“Huyu ni mpiganaji kama sisi. Lakini bunduki yake ni tofauti na zetu. Bunduki yetu inaweza kuua askari mmoja kwa wakati mmoja, na mlio wake hausikiki hata Mueda. Lakini bunduki yake (kalamu) inaua maadui wa uhuru kwa mamilioni duniani kote na mlio wake utasikika katika historia daima.”

Hayo ni maneno ya Samora Machel akimtambulisha Mwandishi wa Habari, Jenerali Twaha Ulimwengu, kwa wapiganaji wa FRELIMO msituni Msumbiji mwaka 1972. Baadaye Samora Machel alikuwa Rais wa Msumbiji kuanzia mwaka 1975 hadi 1986 alipouawa katika ajali ya ndege huko nchini Afrika Kusini.

Nimenukuu maneno hayo kutaka kuonesha uzito na muhimu wa maneno hayo yaliyotolewa na mwanasiasa na mpigania uhuru na ukombozi wa Mwafrika. Pili, kutambua thamani ya mwandishi wa habari mbele ya jamii yoyote, na tatu, hekima na busara mwandishi wa habari anayotakiwa kuwa nayo anapotumia kalamu yake kuandika habari na kuelimisha jamii.

Leo imetimu miaka 43 tangu maneno hayo kutamkwa na kutambulishwa na Samora Machel huko msituni Msumbiji. Hadi sasa na hata kesho mantiki na ukweli wa kauli hiyo haijachuja na wala haitatoweka duniani. Sababu yake ni ukweli tu na ni maneno kuntu. Laiti wanasiasa na mashabiki wangeliona hilo wasingethubutu kuwalaghai waandishi wa habari.

Baadhi ya waandishi wanatuhumiwa kukubali kunyengwa na kuhadaiwa wakati wanapofanya kazi zao. Hili halina ubishi. Waandishi tunalaumiwa kwa kushindwa kufikisha habari zinazotakiwa na kukidhi mahitaji na matarajio ya jamii yetu.

Ni majuma sita sasa nazungumzia mahitaji ya Watanzania ya kutaka mabadiliko, mapinduzi au mageuzi katika maeneo ya mfumo wa maisha na uendeshaji wa uongozi na utawala, utoaji wa huduma za jamii, uchumi, haki na maadili ndani ya mwenendo wa jamii yetu.

Waandishi tunapopuuza au kukataa kutii wajibu na dhima yetu kwa Taifa letu, ni yumkini tunafanya mambo mawili hatari. La kwanza, kudhalilisha taaluma yetu na sisi wenyewe kujitoa thamani mbele ya jamii. La pili, tunajenga chuki, uhasama na kuandaa uvunjifu wa amani nchini. 

Ushabiki sisi unatuhusu nini wakati kazi yetu ni kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na zaidi kuchunguza, kuchambua na hata kukemea maovu yoyote na kusifu mema yoyoye kwa kiwango kilicho sahihi?

Samora Machel anamuona na kumpa hadhi mwandishi kuwa ni mpiganaji sawa na askari mpigania uhuru na ukombozi wa mtu huru, nchi huru. Mwandishi ni mtu anayejenga heshima yake na anayetafuta heshima na kulinda nchi yake na utu wake. Kalamu ya mwandishi inaua mamilioni ya watu kwa muda wote wakati bunduki inaua mtu mmoja kwa wakati mmoja.

Kalamu ya mwandishi isipoheshimu hoja na nguvu ya hoja kwa sababu tu ya kujali ushabiki, au kulenga tukio badala ya jambo jadidi, ni kuweka poni usalama wa Watanzania. Gharama ya kuukomboa utulivu na usalama kutoka poni ni kubwa mno na huchukua muda mrefu kupona majeraha yake.

Wakati huu tunapojiandaa kuchagua madiwani, wabunge na rais bora katika Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba, 25 mwaka huu, hatuna budi tuheshimu mawazo ya Watanzania, tuthamini uhuru na amani yao na tupime kauli za wagombea wetu kwa kuelekeza kalamu zetu katika zizi la usalama.

Kalamu inapokubali kuandika mahitaji ya dhana pumbaza, danganya, zushi na shawishi ni dhahiri shahiri inadharau mahitaji ya dhana ya ukweli, haki, upendo na tulivu. Je, kalamu haiheshimu ndevu, hata kidevu? 

Mwandishi Jenerali Ulimwengu, namnukuu akisema, “Uhuru wa kusema unakwenda pamoja na uhuru wa kuandika habari pasi na vizuizi visivyo vya lazima” mwisho wa kumnukuu (Gazeti Dimba Mei 19-25, 1994)

Kauli hiyo ukweli inatoa inthari kwa waandishi wa habari tuzingatie taaluma yetu na tujitahidi kuvishinda vishawishi vinavyoweza kuchafua na kuondoa thamani ya uhuru wetu wa habari. Tunapojaribu kukomaa katika kuharibu uhuru wetu wa habari, tunakaribisha hatari kwa Taifa letu.

Baadhi yetu waandishi hatupendi wala hatutaki kukubali, ukweli ni ukweli, haki ni usalama na ushabiki wa kisiasa ni janga kwa taifa lolote. Ni muhimu tukakumbuka na kuelewa hivyo ili tuweze kurudi kwenye kanuni zetu ya uandishi wa habari.

Kudharau nasaha kama hizo ni sawa kama vile kudharau ndevu zilizoota juu ya kidevu. Ndevu zinaponyolewa kidevu huwa kitupu. Je, kidevu hakistahiki kuheshimiwa? Usipoheshimu kidevu utaheshimu nini chini ya kidevu? Tafakari!

By Jamhuri