Seoul, Korea Kusini

Rais mstaafu wa Korea Kusini, Lee Myung-bak, amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela pamoja na faini ya dola za Marekani milioni 11.5 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 25) kutokana na kukutwa na hatia ya makosa kadhaa ya rushwa.
Rais Lee alihukumiwa katika Mahakama ya Seoul wiki iliyopita kwa tuhuma za rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Tukio hilo linamfanya Rais Lee kuingia katika mkumbo wa marais wastaafu wanne ambao mpaka sasa wamefungwa kutokana na kukutwa na hatia baada ya kumaliza vipindi vyao vya uongozi.

Mtangulizi wa Rais Lee alihukumiwa kifungo Aprili mwaka huu kutokana na kukutwa na hatia katika shauri lililohusu rushwa. Lee amekuwa Rais wa Korea Kusini katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2008 hadi 2013.
Rais Lee alikamatwa Machi mwaka huu jijini Seoul, baada ya kufikishwa mahakamani alikana tuhuma dhidi yake huku akisisitiza kuwa tuhuma hizo zilikuwa na msukumo wa kisiasa.
Lee mwenye umri wa miaka 76 hakuhudhuria hukumu yake jijini Seoul kama ishara ya kupinga kesi dhidi yake. Hukumu ya kesi hiyo ilionyeshwa mubashara na runinga nchini humo. Mara kadhaa amekana tuhuma dhidi yake na kusisitiza kuna mkono wa kisiasa. Mwendesha mashtaka alitaka Lee afungwe miaka 20 jela.

Mahakama hiyo ya jijini Seoul ilitoa uamuzi kwamba Lee alikutwa na hatia ya kupokea hongo kutoka kwa kampuni kubwa nchini Korea Kusini, ikiwemo Samsung pamoja na idara ya usalama nchini humo.
Pia alikutwa na hatia ya kufuja dola za Marekani bilioni 24 (zaidi ya Sh trilioni 55) kutoka kwenye kampuni kadhaa nchini humo ambazo anahusishwa na umiliki wake.
Katika utetezi wake alisema kampuni hizo zilizo chini ya mwavuli wa DAS, zinamilikiwa na mdogo wake, lakini mahakama ilithibitishiwa pasipo shaka kwamba zinamilikiwa na Lee.
Sehemu ya hukumu hiyo inasomeka: “Katika kuweka mambo kadhaa sawa, adhabu kubwa kwa mtuhumiwa haiepukiki.”

Wakati wa shauri hilo mahakama ilijiridhisha kwamba Kampuni ya Samsung ilimlipa Rais Lee kiasi cha dola za Marekani bilioni sita ili aweze kutoa msamaha kwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo, Lee Kun-hee, aliyekuwa amefungwa kwa kosa la kukwepa kodi.
Marais wengine wa Korea Kusini ambao wamewahi kukutwa na masaibu kama ya Rais Lee ni pamoja na Chun Doo-hwan, aliyekuwa rais kati ya mwaka 1980-88, na Roh Tae-woo, aliyekuwa rais wa nchi hiyo mwaka 1988 hadi 1993. Wawili hao kwa nyakati tofauti walikutwa na hatia ya kula rushwa pamoja na uchochezi, baadaye waliachiwa huru.

Please follow and like us:
Pin Share