Salamu zangu nazielekeza kwa wasomaji wote wa waraka huu kila wiki. Najua kuwa mnaishi kwa matumaini sana, hasa katika kipindi hiki kigumu cha mpito, lakini kipindi hiki cha mpito ni kirefu kuliko wengi walivyotarajia. Najua dhamira ni nzuri na matokeo ni mazuri, lakini muda uliopangwa kuyasawazisha mambo haya haukutarajiwa uwe mrefu kiasi hicho, muwe wavumilivu, na siku zote wavumilivu hula mbivu.

Mheshimiwa Rais, naona kama nakuonea kila siku kukuandikia waraka kwa watu wako, niwie radhi kwa kuwa nafasi uliyoko ni nafasi ambayo hakuna namna ambayo huwezi kuguswa kwa sasa hivi, kwa mujibu wa madaraka uliyonayo kila jambo linaloendelea katika nchi yetu linakuhusu, uwe umaskini wetu au utajiri wetu, iwe amani yetu au vurugu yetu, iwe furaha yetu au huzuni – yote pamoja na mengine yanakuhusu moja kwa moja.

Hivyo naomba uwe mvumilivu katika kipindi chote cha utawala wako, kwa kuwa unatuongoza watu wenye tabia tofauti na akili tofauti, ukubali kuwa mtu wa lawama siku zote na waogope wanafiki wanaokudanganya, pia kaa mbali na watu ambao kazi yao ni kukusifia kwa kila jambo na mwisho tuambie jibu zuri ambalo ukiulizwa na mtu yeyote sema muda ndio  utajibu maswali yao.

Mheshimiwa Rais, najua siruhusiwi kufanya utafiti bila kupata kibali, lakini niseme kwamba nimefanya umbeya kidogo wa kujua tatizo la baadhi ya watu katika utendaji unatokana na nini, kimsingi nianze kwa kukiri kwamba msalaba mkubwa tumekuwa tukiwabebesha viongozi waandamizi lakini nadhani inawezekana kukawa na tatizo pia ila ukweli ni kwamba  matatizo yapo kada ya kati ambayo siku zote haikumbwi  na msukosuko wa kuwajibishwa. Kumbuka kuwa hii ndiyo kada ya utendaji hasa, ndiyo kada inayoingia na kufanya  mikataba mbalimbali.

Ndiyo kada ambayo ni injini ya uendeshaji wa majukumu mbalimbali ya serikali na taasisi za serikali, ndiyo kada ambayo inajua mwenendo wa shughuli za kila siku, ndiyo kada ambayo inajua siri zote za serikali na taasisi za serikali, kada hii ndiyo inaweza ikavuruga jambo lolote – wakati wowote na anayebeba lawama ni kiongozi mkuu wa serikali au taasisi ya serikali.

Nimewaza sana kabla ya kuandika utafiti huu binafsi ni jinsi gani ambavyo kada ya kati imekuwa ikikwamisha mambo kutokana na urasimu ambao hauna maana. Kuna wakati unataka mambo yaende lakini kuna watu wanataka mambo yasiende kwa kasi hiyo kutokana na mambo yao binafsi, na hapo ndipo unapojua kuwa bado kuna wapigaji na ni kikundi kikubwa.

Mheshimiwa Rais, pia tatizo si wafanyakazi wanyonge wa chini, na labda leo nikupe siri kwamba kundi hili ndilo linaloumia sana katika utumishi wa umma, ni kundi ambalo linafanyishwa sana kazi na watu wa kada ya kati na ni kundi ambalo linatupiwa lawama sana na hawa madalali wa kati, kimsingi hili ndilo kundi ambalo ni injini ya ukweli ya kukamilisha majukumu ya kila siku.

Najua kwamba unawawajibisha vizuri viongozi mbalimbali, hasa ambao hawatekelezi majukumu yao ya kila siku, wapo wanaowajibishwa kutokana na kushindwa kufuatilia mambo mbalimbali katika ofisi zao, na hawa ni lazima wawajibike kwa sababu hawaendi chini ya kada ya kati kujua nini kinachoendelea, endelea kuwawajibisha kwa sababu litakuwa fundisho kwa wengine ambao wanaamini katika menejimenti na si watumishi mwega na wanataaluma wa kawaida.

Mheshimiwa hapa kuna tatizo la kutishwa  na kuonewa sana na hao wanaoitwa wakuu wa idara na vitengo, hapa kuna maisha ya wasiwasi sana baina ya mtumishi na ofisa uajiri, ni kama vile wanatumia jina lako vibaya na kukujengea ukuta na uadui mkubwa na watumishi wako wa ngazi ya chini. Nimeamua nikueleze ukweli ili ujue nini kinachoendelea.

Nadhani mazoea ya zamani hawataki yawaguse bali wameamua kuwasukumizia watumishi wa chini, pia nadhani kwa kutumia jina lako na kulewa madaraka wamepata fursa ya kuwaonea watumishi wengine, hivyo kwa kufanya hayo wanaendelea  kufifisha juhudi zako za kufanya kazi kwa amani na ufanisi.

Naipenda nchi yangu lakini kwa mtindo wa baadhi ya watumishi, tena wa umma ambao kimsingi mkono wako hauwafikii wananifanya niichukie kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, wananifanya nione kuajiriwa ni kuingia jela ya kujitakia, wananiaminisha kuwa mjasiriamali ni kukumbana na vikwazo vya kada ya kati yenye mtazamo tofauti kabisa na wako.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri