Kwanza, nikiri wazi kwamba sizungumzii Tv Online zote, la hasha! Zipo ambazo unatamani kuzifuatilia kwa jambo lolote makini na zipo ambazo zinajibainisha kuwa ni za watu makini, lakini huo ujinga ambao unaupata kila unapojiunga nao, kwa kweli ninashauri tuangalie upya jinsi ambavyo wamepata vibali vya kurusha hayo matangazo yao.

Leo nina miaka dahari kidogo, kwa ufupi mimi ni mtu mzima ambaye kwa sasa sipendi kudanganywa kabisa, huwa ninahisi kupandwa presha kila ninapodanganywa dhahiri na hao wanaojiita watangazaji katika hizo Tv Online ambazo sina hakika kama zina ithibati kutoka katika mamlaka zinazohusika. 

Ni kwa muda mrefu sasa Watanzania wana kiu kubwa ya kupata habari mbalimbali, ziwe za siasa, michezo, elimu, matukio na hata habari za maisha ya kawaida. Ni kipindi ambacho wananchi wa Tanzania wamegundua kuwa wanaweza kupata elimu na burudani kupitia vyombo vya habari ambavyo kimsingi vimepewa dhamana ya kufanya hivyo.

Leo naandika waraka huu nikikumbuka jinsi ambavyo vyombo vingi vya habari yakiwemo magazeti na redio vilipokuwa vikipinga baadhi ya sheria za habari wakati zikipitishwa, nilikuwa miongoni mwao katika hili na niliamini ni kutunyima uhuru wa kutoa habari kwa wananchi kwa wakati huo, na bado unaweza kuwa msimamo wangu iwapo tu baadhi ya vyombo vitafanyiwa usaili na kurekebishwa namna ya utoaji wa habari zake.

Najua wapo watakaonichukia kwa kusema ukweli kwamba eneo hili baadhi yetu wamelivamia na kulitumia kwa staili ambayo ni ya kiuendawazimu, hasa katika kuwasilisha habari yoyote kwenye jamii yenye uchu wa kupata habari. Wapo wanaotudharau kwa sababu ya wachache na wapo wanaotulinganisha na wenzetu wanahabari.

Siku za hivi karibuni kumeibuka utitiri wa vyombo vya habari, vipo ambavyo vimejikita kwa maeneo maalumu kama ya michezo, hivyo vinaelewa wajibu wao na jinsi ambavyo wanautendea haki uwanja huo.

Vipo ambavyo vimekuwa vinatoa habari muhimu za matukio ya kufunza na yaliyovuma, havikosei sana, na vipo vyombo ambavyo vinawatumia Watanzania wa kawaida kwa akili zao kama vyanzo vya habari, hivi vinakera sana, hasa kama habari yenyewe ni nyeti na inahitaji uthibitisho kutoka kwa mtu mwenye mamlaka.

Leo nimeamua kujivua nguo za uanataaluma kwa aibu ya baadhi ya hao wanaoitwa wanahabari, wanahabari ambao hawajui ipi ni habari na ipi wailete kwenye jamii yetu, wanahabari ambao wanadhani kuweka habari za watu fulani hata kama ni za aibu wanaitendea haki taaluma ya habari, nadhani labda lengo lao huwa ni kuielimisha jamii hata katika mambo ya kijinga. 

Ninakerwa sana na hizi Tv Online ambazo zinajipambanua na vichwa vyao vya habari kwamba suluhisho limepatikana kutokana na habari yao, lakini ukisikiliza ni ‘utumbo wa kuku’. Katika hili nadhani Kamati ya Maudhui inapaswa kujitafakari kuendelea kuviachia vyombo hivi kujinasibu kama vingine. 

Kumekuwa na kugombania kutoa habari mpya mapema lakini hakuna uthibitisho wowote na wala mwisho wa taarifa zao, wengi huokota ushahidi wa kwenye mitandao ya kijamii, tena ambazo zimeandikwa na watu wajinga katika jamii yetu.

Vyombo hivi vimekuwa vikitumia neno ‘breaking news’ kwa jambo ambalo ni ‘serious’ na kisha kuweka utumbo wao ambao unawakera wasikilizaji, lakini pia unawadhulumu amana ya vifurushi watu wenye uchu wa kujua jambo ambalo limeitwa ‘la sasa hivi’.

Ni jambo la kukerehesha sana unapomsikiliza mtangazaji anayeshindwa hata kusoma meseji za watu walizoandika mitandaoni, na pengine hata kuitengeneza habari yenyewe anashindwa. Najiuliza, katika kipindi hiki cha ushindani wa kibiashara tunaweza tukaingia kwa kasi hii ambayo inawakera wasikilizaji?

Wito wangu, nadhani umefika wakati wa kukataa kuwa walaji wa mambo ya kijinga, ufike wakati wenye dhamana waseme inatosha, ifike mahali wenye kukashifiwa wawapeleke mahakamani, ufike wakati wanahabari tuseme inatosha kuwa na watu wanaotutia aibu katika tasnia yetu.

Ifike mahali tushikane mikono kuwasema wenzetu ambao ni ‘makanjanja’ na wanatufanya wote tudhalilike, wote tukatae kuwekwa katika kapu moja linaloitwa la wana habari, tasnia ambayo tulidhani ungeweza kuwa mhimili kamili.  

 

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri