ninazoziendesha kwa ajili ya walimu, Jumatano April 10, mwaka huu niliendesha semina ya uraia Shule ya Msingi Kinondoni, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam. Semina hiyo ilifunguliwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni aliyepata nafasi ya kujionea chati za uraia zilizotengenezwa na walimu.


Walimu wametengeneza chati hizo kutokana na maelezo yaliyomo kwenye vitabu vya uraia vilivyopitishwa na Wizara ya Elimu. Nyingi zilikuwa na makosa na upotofu wa kutisha. Kuhusu vitabu vya shule, walimu wamepiga kelele kwa mambo matatu.

 

Kwanza, matumizi ya vitabu vingi vya kiada kwa somo moja kwa darasa moja yamevuruga sana elimu. Hii ni kwa sababu vitabu hivyo vinatofautiana katika maelezo kiasi kwamba walimu hawajui ukweli uko wapi. Waziri wa Elimu wa zamani, Profesa Jumanne Maghembe, aliwaunga mkono walimu kwa  asilimia 100.

Lakini kwa sababu watendaji wakuu wa Wizara wameendelea kujitajirisha kwa asilimia kumi kutokana na utitiri huu wa vitabu vya kiada, walimpuuza Maghembe. Na leo Waziri wa sasa wa elimu na Naibu wake wamejiunga upande wa watendaji wakuu wa wizara, wanashiriki hujuma hii dhidi ya shule za watoto wa maskini kwa kugeuza shule hizo kuwa dampo la vitabu vibovu.

 

Pili, walimu wameendelea kulalamika kwa kupelekewa shuleni vitabu vya masomo ambavyo havitumiki kama vya stadi za kazi na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama). Havitumiki kwa sababu shule hazina vifaa vya kufundishia masomo hayo, tena walimu hawakupewa mafunzo yoyote kuhusu ufundishaji wa masomo hayo. Kwa hivyo, vitabu hivyo pia ni sehemu ya vitabu vibovu mradi kila mwaka watendaji wakuu wa wizara wanaendelea kupata asilimia kumi yao kutoka kwa wachapishaji.

 

Tatu, walimu wameendelea kulalamikia kitendo cha Wizara kutoa zabuni kwa wachapishaji, inayowaruhusu kuchapisha upya vitabu ambavyo walimu wameona siku nyingi kwamba havifai.

 

Na sasa inadaiwa kuwa baadhi ya walioko wizarani wameamua kugawana na rafiki zao Sh bilioni 56.9 za rada. Ni kashfa nzito na hujuma kwa shule za watoto wa maskini. Wamegawa zabuni bila kuzishindanisha.

Natoa mwito kwa wabunge wenye uchungu na elimu na watoto wa maskini, kama akina James Mbatia, kuhakikisha fedha hizo za rada hazitumiki kuchapisha upya vitabu visivyofaa. Wabunge wenye uchungu na fedha za umma wanadai kuundwa mara moja kwa kamati itakayochunguza matumizi ya fedha za rada. Umma wa Tanzania unahitaji kujua mambo mawili.

 

Kwanza, kwanini wizara imeamua kuchapisha upya vitabu vya zamani bila kwanza kukusanya maoni ya walimu waliovitumia? Wao wangeamua vitabu vipi vichapwe upya na marekebisho yapi na vipi visichapwe tena.

 

Pili, tunataka tujulishwe kwanini wizara imetoa kazi ya kuchapa vitabu hivyo kwa kujuana. Zabuni zimetolewa bila ushindani, kampuni zimeteuliwa tu. Tunaambiwa kampuni nyingine zilizopewa kazi hiyo ni za watu wa hapo hapo wizarani.

 

Nyingine zilichapa vitabu miaka mingi iliyopita na vimepitwa na wakati. Lakini vinapelekwa kutumika shuleni. Kampuni nyingine ni mpya kabisa kutoka nchi za nje na hazijawahi kuchapa vitabu vyovyote kwa ajili ya shule za Tanzania. Kubwa zaidi kampuni ziliteuliwa tu hakuna zabuni iliyotangazwa.

 

Bunge lisiruhusu ufujaji huu wa fedha za umma. Lizuie kabisa shule zetu kugeuzwa dampo kwa kupelekewa vitabu vibovu kwa maslahi ya watu wachache wasio na uchungu na watoto wa maskini. Nami nitatoa ushirikiano mkubwa kwa kamati yoyote itakayoundwa na Bunge kuhusu suala hili.


1042 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!