Niliwahi kuandika waraka mmoja hapa kwamba mataifa yaliyoendelea yamepitia misukosuko mingi ya kukamilisha maendeleo yao. Kuna makosa waliyopitia na wapo walioweza kupita njia sahihi kufikia malengo. Kuna usemi kwamba hata siafu au mchwa wanaofanya kazi kwa umoja na kushirikiana, kuna wengine hugeuka kuwa wasaliti kwa uvivu.

Taifa letu sasa hivi lina kaulimbiu ya maendeleo, si kwamba kaulimbiu hiyo ndiyo imeanza leo, ilianza tangu tulipopata uhuru wetu, kilichotuponza ni wachache kuamua kujilimbikizia mali na uvuvi wa kuwajibika katika jamii ambayo malengo yake ni kuhakikisha tunafika mbali, hiki ni kikwazo kama cha baadhi ya mchwa na siafu.

Yapo mengi yanayozungumzwa katika maendeleo, yapo maelezo ya miundombinu ya Taifa na uwezeshaji maendeleo, yapo ya ardhi yenye rutuba na nguvu kazi, yapo ya maliasili zote zilizo juu ya ardhi kwa maana ya wanyamapori na chini kwa maana ya madini.

Yapo ya ubora wa hali ya hewa na umiliki wa eneo kubwa la maji ya mito, maziwa na bahari kwa uvuvi na bandari, yapo ya kiunganishi cha nchi ambazo hazina bandari na biashara kwa ujumla. Haya ni maeneo ambayo kwa macho ya karibu bila kutumia kurunzi ndiyo ambayo kila mtu anayapigia kelele kama sehemu za kutajirisha Taifa hili.

Leo nimeamua kuandika waraka mwingine wa kizuzu kujaribu kuangalia ni jinsi gani jicho fupi linavyoona umaskini wa Taifa hili kwa kushindwa kuyatumia maeneo haya kama sehemu ya kuvuka umaskini tulionao kwa kipindi cha miaka hamsini iliyopita.

Ni ukweli kwamba siasa ni nguzo ya amani na maendeleo kwa Taifa lolote lile, ni ukweli kwamba demokrasia ina mchango mkubwa sana katika mataifa yote yaliyofikia kupata maendeleo, lakini si kwamba siasa ni sehemu ya maendeleo kiutendaji, siasa inatakiwa kusimamia sera za utendaji na siasa ina mipaka yake katika taifa lolote lile.

Kigezo cha maendeleo kwa Mtanzania wa kawaida huku kijijini, ni kuwa na fedha na nyumba ya bati, hiki ni kigezo cha hali ya chini sana bila kuzingatia idadi ya milo, huduma za jamii kama elimu, afya, maji na kadhalika. Kigezo cha maendeleo kwa kada ya juu ni umiliki wa mali zisizohamishika na zinazohamishika.

Katika Taifa letu ambalo watu wengi ni maskini, tunajikuta tukiimba wimbo wa umaskini bila kuchanganua mahitaji yetu ya msingi yanayotutenganisha na dhana iitwayo umaskini. Tunapata elimu, huduma za afya, maji, umeme na nyinginezo kwa asilimia ndogo. Lengo ni kupata huduma hizo kwa asilimia kubwa na watu wengi. 

Ili tuweze kutoka hapa tulipo, tunahitaji kujifunga mkanda zaidi na kukubali machungu yanayotokana na mazowea ya kujitwalia mapato na kupoteza muda bila kujali, tunahitaji kuwa wachumi kila mmoja kwa kiwango chake, tunahitaji kukataa umaskini kwa vitendo na si kwa maneno.

Mataifa yaliyopata maendeleo yalitumia nadhiri ya kujitoa kafara kwa nia ya kutoogopa mtu au watu, au kikundi fulani cha watu wachache wenye kudhihaki juhudi za wengine, walipitisha sheria zilizokata bila kuangalia sura ya mtu, walipitisha ondoleo la hofu kwa kila jambo na hatimaye wakajikuta wakiweza kuzikabili huduma za jamii kiurahisi.

Fikra za maendeleo ya siku moja kwa Taifa letu zitakuwa za kijinga kwa kuwa hatujajitoa kafara kuwa wazalendo kwa Taifa letu, tunawafuga wenzetu ambao ni mahasimu kwa suala la maendeleo, tunabebana na kulindana hata pale tunapojua kufanya hivyo ni kosa na kunatunyima kupata huduma za kimaendeleo.

Tumefungua uwanja wa siasa na kugeuza rasilimali ya kutegemea kutupa mabadiliko ya maendeleo, siasa ni maendeleo lakini haileti maendeleo, siasa safi, watu, viongozi na ardhi vinachangia sana katika maendeleo, hizi siasa za kutaka umaarufu na kuleta vurugu zinaweza kuleta umaskini zaidi.

Kwa ujinga wangu nachelea kusema iwapo hatutaamua kwa dhati ya mioyo yetu, basi hata tuishi kwa uhuru wa miaka elfu moja tutakuwa na undugu na umaskini. Ni lazima tufike mahali tuseme inatosha na sasa tunataka kubadilika tuwe na maendeleo.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri