Na Deodatus Balile, aliyekuwa Mombasa

Kuna kila dalili kuwa mwanasiasa Raila Amolo Odinga (73), miaka minne ijayo atachaguliwa kuwa Rais wa Kenya, yaani mwaka 2021.
Hivi karibuni nimepata fursa ya kuwa jijini Nairobi na baadaye nikasafiri hadi Mombasa, ambako nimepata fursa ya kukaa na watu wa kada mbalimbali wanaozifahamu siasa za Kenya.
Sitanii, katika nyakati tofauti watu niliozungumza nao hitimisho lao linaelekea huko huko, kuwa mwaka 2021 ni zamu ya Odinga kuwa Rais wa Kenya. Wanasema Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, ana historia isiyoelezeka katika suala la utajiri alionao na hilo sasa linawakera Wakenya.
“Ruto amekuwa tajiri ghafla. Uhuru tunaelewa kuwa utajiri wake ni wa urithi, kutoka kwa Muzee [Jomo Kenyatta], lakini Ruto chachachachaaaa, sijui niseme nini,” haya ni maneno aliyoniambia muuza duka ambaye awali alikuwa mfuasi wa Ruto jijini Nairobi.

Ruto pia pamoja na kwamba aliukwepa mkono wa sheria kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (The Hague), bado jamii haijamsamehe. Wanasema alichangia kwa kiasi kikubwa vurugu za mwaka 2007 zilizopoteza maisha ya Wakenya wengi, kwani alikuwa akifadhili vikundi vya Mungiki.
Uhusiano kati ya Uhuru na Ruto nao unaleta maswali mengi. Kwa siku za karibuni Uhuru Kenyatta amekuwa akitaka kila mtu ataje mali alizonazo. Amemtuma Odinga kuiwakilisha nchi kwenye mazishi ya Kofi Annan na akamtuma kuiwakilisha nchi katika ziara ya kikazi India.

Sitanii, itakumbukwa Odinga na Kenyatta walikutana katika sala ya asubuhi jijini Nairobi, ambapo waliombana msamaha hadharani. Wakasema Kenya ni kubwa zaidi yao. Wakaamua kuijenga Kenya. Nimeelezwa jambo jingine. Kuwa Uhuru Kenyatta anataka kuweka historia ya kufuta ukabila.
Kwa Uhuru kuwa Mkikuyu, anaona akimpatia urais Odinga, ambaye ni Mluo, basi atakuwa amesimika nguzo ya kufuta ukabila nchini Kenya. Si hilo tu, Wakenya wengi sasa bila kujali ukabila wao wanaanza kuangalia Odinga mambo aliyolifanyia taifa hilo. Kubwa wanazungumzia mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo.

Wanazungumza kuwa kama si Odinga, Kenya isingepata Katiba mpya bora kabisa. Katiba hiyo inawapa uhuru wa kutosha. Mji kama Mombasa, ambako wengi wanamwita Odinga ‘Baba’ wanasema kama si Odinga, tayari walikuwa wamepelekwa utumwani. Fukwe zote zilikuwa zimevamiwa na wawekezaji baharini na ilikuwa tabu kwa mwananchi wa kawaida kufika ufukweni.
Kwa sasa Katiba mpya imetamka kuwa fukwe ni rasilimali ya umma, inayomilikiwa na Wakenya kwa pamoja. “Unaona hapa mchangani, katika ufukwe wa bahari wala miaka michache iliyopita usingefika hapa. Walinzi wa hii hoteli wangeweza kukupiga hata risasi. Ilikuwa wamejenga vizuizi vingi tu, lakini baada ya Katiba mpya kupitishwa vyote vimebomolewa. Unajua yote haya kaleta nani? Ni kazi ya ‘Baba’,” ameniambia kijana mmoja.
Sitanii, harakati za kisiasa za Odinga unaweza kusema zilianza rasmi mwaka 1982 alipokamatwa kwa tuhuma kuwa alitaka kumpindua Rais Daniel arap Moi na akafungwa jela miaka sita bila kupitia mahakamani. Alipotoka gerezani, alikamatwa mara kadhaa kati ya mwaka 1989 na 1990 kwa madai kuwa alikuwa anafanya kampeni za kupinga mfumo wa chama kimoja.

Mwaka 1991, alikimbilia nchini Norway kama mkimbizi wa kisiasa. Mwaka 1992 alirejea Kenya na kuchaguliwa kuwa mbunge kupitia Chama cha FORD-K. Chama hiki kilikuwa kinaongozwa na baba yake, mzee Jaramogi Oginga Odinga. Mzee Jaramogi alipofariki dunia mwaka 1994, Raila alianza mapambano ndani ya chama na ilipofika mwaka 1996, akakihama na kwenda NDP.
Mwaka 1997 aligombea urais na mzee Moi, ila akashindwa. Hata hivyo, alishinda ubunge na akaamua kujiunga na KANU ambapo mwaka 2001, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati. Mwaka 2002 alitarajia angeteuliwa kwa tiketi ya KANU kuwa mgombea urais, lakini Moi akamteua Uhuru Kenyatta kuwa ndiye mgombea wa KANU. Raila akaihama KANU akaungana na Mwai Kibaki, wakaunda muungano wa NARC uliomshinda Uhuru. Kibaki akawa rais, na wakapata wabunge zaidi ya nusu. Je, unajua nini kiliendelea baada ya hapo? Usikose toleo lijalo.

Please follow and like us:
Pin Share