Najua ili uweze kuwa rais wa nchi hii, katiba inakutaka uchaguliwe na chama chako kwa kura zinazotosha na upitishwe kwa vigegele na mkutano mkuu wa chama  kwamba wewe unafaa kuwa kiongozi baada ya wenzako kuthibitisha kuwa hutawaangusha, lakini pia wenzako haohao ndio wanaokutayarishia kaulimbiu ya kuingia nayo katika ushindani uweze kuwashinda wapinzani wako.

Nawapongeza wote ambao katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru wameweza kuchaguliwa na wanachama wao na kuweza kushika mpini wa chama kuingia katika kinyang’anyiro cha kuomba kura na kwa ridhaa ya wananchi wakapata fursa  hiyo na kuifanyia kazi, kwa ufupi kura zao zilitosha kikamilifu.


Namkumbuka Julius kwa kauli mbalimbali ya kwanza kabisa ni uhuru ni kazi, siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo iligubikwa kwa nguvu na Azimio la Arusha ambalo liliibuliwa katika kati ya kaulimbiu hii, vijiji vya ujamaa kwa maana ya kusogeza huduma za msingi kwa jamii, pamoja na matatizo yake ya bomoabomoa ya sogeza na kuacha mahame tofauti na bomoabomoa ya leo ya ujenzi wa barabara kutokana na kiburi cha Watanzania kutotaka kufuata sheria za mipaka ya barabara.


Nakumbuka siasa ni kilimo na kilimo cha kufa na kupona, nakumbuka ushirika wa vijiji na manufaa ya kuwa na mali zetu wote, kuzimiliki kwa hisa za nguvu na siyo hisa za fedha kama mambo yalivyo leo.


Nakumbuka siasa ya kuzalisha na kutumia raslimali tuliyonayo na hapa ndipo tulipoanza kujenga viwanda vyetu vingi vya kuzalisha bidhaa badala ya kuuza malighafi nje ya nchi.


Wanangu haya yote yalikuja kupotea baada ya vita ya Uganda na kutufanya tufilisike kabisa lakini kwa kuwa Julius alikuwa madarakani bado tulipitisha azimio la kufunga mikanda kukabiliana na matatizo tuliyokuwa nayo, tulifunga mikanda kwa miezi kumi na minane ambayo baadaye iligeuka kuwa miaka ili tuweze kurudi tulipokuwa kiuchumi.


Wanangu upepo wa madaraka kwa mtu mmoja kwa kipindi kisichojulikana ukapeperusha nguvu za Julius Kambarage Nyerere na kutufanya tuingie katika ulimwengu mwingine wa soko huria na ndipo Mheshimiwa Mwalimu Mwinyi alipopewa bendera ya chama chake aweze kukabiliana na changamoto mpya ambazo wazawa ambao tulikuwa tumekunywa maji ya bendera ya TANU tukaona kama tumepotea njia kwa mwalimu aliyekubali soko huria kutokana na shinikizo kutoka kwa wanaoitwa wafadhili wa Tanzania, hapa msemo wa ruksa ulishika kasi na kuamini hakuna kosa lolote ambalo mtu anahesabiwa kwa kuwa kila kitu ni ruksa.


Nyuma ya mgongo wa Mwalimu Mwinyi, viongozi ambao hawakuwa waaminifu waligeuza uchumi wa Tanzania kuwa kichekesho, mfumuko wa bei ukaibuka wafanyabiashara wakawa wanatembea na hela katika soksi, rushwa ikawa njenje, kilimo kikafa kwa kuwa kila mtu aliamini kufanikiwa katika biashara.


Sera za Julius za siasa ni kilimo na kilimo cha kufa na kupona zikawa zimeota mbawa, kundi kubwa la waliofanikiwa Tanzania likatokea.


Wanangu dunia tambara bovu haliishi viraka, ukaja mfumo wa vyama vingi uchaguzi wa ndiyo na hapana, uchaguzi wa jembe na nyundo ukafa ukawa uchaguzi wa mtu na mtu, kikaongezwa kipengere maalumu katika katiba cha vyama vingi vya siasa Tanzania.

 

Itaendelea

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu – naomba kura zenu,

Kipatimo.


Simu: 0759 784583

5105 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!