Mzee Ben akapewa rungu la kutetea uhai wa chama katika uchaguzi huo na akaibuka kidedea, lakini nguvu ya soko la dunia katika bidhaa ikaanza kupungua kutokana na mizizi yake kukomaa ikawa siyo habari tena ya kuwaelekeza Watanzania ambao awali walijifanya wanalipokea kwa shingo upande, wakoloni waliona mianya ya kutawala vitaifa vidogo kwa kisingizio cha uwekezaji.

Wanangu hatukuwa na njia nyingine, katikati ya bahari umuokoe nani hakuna ikawa kila mtu afe ki vyake, wenye mitaji wakaja na waliokuwa na mitaji wakajitokeza, walichukua mali za Tanzania kwa hoja hiyo ya uwekezaji na serikali kujitoa katika biashara bali ikusanye kodi, tuliweza kwa kiasi fulani lakini utundu wa sheria ulianza kuonekana baada ya miaka michache ya uwekezaji.


Baadhi ya maeneo tulibugi kweli na mengine tuliweza kujinasua lakini ndio kwanza Watanzania tuko katika mchakato wa kujifunza mambo ya uwekezaji, tukajua ni mambo ya mpito na tutakuja kujikomboa, wapo waliolalamika sana na wapo waliothubutu kumlaani Mzee Ben wakiamini anatumia mabavu kuwapa wakoloni mali za Watanzania, hili sina hakika nalo lakini najua kuwa huo ndio upepo uliokuja baada ya yeye na chama chake kupewa nafasi ya kuongoza taifa hili na kuwashinda walioitwa wapinzani ambao walidai wao wangeweza kukabiliana na hoja ya uwekezaji.


Mzee Ben akampa ushindi Rais Jakaya ambaye ndio yuko katika ungwe yake ya mwisho ya utawala na ambaye alihakikisha chama kilekile ambacho Julius alikiasisi hakishindwi katika uchaguzi wa vyama vingi pamoja na makeke yake ya mvutano wa kisiasa, hapa ndipo palipoibuka wanasiasa nguli wanaojua kujenga hoja hata kama si ya msingi lakini ina ushawishi kwa wananchi wapiga kura.


Mengi yametokea na tunayaona kwa kuwa tuko nayo, kaulimbiu aliyopewa na chama chake aingie nayo katika kinyang’anyiro cha kuomba kura, maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana ilikuwa na mvuto usio na kifani, Mzee Zuzu niliyegoma kupiga kura tangu enzi za ndiyo na hapana safari hiyo niliingia katika chumba cha kupiga kura na kumwaga wino wangu kuyataka maisha bora zaidi.


Wanangu mtazamo wetu ni tofauti na ambacho tulikuwa tukisubili kwa kipindi kifupi, tulihisi kunywa maziwa bure, kutibiwa bure, kusoma bure, mishahara ya wafanyakazi minono, ajira za kumwaga, usalama wa kutosha wa raia, hospitali na zahanati kila mtaa, umeme na maji salama hadi Kipatimo, mafuta ya mitambo mbalimbali na chakula vije kwa bei ya chini, lakini hatimaye mambo yamekuwa kinyume kabisa, sina hakika kama amegeukwa kama Mwalimu Mwinyi.


Sasa wanangu tunaelekea uchaguzi mwingine wa vyama vingi, mimi sina chama lakini nina sera ambazo zinaweza kuniuza na nikapata fursa ya kuongoza nchi hii bila kujali sana masuala ya siasa, nitaangalia awamu zote wapi wamebugi na wapi tumeweza kuthubutu na tukafika hapa tulipo, naweza kwa sababu sina chama na sina mtu ambaye atasema mimi ni rais kwa sababu nimesaidiwa na chama changu.


Nitaangalia yanayowasibu Watanzania badala ya kuangalia nguvu ya wakoloni na ujanjaujanja wao, nitajiuliza Watanzania hawa wanataka maji salama ama wanataka ving’amuzi? Nitajiuliza Watanzania hawa wanataka amani ama askari wengi wa kutuliza ghasia.


Nitaangalia Watanzania wanataka suti na mikate kutoka nje ama  mbolea? Nitaangalia wanataka umeme ama vibatari vya kutosha? Wanataka michezo ama elimu, wanataka siasa ama utekelezaji?


Wanangu baada ya tathimini ya mazuri yote katika awamu nitakuja kwenu kuomba kura ya ndiyo si ya mtu wala chama halafu mnipime kwa kipindi kifupi muone ninatosha ama sitoshi kuwa rais wenu? Mkiona ninatosha mnaweza kuamua niongoze kwa miaka mingapi ndipo ning’atuke na kuwaachia, ama balaa, au mnachotaka.

Wasaalamu,

Mzee Zuzu – naomba kura zenu,

Kipatimo.


1154 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!