Inaweza kuwa nyaraka muhimu kama hati ya nyumba, mkataba wa mauziano au mkataba mwingine wowote, wosia, kadi ya gari au ya mashine yoyote, hati ya kusimamia mirathi, cheti cha ndoa au vyeti vinginevyo na nyaraka nyingine mbalimbali.

Nyaraka hii inaweza kuwa inatakiwa sehemu muhimu kama mahakamani ili kuthibitisha shauri au kesi yako. Na inaweza ikawa ni nyaraka ambayo kuwepo kwake ndiko kushinda kwako na kutokuwepo kwake ndiko kushindwa kwako.

Pamoja na umuhimu wa nyaraka hii, bado umeitafuta kote pa kutafuta na haukuweza kuipata. Au haukuitafuta madhali tu unajua ilishapotea au iko mikononi mwa mtu ambaye hujui alipo na hawezi kupatikana. Katika mazingira ya namna hiyo makala hii itaeleza vitu vichache vinavyoweza kukusaidia kutoka Sura ya Sita, Sheria ya Ushahidi.

1.  Ushahidi wako

Kitu kikubwa kinachomsaidia mtu kushinda kesi mahakamani ni ushahidi. Kadhalika kushindwa kwako pia ni ushahidi. Ukisema hiki kiwanja au nyumba ni yangu, unatakiwa kuonyesha hati au mkataba wa mauziano au vyote viwili.

Ukisema hili gari ni langu, kadhalika unatakiwa uonyeshe kadi yenye jina lako ama vinginevyo. Ukisema nilikuwa na ndoa halali, unatakiwa uonyeshe cheti cha ndoa ama vinginevyo. Ukisema nilimuuzia au kununua kitu fulani, unatakiwa uonyeshe mkataba ama risiti, vivyo hivyo nk.

Hakimu au jaji si mtu ambaye anakuwa eneo la tukio, hivyo kuwa katika nafasi ya kujua nini kilitokea huko. Yeye hajui chochote kilichotokea, hivyo taarifa zote anazipata kwenu mnaoshtakiana.

Kwa msingi huo, yupo katika wakati mgumu kuamua nani yuko sahihi na nani hayuko sahihi kwa kitu ambacho hakushuhudia na hakijui.

Kama hivi ndivyo, kitu pekee cha kumuongoza hakimu/jaji huyu ambaye hakuwepo wakati mnadhulumiana, ni ushahidi wa kila mmoja atakaowasilisha. Hataangalia sura ya mtu, kulia machozi kwa mtu, kuongea kwa kujiamini au kwa unyonge kwa mtu, umri wa mtu, rangi ya mtu, wala jinsia, bali ushahidi uliowasilishwa na mtu.

2. Mambo mawili yanayoweza kukusaidia ikiwa umepoteza nyaraka

Jambo la kwanza: Lipo Kifungu cha 65 (a), (b) na (c) cha Sheria ya Ushahidi. Ni uwepo wa nakala (kopi) ya nyaraka halisi (orijino), kama umepoteza orijino lakini ipo kopi au unajua sehemu ambayo unaweza kupata kopi, basi inaweza kukusaidia.

Ndiyo maana ni muhimu kuwa na kopi ya kila nyaraka ambayo una orijino yake. Kifungu cha 63 cha Sheria ya Ushahidi kinasema kuwa nakala isiyo halisi/kopi inaweza kutumika kuthibitisha jambo. Lakini pia vitu vingine vinaweza kuhitajika kuthibitisha kupotelewa nakala halisi, kwa mfano taarifa ya Polisi ya kupotelewa nk.

Jambo la pili: Lipo Kifungu cha 65 (e) cha Sheria hiyohiyo ya Ushahidi. Ni kumleta shahidi ambaye anakumbuka na kujua kile kilichokuwa kimo/kimeandikwa katika nyaraka hiyo ambayo haionekani.

Anaweza kuwa mtu aliyeiandaa, aliyeishuhudia, aliyeisoma au yeyote ambaye kwa uhakika alijua nini kilichokuwa kimeandikwa ndani mwake. Kazi yake itakuwa ni kueleza nini kilikuwa kimo/kimeandikwa humo na atahojiwa na kuulizwa kuhusu hicho alichosema.

Hili nalo laweza kusaidia.  Kama hivi vyote havipo, kuthibitisha kwaweza kuwa vigumu, hivyo kujikuta unapoteza hata kama haki ni yako.

Please follow and like us:
Pin Share