Wizara isiwapuuze Botswana

Katika gazeti la leo tumechapisha habari za uchimbaji wa madini nchini Botswana na jinsi wakazi wa nchi hiyo wanavyonufaika. Tumempeleka mwandishi Botswana kufuatilia habari hizo na amekuja na maelezo yenye kutia moyo kuwa nchi yetu ikipata watumishi wanaoitanguliza nchi, Tanzania inaweza kufuta umaskini.

Botswana inategemea almasi kwa mauzo ya nje kwa asilimia 89 ya pato la taifa kwa fedha za kigeni. Nchi hiyo imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini, ikiwamo kuanzisha, kusimamia minada ya madini, ukataji, uhifadhi na kampuni ya madini ya taifa lao. Pia kampuni zinazochimba almasi na madini mengine zinamilikiwa kwa ubia na serikali kwa uwiano wa hisa 50 kwa 50.
Waziri wa Nishati wa Botswana, Onkokame Mokaila, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba Serikali ya Botswana na mwekezaji, De Beers Group, waliingia mkataba wa miaka 10, mwaka 2011 na kwamba mkataba huo utadumu hadi mwaka 2021. Mkataba huo unahusu kuchambua, kuthamini na kuuza almasi inayochimbwa kupitia Kampuni ya Debswana.

Anasema sehemu ya makubaliano ya kimkataba yalihusisha Kampuni ya De Beers Group ambayo ni mbia, kuhamishia nchini Botswana shughuli zake za kuuza almasi ghafi, jambo ambalo linaifanya nchi hiyo kuwa moja ya nchi zinazonufaika kwa rasilimali. Mwaka jana Tanzania imepitisha sheria mbili za kuimarisha mapato ya nchi katika sekta ya madini.

Sheria hizo ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017, ambapo sheria hii inaweka utaratibu ambao wananchi kupitia chombo chao cha uwakilishi ambacho ni Bunge, kitapitia na kujadili makubaliano na mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi, ambayo imeingiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujiridhisha na masharti.
Sheria ya pili ni Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017.  Sheria hii inaweka masharti yatakayohakikisha kwamba hatua yoyote inayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za taifa inatambua na kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama taifa huru, lenye mamlaka ya kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa masilahi ya taifa.

Waziri huyo pia ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa mwaka 2016 Tanzania iliomba kutuma wataalamu wake nchini Botswana kujifunza inavyonufaika na sekta ya madini, lakini pamoja na kujibu maombi hayo, Tanzania haikupeleka wataalamu hao.
Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila, ameulizwa na Gazeti la JAMHURI akasema haoni kama Tanzania ina cha kujifunza kwa Botswana, kwani Botswana inakuja kujifunza Tanzania.
Kwa mwandishi wetu aliyoyashuhudia Botswana, tunadhani msimamo wa Prof. Msanjila usiwe msimamo rasmi wa Serikali ya Tanzania. Botswana inaongoza duniani kwa uchimbaji wa almasi na ni mfano bora wa jinsi serikali inavyopata mapato kutokana na uchimbaji na uuzaji wa madini si kwa Afrika pekee, bali duniani. Kuwabeza kuwa hatuna cha kujifunza Botswana, tunaamini ni kuwakosea Watanzania na Mungu aliyetuleta duniani. Fursa hii kama bado ipo tunaomba nchi yetu iichukue. Tunalo la kujifunza kutoka Botswana.