Na Alex Kazenga, Dar es Salaam

Maofisa Ardhi wa Manispaa ya Temeke jijini
Dar es Salaam wanatuhumiwa na wananchi wa
Kata ya Yombo – Makangarawe kwa kuendesha
zoezi la utoaji wa hati za viwanja kwa njia za
rushwa.
Tuhuma hizo zinatokana na ofisi hiyo kudaiwa
kuwatoza wananchi Sh 50,000 za kufuta hati za
makazi bila kuwapa risiti wanapofika ofisini
kufuatilia hati za viwanja vyao.
Wananchi 71 waliitikia wito wa kupima viwanja
vyao kwa mujibu wa agizo la serikali, lakini
wananchi saba hawajapata hati kutokana na
kikwazo cha kudaiwa Sh 50,000 kwa ajili ya
kufuta hati za makazi.
Wananchi wanalalamika kuwa tayari wamelipa
gharama zote za kisheria ila wanashangaa
kuambiwa walipe fedha za kufuta hati za
makazi bila kupewa risiti.

“Ukifika pale unaombwa utoe hela ya chai ili faili
lako liende haraka, usipotoa wanakuzungusha
sana, ukiwauliza wanakwambia bado
linashughulikiwa na kwamba mchakato wake
unachukua muda,” amesema mmoja wa
wananchi hao ambaye hakupenda jina lake
litajwe.
“Wanasema ‘hatuna karatasi na kompyuta
hazifanyi kazi’” ameongeza mwananchi huyo.
Kwa mujibu wa wananchi hao, zoezi la upimaji
na urasimishaji wa viwanja hivyo limeanza
mwaka 2015 na kwamba upimaji wa viwanja
uligharimu takriban Sh 260,000 kwa mtu
mwenye kiwanja cha mita za mraba kuanzia
200.
Ofisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Temeke,
Alex Masoy, ameliambia JAMHURI kuwa yeye
si msemaji, hivyo akashauri aonwe Mkuu wa
Idara ya Mipango Miji aliyemtaja kwa jina la
Banyikila.
JAMHURI limemtafuta Rugambwa Banyikila,
ambaye naye amerusha mpira akisema yeye si
Msemaji wa Manispaa ya Temeke na kwamba
anayeweza kutoa ufafanuzi ni mkurugenzi wa
manispaa.
Amehoji ni kwanini Ofisa Ardhi Mteule

anayetakiwa kulitolea ufafanuzi anashindwa
kufanya hivyo na badala yake anataka yeye
ndiye alizungumzie?
Akahoji zaidi taarifa hizo za kupima viwanja
katika Manispaa ya Temeke ni za mwaka gani,
kwa sababu yeye tangu amehamishiwa hapo
miezi mitatu iliyopita hana taarifa za upimaji wa
viwanja katika eneo lolote la Temeke.
Kwa upande mwingine, Luka Chaula, Ofisa
Ardhi wa manispaa hiyo amesema wananchi
hawajaelewa utaratibu wa kupata hati mpya za
makazi.
Amesema mwananchi mwenye leseni ya
makazi kiwanja chake kinapopimwa leseni hiyo
inakosa nguvu, hivyo mwananchi anapaswa
kuisalimisha leseni hiyo ili aweze kuandaliwa
hati ya kumiliki kiwanja kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa leseni ya makazi
inamilikishwa kwa mwananchi kwa muda mfupi
na kwamba mwananchi akiwa na umiliki wa
leseni anapaswa kulipa ada ili apate hati na
utaratibu huo upo kisheria.
“Mtu aliyewasilisha leseni yake ya kumiliki
kiwanja anatakiwa kulipa ada ya Sh 50,000
ambayo ni ya kurudisha umiliki na hii ipo
kisheria na utaratibu wa kuilipa unaeleweka,”

amesema Chaula.
Ameongeza kuwa ada hiyo hulipwa kwenye
akaunti ya manispaa na kwamba risiti
anayopatiwa maelezo yake ndiyo hujazwa
kwenye hati ya utambulisho.
Amesema kuwa mwananchi anapomaliza
mchakato wa kulipa ada hiyo ndipo utaratibu
mwingine wa kumwandalia hati ya utambulisho
unaweza kuendelea.
Amefafanua kuwa gharama za matayarisho ya
hati za kiwanja hutegemeana na ukubwa wa
kiwanja cha mtu mwenyewe.
Ameongeza kuwa ni haki ya wananchi hao
kuhofia kwamba fedha zao zinaliwa endapo
utaratibu unaotumika kulipa ada hizo
hauzingatii utoaji risiti.
Ameshauri wananchi kufika ofisini na kukutana
na Ofisa Ardhi au Mkuu wa Idara ya Mipango
Miji wasaidiwe kueleweshwa kuhusu taratibu
hizo.
Gazeti la JAMHURI, toleo namba 267,
lililochapishwa Juni 6, 2017, lilikuwa na
malalamiko ya wananchi hao wakitaka zoezi la
upimaji viwanja lililofanywa na Manispaa ya
Temeke kwa watu 64 lifanyike kwenye viwanja
vyao pia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa ni kuwa
kati ya wananchi 71, wananchi saba
wameachwa nje ya upimaji, kwa hoja kwamba
viwanja vyao vilionekana kuwahi kupimwa siku
za nyuma na umiliki wake kuonekana upo kwa
watu wengine.
Watu hao walihoji umiliki wao unakuwaje na
shaka ilhali watu wote waliopakana nao umiliki
wao upo sahihi na kwamba miongoni mwao
ndio waliochangishana Sh 300,000 viwanja
vyao vipimwe na kumilikiwa kisheria.
Katika maelezo yao walimtaka Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi, kuingilia kati suala hilo kwani lilionekana
kuwanyima haki ya kupata mikopo na kuwapa
hofu ya kudhulumiwa viwanja vyao.

MWISHO

Please follow and like us:
Pin Share