Mtandao wa utapeli unaowahusisha
wafanyabiashara na watendaji wakuu wa
baadhi ya taasisi za serikali umebainika
kuwapo kwenye biashara ya usafirishaji wa
magari nje ya nchi (IT).

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa
miezi mitatu umebaini mtandao huo
unaowahusisha baadhi ya watendaji
waandamizi katika Bandari ya Dar es
Salaam, Wakala wa Usafiri wa Nchi Kavu
na Majini (SUMATRA) na kampuni za bima.
Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato
Zambia (ZRA) Kanda ya Kaskazini, Joe
Simwanza, amezungumza na JAMHURI
ofisini kwake mpakani Nakonde, Zambia na
kusema utapeli huo unatishia kuua biashara
ya usafirishaji wa magari yanayokwenda
nchini humo kupitia Bandari ya Dar es
Salaam.
Anasema yamekuwapo malalamiko mengi
na ya muda mrefu ya Wazambia kuhusu
utapeli huo, lakini hakuna hatua
zilizochukuliwa na mamlaka upande wa
Tanzania kumaliza kero hiyo.
Kwa sasa Serikali ya Msumbiji iko kwenye
upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Beira,
na kukamilika kwake kunaelezwa kuwa
huenda kukadhoofisha usafirishaji wa
magari na shehena nyingine kupitia Dar es
Salaam.

Uchunguzi umebaini kuwa karibu magari
300 yanasafirishwa kwenda nje kupitia
Bandari ya Dar es Salaam kila siku,
ambapo wenye magari hayo wanauziwa
bima za kitapeli.
Bima hizo hazina viwango maalumu vya
malipo, badala yake kinachofanywa ni
makubaliano kati ya muuzaji na mnunuzi.
JAMHURI tumenunua baadhi ya bima hizo
kwa kiwango cha Sh 15,000; Sh 20,000 na
Sh 25,000 kwa kila stika. Pia tumenunua
bima ya COMESA (Umoja wa Soko la
Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika) kwa Sh 40,000. Tanzania ilijitoa
katika umoja huo mwaka 1999.
Nchi wanachama wa COMESA ni Burundi,
Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC), Djibouti, Misri, Eswatini
(Swaziland), Eritrea, Ethiopia, Kenya,
Libya, Madagascar, Malawi, Mauritius,
Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan,
Tunisia, Uganda na Zambia.
Shirika la Bima la Taifa (NIC) ndilo
lililokabidhiwa dhima ya kuuza stika za
COMESA; lakini kwa sasa zinauzwa mitaani

kama njugu zikiwa zimerudufiwa.
Msimamizi wa uuzaji wa stika hizo kutoka
NIC aliyejulikana kwa jina la Holo,
amekataa kuzungumza kwa masharti kuwa
hadi apate kibali kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa NIC, Samwel Kamanga. Hata
hivyo, Kamanga hakuweza kupatikana
kutoa kibali kwa kile kilichoelezwa kwamba
alikuwa kwenye mkutano wa wadau wa
bima mkoani Tanga.
Stika za kampuni za bima zinazouzwa kwa
wanaosafirisha magari ya IT zinapatikana
hadharani, lakini wakati mwingine kwa
kificho pale polisi wanapokuwa
wakiendesha msako wa kuwakamata
wahusika.
Zimezagaa katika maeneo yote
yanayozungumza Bandari ya Dar es
Salaam na katika vibanda vilivyopo Mnara
wa Saa, Water Front, Gate No. 2, Dawasa,
Mnazi Mmoja na Kariakoo.
Hapo Kariakoo, yupo mtaalamu wa
kurudufisha stika hizo anayejulikana kwa
jina maarufu la Mjaluo. Kwa Mjaluo, kitabu
cha stika huuzwa kuanzia Sh 250,000 hadi

Sh 400,000 na mteja anapata stika za
kampuni yoyote ya bima anayohitaji.
Kutoka kwake, walanguzi ndipo hupata stika
wanazokwenda kuuza rejareja. Kwa
kufanya hivyo, ndiyo maana bei ya stika
hubadilika kulingana na muuzaji
anavyomwona mnunuzi alivyo.
Wanauza kuanzia Sh 15,000 alimradi
kuhakikisha wanapata faida kutoka kwenye
kiwango walichonunua kitabu kutoka kwa
Mjaluo.
JAMHURI limetumia nyaraka za magari ya
IT yaliyokwisha kusafirishwa nje ya nchi
kununua stika mpya za bima. Limetumia
nyaraka hizo kununua stika za bima kutoka
kwa kampuni tano tofauti tofauti jijini Dar es
Salaam, bila hata wahusika kuona magari.
Namba za stika zilipoingizwa kwenye
mtandao wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Bima Tanzania (TIRA), zilisomeka kuwa
zimeshatumika. Hata hivyo, bado stika hizo
feki zinaweza kutumiwa kwa kubandikwa
kwenye gari lolote la IT. Kwa kawaida,
namba za magari ya IT huwa ni tarakimu
nne za mwisho za chesesi ya gari husika.

Mtandao wa fedha

Waagizaji wa magari kutoka mataifa ya
Zambia, Malawi, DRC, Rwanda, Burundi na
Uganda hutakiwa kulipa dola 200 (wastani
wa Sh 450,000) za bima kwa gari. Fedha
hizo hulipwa ili pamoja na mambo mengine,
zigharimie bima ya gari kuanzia linakotoka
hadi kwa mmiliki. Kiasi hicho pia huhusisha
malipo ya dereva wa kulipeleka hadi
mpakani.
Bima hizo zimebainika kuwa si lolote, wala
chochote, kwani magari mengi ya IT
yanapopata ajali madereva kwa kuwa ni
sehemu ya mchongo huo huzibandua na
kutoweka.
Licha ya wanunuzi wa magari kutozwa
fedha za kutosha kuwalipa madereva
wanaopeleka magari hayo mipakani,
imebainika kuwa baadhi ya kampuni za
uwakala huwalipa madereva wao Sh
300,000 kwa mwezi, na Sh 100,000 kwa
kila gari wanalopeleka mpakani.
Kiwango hicho kidogo cha fedha kinaelezwa

kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya
madereva hao wawe kwenye mwendo kasi
muda wote, hivyo kupata ajali mara kwa
mara.
“Dereva analipwa Sh 100,000. Humo
anatakiwa ale, na ikiwezekana alale
nyumba ya wageni, akifanya yote hayo
habaki na kitu,

” kimesema chanzo chetu.
Kwa kukabiliana na hilo, magari hayo
yamekuwa yakisafirishwa usiku, tena
yakiwa yamepakiwa abiria ingawa sheria za
usalama barabarani zinazuia.
Madereva wanapoendesha usiku
uhakikisha wanawasili Tunduma mapema
alfajiri na hapo hukabidhi gari kwa wahusika
kabla ya kupanda mabasi ya alfajiri hiyo
hiyo kurejea Dar es Salaam.
“Tunafanya hivyo kukwepa kulala gesti.
Ukilala gesti utakosa nauli ya kurudi Dar es
Salaam,

” amesema dereva mmoja.

Wanaofaidi fedha za bima

Imeelezwa kuwa fedha zinazotokana na
utapeli kwenye stika za bima ni mapato ya

mtandao mahususi wenye nguvu na
ushawishi.
Baadhi ya wahusika tuna majina na vyeo
vyao, lakini kwa sababu za kitaaluma
tunaendelea kuwahifadhi hadi hapo
tutakapozungumza nao. Baadhi yao
wameulizwa na kuahidi kutoa majibu
baadaye.
Miongoni mwao ni baadhi ya watendaji
waandamizi katika Bandari ya Dar es
Salaam, SUMATRA na mfanyakazi mmoja
mwanamke katika Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA). Mwanamke huyo ana
watoto wake wawili wanaofanya kazi ya
uwakala wa kununua na kuuza magari
ughaibuni.
Uchunguzi umebaini kuwa kigogo wa
Bandari ya Dar es Salaam ni mbia kwenye
mpango wa kuajiri madereva
wanaosafirisha magari ya IT pamoja na
uuzaji wa stika hizo za bima.

Ajali za magari

Mwandishi wa habari hizi amesafiri hadi

Mbala, Zambia na kushuhudia magari
mengi yaliyopata ajali upande wa Tanzania
yakiwa yametelekezwa njiani – katika vituo
vya polisi na kwenye yadi nchini Zambia.
Magari yanayopata ajali mbali na Tunduma
yamehifadhiwa katika vituo vya polisi, lakini
yaliyopata ajali kuanzia Mbeya na
kuendelea, hukokotwa na kampuni ya
uwakala [jina tunalo] na kuyavusha hadi
kwenye yadi nchini Zambia.
Baadhi ya maeneo ambako kuna magari ya
IT yaliyopata ajali ni Kituo cha Polisi Mikumi,
Iringa, Ifunda na Makambako nchini
Tanzania. Kwa upande wa Zambia, magari
hayo yako kwenye eneo linaloitwa “Yard ya
Mzungu”

, Barabara ya Mbala, kilometa

kadhaa kutoka mpakani Nakonde.
Magari hayo kabla ya kuhamishiwa “Kwa
Mzungu” yalikuwa kwenye yadi ya Inland
Investment Limited, iliyopo Nakonde. Yadi
hiyo kwa sasa inakarabatiwa.
Baada ya ajali madereva huyaletekeza,
hivyo walioyanunua hukosa vyote – gari na
fidia. Kule yanakohifadhiwa, imebainika
kuwa vifaa vingi huibwa na waliopewa

dhamana ya kuyalinda.
“Tunapokea malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi (Zambia), gari linapoharibika
kabisa hawana namna ya kulipwa fidia licha
ya kuyakatia bima, hii inasikitisha sana,

anasema Naibu Kamishna Simwanza wa
ZRA.
Kituo cha Polisi Ifunda kumetunzwa magari
kadhaa ya IT yaliyopata ajali na kuua
waenda kwa miguu na abiria, lakini hakuna
maelezo ya madereva wala wamiliki wake.
Polisi aliyezungumza kwa masharti ya
kutotajwa jina anasema ajali zaidi ya
asilimia 90 hutokea alfajiri au asubuhi,
muda ambao madereva huwa wamechoka.
Pamoja na kuutumia usiku kusafiri ili
wawahi kurejea Dar es Salaam kwa mabasi
ya asubuhi, sababu nyingine ya kusafiri
kwao usiku ni kutokana na kuwakwepa
polisi kutokana na mwendokasi na kupakia
abiria.
Katika mji wa Mbala, mabaki ya magari ya
IT zaidi ya 30 yameonekana, na kama ilivyo
kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
ZRA huuza mabaki hayo baada ya muda

uliopangwa wa miezi mitatu kupita bila
wenyewe kujitokeza kuyachukua.

Je, bima ni halali?

Sheria ya Usalama Barabarani inaagiza
kuwa chombo cha moto kilichosajiliwa
nchini lazima kiwe na bima. Gari lenye
namba za chesesi, kwa mujibu wa sheria,
halijasajiliwa nchini.
Sheria inatoa mwanya kwa gari kutolewa
bandarini hadi nyumbani au karakana likiwa
na kibao maalumu cha kuonyesha kuwa
halijasajiliwa. Malipo kwa kibao hicho ni Sh
5,000.
Magari ya IT, kwa kuzingatia sheria hiyo,
hayana usajili hapa nchini, badala yake
namba (tarakimu nne) zinazoonekana
kwenye kibao cha utambulisho wa gari ni za
kwenye chesesi. Wataalamu wa usalama
barabarani wanasema kwa kuzingatia
sheria hiyo, ni makosa kulikatia gari bima
kwa kutumia namba za chesesi.
“Mfano mzuri ni bima ya nyumba. Huwezi
kukatia bima matofali au mifuko ya saruji

iliyoko dukani. Hata nyumba ikijengwa
lazima kiwanja kiwe na hati ndipo ukikatie
bima. Sasa kukatia bima magari kwa
kutumia chesesi ni sawa na kukatia bima
nyumba kwa kutumia matofali,

” amesema

mtaalamu huyo.

Msimamo wa TIRA

Ofisa Mawasiliano wa TIRA, Oyuke
Filemon, anasema bima za magari ya IT
(yellow card) zinatolewa na Shirika la Bima
la Taifa (NIC).
Anasema ingawa Tanzania si mwanachama
wa COMESA, mizigo mingi ya nchi
wanachama zilizo Kusini, Mashariki na Kati
mwa Afrika inapitia Tanzania.
“Kama kuna kampuni tofauti
zinazotoa yellow card, inapaswa wapate
kibali kutoka NIC,

” anasema.

Oyuke anasema bima zinazotambulika kwa
magari ni mbili –Third
Part na Comprehensive kwa magari
yaliyosajiliwa nchini. Third part, pamoja na
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni Sh

118,000; ilhali comprehensive hutegemeana
na thamani ya chombo kinachokatiwa bima,
thamani ya chini ikiwa ni asilimia 5 ya
thamani ya gari.
Anakiri kuwa mara kadhaa maofisa wa
TIRA wameshirikiana na polisi kuwakamata
wanaojihusisha na uuzaji wa stika feki za
bima.
“Tuna kikosi chetu cha udhibiti dhidi ya
wanaokiuka sheria za bima, tunajua pale
nyuma ya TPA (Mamlaka ya Bandari) ndiyo
wanauzia hapo,

” anasema Filemon.

Wakati Oyuke akisema hivyo, Meneja wa
Mifumo wa TIRA, Aron Mlaki, anasema
bima za muda mfupi (short cover)
zinatambulika na ni mahsusi kwa ajili ya
kuwalipa watu wanaopata ajali au madhara.
Kamishna Mkuu wa TIRA, Dk. Baghayo
Saqware, amezungumza na JAMHURI
ofisini kwake Dar es Salaam na kusema
suala la magari ya IT ni changamoto kubwa.
Anasema kumekuwapo magenge ya
wanaouza stika feki za bima na TIRA
imejitahidi kukabiliana nao.
Anasema Mamlaka inaangalia namna ya

kuingiza yellow card za COMESA kwenye
mfumo wa TIRA wa utambuzi ili kukabiliana
na wimbi hilo.
“Tunashindwa kuingilia moja kwa moja hili
suala kwa sababu ni la kikanda, kuna
mikataba iliyosainiwa kwa ajili hiyo kwa hiyo
tunapaswa kufuata taratibu,

” anasema Dk.

Saqware.
Anasema kwenye mabadiliko ya kisheria
yaliyofanywa, mizigo inayoingia nchini kwa
maji, barabara na anga sasa inakatiwa bima
hapa hapa nchini.

Kauli ya Polisi Usalama Barabarani

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani Tanzania, Fortunatus Musilimu,
anasema chombo cha moto hakiwezi
kukatiwa bima kama hakijasajiliwa.
“Kama gari linatolewa bandarini kwenda
nyumbani, na likiwa halina bima,
kinachofanywa ni wakala kukata kibao cha
gereji. Hizo namba sheria inataka gari
litembee mwisho saa 12 jioni. Baada ya
hapo halitakiwi kutembea.

“Na iwe kweli hilo gari linatolewa bandarini
kwenda nyumbani likisubiri bima, au
kwenda gereji; na si kinyume cha hivyo.
Likikutwa nje ya hapo linatembea
litakamatwa kwa mujibu wa sheria. Siku hizi
mambo mengine ni online [mtandao], kwa
hiyo gari linaweza kulipiwa bima online na
likatolewa bandarini likiwa na bima. Hiyo ni
kwa magari yanayosajiliwa hapa nchini.
“Hizo bima za kwenye IT hapo ni
ubabaishaji. Najua zipo bima za COMESA
ambazo ni halali kisheria. Lakini hizi
nyingine ni uhuni tu, pale kuna uhuni, lakini
uhakika wa haya utaupata TIRA,

” anasema.

Anasema magari ya IT yana namba
yanazopewa Bandari, na kwamba mfumo
uliopo unawezesha zisomwe pia TIRA.
“Kuna ubabaishaji mwingi kwenye IT maana
hata madereva wakipata ajali wanabandua
hizo bima halafu wanakimbia. Kama bima ni
halali kwanini wabandue bima na
wakimbie? Kuna matapeli wengi sana,

anasema.
Kamanda Musilimu anasema bima za
COMESA zinapigwa vita, na sababu kuu ya

kuwapo vita hiyo ni masilahi ya makundi
yanayojitafutia fedha.
“Wanapigwa vita, ni vita kweli kweli wala
siyo ndogo,

” anasema Kamanda Musilimu.
Usikose matoleo yajayo kusikia kauli ya
Bandari, TRA na SUMATRA.
Uchunguzi huu umefanywa kwa ushirikiano
kati ya Gazeti la JAMHURI na Wakfu wa
Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).

Itaendelea…

By Jamhuri