Tanzania ni moja kati ya nchi maskini sana duniani kutokana na kutotumia vizuri rasilimali zake na kuziendeleza.

Lakini, pia ni nchi mojawapo ambayo utawala wa kujipendelea kisiasa katika kujilimbikizia mali umekithiri, hali ya kimaisha ya wanasiasa ni tofauti kabisa na wafanyakazi kwa maana ya wanataaluma na wakulima kwa maana ya wazalishaji mali ni kubwa.

Awamu ya tano imeanza kazi kwa kujaribu kuweka usawa wa vipato baina ya wafanyakazi na wakulima kwa kuondoa posho nyingi na marupurupu yaliyokuwa yametengenezwa na vigogo wachache kujilipa pasi kuona haya kama kuna huduma mbalimbali zinakosekana katika jamii, hili limewezekana tena kwa kauli ya siku moja na mara moja, waliofanya tofauti na maagizo ya mkuu wametumbuliwa.

Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kusimamia matumizi ya fedha za Serikali, wapo bado ambao wanajiona ni manunda wanaoweza kutumia pato la Taifa kujinufaisha wao na familia zao, lakini mkono mrefu wa Serikali utaendelea kuwabaini wachache na kuwatumbua kila siku, ni jambo endelevu na linalohitaji ushirikiano wa hali na mali kuweza kuwasaidia watumbuaji.

Hivi sasa wanasiasa makini wanakutana Dodoma kujadili kile ambacho walikuwa wakikinadi katika mikutano yao ya kampeni kwamba ‘nichagueni nikawaletee maendeleo katika jimbo letu’. Wapo wanasiasa ambao wana dhamira ya kweli na jambo hili na wapo ambao ni madalali wa kisiasa na wapo kimaslahi, sisi wapigakura tutawajua katika mkutano wao.

Leo nimeanza na kikao cha Bunge tukufu ambalo watu wengi wanajua kuwa wao ni baadhi ya watu wachache wanaolipwa mishahara na posho nzuri tofauti na kundi kubwa la wafanyakazi na wakulima, hili ni kundi ambalo linafaidi malipo mazuri katika nchi maskini kuliko kundi jingine lolote lile, ni kundi linalojiita la wakereketwa wa maendeleo ya nchi yetu, ni kundi linalojidai linataka kuleta maendeleo ya kweli Tanzania.

Kundi hili la wanasiasa nalipenda kwa sababu nahisi litakwenda na kaulimbiu ya kiongozi mkuu wa nchi ya ‘hapa kazi tu’. Wengi wao walinadi na kuimba wimbo huo wa Magufuli wakituaminisha ni wimbo wanaoupenda na wapo pamoja naye, na tutathibitisha katika hoja zao za kukataa posho kubwa ambazo wenzao katika Bunge lililopita walikuwa wakipokea isipokuwa mbunge mmoja tu wa Kigoma.

Nimejifunza mengi ambayo nilikuwa najua hayawezekani katika maisha, mojawapo ni kuzuia sherehe za Uhuru na matokeo yake nayaona katika barabara mojawapo hapo Dar es Salaam, nimeona safari chache zisizo na tija kwa Taifa zikifutwa na fedha kupelekwa katika sekta chache muhimu na kubadilisha maisha ya watu. Tumeona katika elimu, hospitali, dawa, na miundombinu.

Tumeona jitihada za kukusanya mapato ya nchi kupitia kodi na jinsi tunavyovuka malengo ya kila mwezi, inadhihirisha kama tukiendelea hivi tunaweza kufanya mambo yetu bila kutegemea bakuli kwa wahisani ambao mara kadhaa wametuyumbisha kisiasa na kiuchumi kwa faida yao, sasa tunathubutu na tunaweza kutembea kifua mbele kwamba sisi tunajitegemea kwa kiasi fulani.

Ni Serikali hii hii ya wanasiasa wanaokutana Dodoma ndiyo itakayothibitisha kuwa wao ni pamoja na kiongozi wao mkuu katika kutuletea maendeleo, iwapo watasema inatosha kupokea fedha ambazo hazipaswi kulipwa kwao badala yake zikawekezwe sehemu muhimu kwa ustawi wa jamii.

Sina hofu kuwa wapo wanasiasa wachache ambao lengo lao halikuwa siasa bali mapato na kutumia fursa ya siasa kuweza kujinufaisha kupitia miradi mbalimbali kutokana na kujulikana kwao, hili ni funzo tuliloliona katika mabunge kadhaa ya huko nyuma ambako mwanasiasa anageuka na kuwa mfanyabiashara mkubwa katika kipindi kifupi.

Natarajia kuona Bunge la Magufuli kimsimamo, Bunge la kuondoa kero za wananchi, Bunge la kazi na kuwajibika, Bunge la kuongeza mapato na siyo kutumia mapato, Bunge la kujitolea, Bunge la kusimamia ipasavyo kazi za Serikali, Bunge la kumsaidia kiongozi mkuu na siyo kumkatisha tamaa jitihada alizoanza.

Najua pia wapo wapinzani katika Bunge, na sidhani kama upinzani ni kupinga ukweli bali kuonesha ukweli ulipofichika, naamini kiongozi wetu yupo kwa ajili ya majipu, hana nasaba na wabadhirifu, wezi na mafisadi, mkimsaidia hilo mtakuwa mmefanya kazi yenu vizuri.

Lakini pia tukumbuke tulikotoka na matatizo yanayotukabili majimboni mwetu wakati mkijadili posho na marupurupu mengine, tunataka kuona siasa ya wito siyo siasa ya mapato. Mungu akawatangulie kuona umaskini wa Taifa letu wakati wa kikao chenu cha Bunge na majipu yaliyokomaa ya posho za vikao. Anzeni kutumbua nyinyi tutawabariki na kuwaombea.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri