Mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alisimama katika majukwaa ya kuongea na wananchi juu ya kiongozi safi na anayefaa kuiongoza nchi yetu katika awamu ya tatu, alisimama akaongea mengi sana ambayo mengine hadi leo hayajafanyiwa kazi na awamu zote zilizokuwapo na kupita.

Hazijafanyiwa kazi kwa sababu kubwa nyingi, lakini kubwa ni kwamba kuna wakati tuliyumba kama Taifa na kuingiza maradhi ambayo ni ngumu kupata tiba, na pengine tiba yake ilitakiwa iwe ya taratibu kwa uangalifu mkubwa.

Kuna baadhi ya mambo ambayo hayajafanyiwa kazi kutokana na vipaumbele ambavyo Serikali imejipangia, hilo halina mjadala kwa kuwa sera ni chaguo la chama na viongozi wa chama ambacho kipo madarakani, kwa ufupi kupanga ni kuchagua na kuchagua ni matokeo.

Sasa Taifa linaingia katika mchakato wa kupata uongozi wa awamu ya tano. Kihistoria ni jambo la kujivunia sana, kila awamu imefanya jambo ambalo kamwe haliwezi kusahaulika katika historia ya nchi hii, na kuongoza nchi ni suala gumu si kama kuongoza familia kama wengi wanavyofikiria.

Awamu inayoondoka, ambayo inamalizia muda wake ina mambo ambayo ukiwauliza wananchi wanaweza kusema iendelee, iendelee kwa kuwa imefanya kazi kubwa sana katika kuwaunganisha wananchi kwa kupitia miundombinu. Sehemu ambazo zilikuwa hazifikiki, sasa zinafikika vizuri na kwa raha. Awamu hii inasifika sana kwa kujenga barabara na madaraja makubwa. Hongera.

Sasa tunaingia awamu nyingine, Watanzania wengi wana mtazamo tofauti wa mwenendo wa utawala, utawala mpya unaotarajiwa kuwapo, swali ni utawala upi utaongozwa na nani kwa manufaa ya akina nani.

Tanzania tunahitaji kiongozi mkali kwa sasa, kiongozi anayeweza kuchukua na kuamua mambo magumu kwa wakati mmoja bila kuhitaji mjadala wa wanasiasa – kiongozi mwenye uwezo kutoa uamuzi mgumu. Bado naamini kiongozi anaweza kutoka katika chama chenye umoja na mshikamano na mizizi iliyotapakaa nchi nzima.

Tanzania tunahitaji kiongozi mkuu wa nchi ambaye hatajua suala la upendeleo wa chama chake. Utamaduni huu unatakiwa kuendelezwa. Kiongozi atakayejua kuwa vyama vingine vya siasa ni vyama vya kutoa changamoto na kuikumbusha Serikali wajibu wake; atakayekubali changamoto kutoka kwa wanasiasa wengine kama sehemu ya kuimarisha utawala wake.

Tunahitaji kiongozi atakayeweza kuchukua hatua madhubuti za papo kwa hapo bila kumuonea haya mtu yeyote kwa kujulikana kwake; atakayekubali kuwajibika kwa jamii anayoiongoza pasi na kujihudumia yeye mwenyewe; tajiri wa roho ya utoaji na si maskini kwa utoaji.

Tunahitaji kiongozi asiyeongozwa, tunahitaji kiongozi mwenye uwezo wote, tunahitaji kiongozi mwenye uzoefu na nyadhifa za juu, hatuhitaji mtu ajifunzie utawala Ikulu; tunahitaji mtu anayeweza kuona mbele kwa macho yake na siyo macho ya wengine; anayejua hali halisi ya wananchi anaowaongoza na siyo kwa kusimuliwa, tunahitaji kiongozi anayetaka kuongoza na siyo kujitajirisha.

Tunahitaji rais atakayesema kuvunja Muungano ni mwiko na suala la Muungano siyo la kujadili bila hoja za msingi, tunahitaji rais ambaye anajua kuwa Ikulu ni mzigo lakini anaweza kuubeba, tunahitaji rais ambaye hajashindwa kitu katika uongozi wake aliopitia.

Tanzania tuna changamoto nyingi ambazo tunatakiwa tuzikabili, hivyo tunahitaji kiongozi atakayekuwa mstari wa mbele kuzikabili. Tuna tatizo kubwa la rushwa, linatakiwa kwisha kivitendo, tuna tatizo la elimu linatakiwa kutatuliwa kwa vitendo na siyo siasa, tuna tatizo la ajira linatakiwa litatuliwe kwa vitendo na siyo siasa za jukwaani.

Tanzania ninayoijua mimi tunataka kiongozi anayeweza kurudisha uzalendo wa kweli, uzalendo wa mtu kuipenda nchi yake, tunahitaji kiongozi ambaye mafisadi wa kweli wanaweza kumwogopa, tunahitaji kiongozi ambaye anaweza akathubutu kwa kiwango cha juu.

Tanzania hatuhitaji kiongozi wa kuingia Ikulu kwa majungu ya kuwachafua wengine, hatuhitaji kiongozi wa majigambo ya kuweza na hali amethibitisha hawezi, tunahitaji kiongozi wa nchi na siyo dini kabila au kundi fulani.

Hatuhitaji kiongozi wa kupigiwa debe na wasioweza, hatuhitaji wanaolazimisha kujulikana, hatuhitaji kiongozi wa mbwembwe, tunahitaji kiongozi anayekubalika na wengi, tunahitaji kiongozi wa kukemea kwa vitendo, tunahitaji kiongozi wa kuondoa nyufa zote na matatizo yote ya nchi hii.

Naomba maoni yenu kwa njia ya sms na siyo kupiga. Watanzania mseme mnataka kiongozi gani. Barua hii itaendelea kumtafuta kiongozi wa awamu ya tano.

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri