Yah: Dakika zinayoyoma, sera zinauzika, kazi kwa wapambe

Kama ingelikuwa ni mashindano ya mpira, basi tungesema kipindi cha mapumziko kimeshapita na kipindi cha pili kinaelekea kwisha, pambano halihitaji kupigiana penalti mshindi lazima apatikane kwa matokeo yoyote.

Wachezaji wote wanatumia nguvu zao zote na kuangalia makosa madogo ya wachezaji wenzao, ili waweze kutumia mwanya huo kupata ushindi.

Siasa ni kazi, lakini siasa ni uongozi pia wa kushika dola, uongozi wa dola siyo kitu cha lelemama, kinahitaji weledi na hekima ya hali ya juu sana kwa kuwa linapofanyika kosa la kuuweka uongozi madarakani kwa miaka mitano siyo jambo dogo la kudharau, miaka mitano inaweza kuwa shubiri na miaka mitano inaweza kuwa bustani ya Eden kwa wapiga kura ambao wanasimika uongozi.

Mimi nina miaka ya kutosha, nimepiga kura awamu nyingi tangu enzi za kivuli na mtu, enzi za nyumba na jembe, enzi za matokeo mwezi mzima, enzi za kampeni bila hela, enzi zile za bila chopa na VX, enzi zile za bila khanga wala fulana, enzi ambazo wapambe walikuwa hawaruhusiwi, enzi za kutopata taarifa hata za kijiji cha pili, enzi za teknolojia ya taarifa ya habari RTD.

Kwangu mimi haya ni mabadiliko ya kufa, mabadiliko ya kuwa kichaa, mabadiliko ya kupata matokeo katika kipindi cha saa moja. Naiogopa teknolojia, lakini sina ujanja nayo kwa kuwa ninyi ndiyo mlioamua kukubali na kwenda na wakati, hili halina mjadala kwa kuwa ndiyo maendeleo.

Ni mabadiliko kwa kuwa kuna demokrasia ambayo hatukutarajia ujio wake, ni kama mwisho wa dunia umefika kwa mtu yeyote mwenye umri kama wangu mzee Zuzu, mabadiliko ya kumsema kiongozi aliyeko madarakani au chama kilichopo madarakani na usichukuliwe hatua za kinidhamu kama kufichwa au kuhojiwa na Serikali.

Huu ndiyo utawala bora ambao baadhi ya waliopata kuwa marais Tanzania wanapewa tuzo kila kukicha, kwa kuamua kwa dhati ya moyo wao kusambaza upendo kwa kuachia demokrasia ifanye kazi yake. Nayapenda mabadiliko japokuwa yananitisha kila ninapoangalia hatima yake. Hivi sasa kila mtu na kila chama kinajinadi ushindi wa mafuriko, kinanadi mafuriko ya wanachama na mashabiki katika mikutano ya hadhara, viongozi na wanachama wanaapiza ushindi wa kishindo. Sera zanamwagwa kwa uwazi na matarajio ya wapigakura ni makubwa pasi na hali halisi.

Leo nimeamua kuandika barua hii nikitaka kutoa wosia wangu juu ya kile ninachokiona, huenda kisitokee lakini kwa kuwa ya Mungu ni mengi basi ni vyema nikaja kukumbukwa kwa wosia wangu huu ninaodhani nitakuwa nimelitendea vyema Taifa langu na watu wake – Watanzania wenzangu.

Katika siasa yoyote duniani tunatakiwa tusiangalie sura ya mtu au chama, tunapaswa kuangalia sera za chama na jinsi kitakavyoendesha mambo yake baada ya kura zetu kuwasimika madarakani hao tunaotaka watuongoze.

Masuala ya urafiki na mazoea ni jambo lisilo na nasaba na uongozi wa nchi, kutaka mabadiliko ni jambo la maana lakini ni lazima yawe mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo siyo mabadiliko ya sura na utawala.

Tanzania ambayo naipenda, ningefurahi siku moja kuendelea kuiona ikiwa na amani ileile pamoja na demokrasia tunayojivunia, isiwe demokrasia ya matusi ambayo itaishia kushikana mashati na kuamua kupigana. Nisingependa kuona demokrasia iliyopo inatumika kuanzisha makundi ya uhasama na kuvuruga amani ambayo gharama yake ni kubwa kuliko tunavyodhani vichwani mwetu.

Ningelipenda niione Tanzania baada ya uchaguzi, ningelipenda niione amani baada ya matokeo, iwe kama ilivyokuwa wakati wa kivuli na mtu, jembe na nyumba, na sera na mtu. Inapotokea kukubali matokeo inamaanisha ukomavu wa kisiasa, kila penye ushindani ni lazima kukubali kushindwa na kushinda.

Fursa iliyopo ya demokrasia isiwafanye wananchi washibishwe kisichowezekana, suala la kupiga kura lisiwe sehemu ya kujineemesha maisha kwa siku moja, suala la kuamua umpigie nani kura lisiwe la kushawishiwa, kila mtu atumie haki yake ya kuchagua anayeridhika naye lakini pia mchaguaji awe na haki ya kukubali matokeo ya uongozi.

Mabadiliko ni muhimu sana, na mabadiliko ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo, mabadiliko hayaletwi kwa siasa yanaletwa kwa sera zinazotekelezeka, mabadiliko yanaletwa na viongozi wanaodhani wameamua kuitumikia jamii na siyo kujitumikia wao, mabadiliko siyo hadithi ni utendaji.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.