Leo tuna siku ya tatu baada ya Mwaka Mpya kuanza. Wapo ambao labda walikuwa na mipango mbalimbali waliyopanga wangefanya mwaka huu lakini isivyo bahati hawakuweza kufika kwa mapenzi yake Mola – mwenye kutoa rehema zake ndogo na kubwa.

Leo ni mwaka mwingine, mwaka umepinduka, wapo walio na afya njema wakifurahi kwa kunywa mivinyo na wapo walio na afya mbaya wakigugudia dawa chungu na viambato vyake, wakati wapo wanaoishi kwa furaha pia wapo wanaoishi kwa mashine hospitalini.

Leo ni siku ya mwaka mwingine, wapo wanaohesabia mafanikio na wapo wanaozidi kuingia katika lindi la kushindwa kufanikiwa kutokana na amana zao kutokuwa timilifu kuyakabili maisha, wapo wanaokula na kusaza na wapo wanaotafuna kitu cha kuziba utumbo ili siku ipite.

Leo ni Mwaka Mpya, nyumba nyingi zina furaha, familia nyingi za mama, baba na watoto zinakumbatiana kwa kumaliza mwaka kwa mafanikio  na upendo, lakini pia kuna familia ambazo zimeparaganyika, watoto hawajui wazazi wako wapi, wazazi hawajui watoto wako wapi, kuna nyumba hazina sherehe, kuna yatima wasiojua kuwa mwaka umepinduka.

Maisha ya mwaka jana si ya mwaka huu, mwaka mpya unaoakisi mambo mapya, yanaweza kuwa yenye heri lakini pia yanaweza kuwa yenye shari. Mwaka unaoingia na kaulimbiu katika kila familia, ni mwaka mpya uliokuja bila rangi mpya, kwa ufupi ni mabadiliko ya tarakimu tu lakini maisha ni yaleyale.

Ni mwaka mpya ambao unakuja na changamoto ambazo hazikukamilika mwaka uliopita, kuna changamoto za maendeleo, mambo ya kijamii, mambo ya siasa, mambo ya uchumi na kadhalika. Nahisi ni changamoto ambazo tutamaliza nazo mwaka, hii ni njozi yangu kutokana na uzoefu wa kushangilia mwaka mpya kwa miaka mingi.

Leo sioti ndoto ila naona mambo kwa uhalisia zaidi, nawaona wananchi wakiwa katika wakati mgumu wa kiuchumi kwa mwezi wa kwanza, nayaona madeni yanavyoongezeka miongoni mwa watu, nawaona wakulima wakipunguza akiba ya chakula chao kwa kuuza ili kukabiliana na ugumu wa maisha.

Nawaona wafanyakazi, ni wachache sana lakini sura zao zimenyongea kwa kukosa akiba ya fedha, wanaishi kwa mshahara ambao haukidhi hata haja ya siku tano kwa mwezi, wanajipa matumaini ya kuwa na mshahara utakaojitosheleza baada ya fumuafumua ya wafanyakazi hewa na kuziba mianya ya rushwa.

Nawaona wafanyabiashara wakubwa macho kodo TRA, si kwa sababu hawalipi kodi, la hasha, ila kwa sababu hawana cha kulipa kutokana na kukosa kuuza bidhaa zao kipindi cha neema, nawaangalia wamachinga wakiwa na furaha ya kupata ruhusa ya kuuza bila kutumia EFD lakini pia bila kulipa kodi wakiwa macho kodo kwa wateja, wateja ni watazamaji si wanunuaji.

Naangalia ofisi nyingi zikifungwa kutokana na dili kukatizwa, naangalia ajira nyingi ambazo hazikuwa rasmi lakini zenye mishahara mikubwa zikiisha kwa waajiriwa, maisha yanazidi kuwa magumu, dili zimefika ukingoni na watu wako wengi wakiwategemea wapiga dili.

Nawaangalia watu – vijana kwa wazee – wakiingiza bahati ya kuwa wakwapuzi ili kujinusuru na maisha ya kutotoka jasho halali, nawaona vibaka wazoefu wakipokea kundi kubwa la ajira mpya, nayaona matangazo ya kuibwa mali yakiwa yanaongezeka kila uchao.

Huu ndiyo Mwaka Mpya mwingine ambao hauna tofauti na ule uliopita na ulikuja kama huu na mambo yakaendelea mpaka leo, hauna nafuu na huu hautakuwa na nafuu tena, kila mwaka itabaki historia kuwa nafuu ya mwaka jana, nafuu itaendelea mpaka utakapokoma kuuona mwaka mpya.

Hongera kwa Mwaka Mpya lakini utamu wa Mwaka Mpya ni kuwajibika kwa kufanya kazi, kazi ni kipimo cha utu na utegemezi ni kipimo cha ujinga. Nadhani mnashuhudia jinsi ambavyo waliokuwa ‘kula kulala’ wanavyohangaika mwaka mpya na kumtafuta mchawi.

 

Wasaalamu, 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1046 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!