Katika kipindi kifupi tu tumeshuhudia kwa kiasi kukubwa Watanzania wakiimba wimbo wa mabadiliko. Wimbo huu unaimbwa na wanasiasa.

Kinachonipa ukakasi kutokana na neno hilo ‘mabadiliko’ kutawala katika vijiwe, mikutano ya hadhara na hata katika majukwaa makubwa yanayotumika kusaka kura kwa wagombea wetu, si neno lenyewe bali ni maana na dhamira ya mabadiliko yanayotakiwa.

Dk. John Magufuli, mgombea urais wa CCM, amesikika mara kadhaa akiongelea mabadiliko anayohitaji kuyaleta kwa Watanzania iwapo atapata ridhaa ya kuiongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.

Hali kadhalika, Edward Lowassa, mgombea kiti hicho kikuu katika Taifa hili, kwa mwavuli wa Ukawa akitumia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), naye katika ahadi zake ni mabadiliko. Hata hivyo, amekuwa akilitumia neno hilo hata kabla hajajiunga na chama hicho.

Aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, na mtu aliyekuwa akionekana kuwa shupavu na mwenye msimamo, Dk. Willibrod Slaa, ni miongoni mwa Watanzania walioimba wimbo wa mabadiliko. Hata hivyo, Dk. Slaa ameamua kuachana na siasa kwa muda. 

Nimeshangazwa na kile nilichokisikia kikitoka kinywani mwa kiongozi huyu. Wananchi wanaotafakari hatua aliyochukua Dk. Slaa na maneno aliyoyazungumza hadharani, wanabaini kuwa amejidhihirishia ubinafsi uliovuka kikomo.

Ina maana Lowassa angeingia Chadema na kuwa mwanachama tu bila kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho, na kama Dk. Slaa angeteuliwa kuwa mgombea urais kupitia Ukawa, je, angeachana na siasa? Je, angejiondoa Chadema na kuanza kunena ayanenayo?

Dk. Slaa anatakiwa kutambua ya kuwa wanaotaka mabadiliko ni mamilioni ya Watanzania walio ndani ya CCM na nje ya chama hicho tawala, hasa wale wanaoumizwa na umaskini wa kupindukia ambao chimbuko lake ni mfumo uliopo – mfumo wa wachache kujitajirisha huku mamilioni wakiwa mafukara. 

Mimi nadhani Dk. Slaa aliingia kwenye siasa kama ajira yake, lakini alipoingia Upinzani akasahau kuwa huko ni kujitoa (dedicate) zaidi ili kufikia lengo husika. Eti anasema kuwa kwenye familia yake wanaishi maisha ya shida ya kula mihogo na maharage! Huu ni utani mwingine usio na mashiko. Hivi familia zinazoishi kwa mihogo na maharage tu anazifahamu huyu?

Au ameamua kuwakejeli na kuwacheza shere Watanzania wanaoishi kwa mlo mmoja usio na uhakika? Mla mihogo anao uwezo wa kuitisha mkutano na waandishi wa habari uliojaa ulinzi? Mla mihogo anaweza kukodi ukumbi wa hoteli kubwa ya kitalii na kuoneshwa moja kwa moja kupitia runinga kwa muda wa saa moja na nusu?

Kama kula mihogo ndiko huku na mafanikio yake ndiyo haya, basi mimi na familia yangu tunaamua kula mihogo kuanzia leo ili tuweze kuyafikia mafanikio haya aliyoyafikia mla mihogo mwenzetu. Dk. Slaa ameamua kwa dhati kutudanganya walalahoi kuwa tatizo letu la umaskini chanzo chake ni mtu mmoja tu. 

 Haki ya Mungu, mamilioni ya Watanzania maskini mwaka huu yatawaumbua wale wote wenye nia mbaya na nchi yetu pendwa.    Watanzania wanahitaji mabadiliko ya mfumo uliowadumaza katika umaskini uliotopea, wana chuki kutokana na umaskini wao.

Mabadiliko hayo hayajali yanatokana na nani bali wanachohitaji ni mabadiliko ya kweli yatakayowatoa hapa walipo na kuwasogea mbele. Sasa wanahitaji viongozi watakaowaonesha dira ya mabadiliko yanayowapeleka kwenye maendeleo ya kweli.

Wanahitaji mabadiliko ya kutumia na kutumika kwa rasilimali za nchi yetu kunufaisha kila mmoja wetu na si kuishia kuwa matunda ya wachache.

Huu si muda mwafaka wa kuanza kurushiana makombora yasiyo na tija kwetu na Taifa letu kwa wakati huu, ambao tunataka kusikia viongozi wetu wanaotuomba kura watatufanyia nini miaka mitano ijayo.

Mimi si muumini wa kuundiana mazengwe, bali muumini wa ukweli na upendo ili upendo na nuru vitawale katika ardhi yetu hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

Ni vyema tukajitafakari na kuhakikisha hatutoi mwanya kwa wale wenye visasi na vinyongo kwa baadhi ya watu kama ilivyoanza kujiweka wazi. Tukumbuke kuwa visasi na chuki zilizofichwa katika mioyo ya watu zisitumike kutugawa na kusambaza vimelea hivyo vitakavyotutumbukiza katika janga la kubezana na kuchokonoana kusikokuwa na faida na nchi yetu.

Tanzania ni moja ya nchi zinazosifika kwa kuwa na amani, ni vyema amani hii tuliyonayo tukailinda na kuitunza hata kama mioyo yetu ina upungufu wa amani hiyo.

Natambua ya kuwa baadhi yetu uvumilivu umefika kikomo, lakini tusitumie chuki kueneza chuki pale pasipokuwa na chuki kwa faida binafsi. Tuwe waangalifu kwa kutokubali kutumiwa na wasiotutakia mema kisha kuchafua taswira yetu.

Tukifanya makosa, ndoto za mabadiliko zitatoweka na Tanzania itaendelea kujengwa na wenye moyo na kuliwa na wenye meno.

By Jamhuri