Mpita Njia (MN) kwa umri alionao, anaona kuna haja ya kuyakaribia Maandiko Matakatifu na kuyaishi.

Kwa umri wake amepitia mengi, lakini la hivi karibuni la kuingia katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili limemfanya azidi kuimarika kiimani.

Ni kwa sababu hiyo MN ameanza kukariri baadhi ya vifungu. Baada ya kufika Muhimbili, akarejea maandiko katika Kitabu cha Ayubu 14:1-2…“Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. 2 Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.”

Naam, ni kwa kutambua hilo, MN kama walivyo waamini wengine wa dini zote, anatambua kuwa kuna siku ataachana na ulimwengu huu. Hilo halina mjadala.

MN alipoingia katika chumba cha kuhifadhia maiti pale Muhimbili alipambana na kitu ambacho nafsi yake imegoma kabisa kukinyamazia.

Anaamini kuwa chumba kile cha kuhifadhia maiti ndicho chumba pekee wanachoingia wote – bila kujali maskini au tajiri. Ni mahali ambako mwanadamu mzima akiingia lazima akili itikisike! Licha na yote hayo, mochwari ndiyo chumba kisichokwepeka.

Pamoja na umuhimu wake, pale Muhimbili hali si nzuri. MN anaweza kuonekana kama anazungumza jambo lisilostahili, lakini anaamini kuwa wasiotaka kulisema hili ndio wabaya.

Hali ya hewa katika chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili si njema hata kidogo. Kuna harufu kali mno ambayo si rahisi kuvumiliwa na mtu asiyeingia humo mara kwa mara.

Inawezekana hili halisemwi na wahudumu kwa sababu wameizoea hali ile, au halisemwi kwa sababu watu ni waoga; au halisemwi kwa sababu kuna imani kuwa mochwari hakupaswi kuwa pa kuvutia!

Mpita Njia, anatambua na kuheshimu kazi kubwa na nzuri inayofanywa Muhimbili. Pamoja na ukweli huo, anatoa ushauri kwa menejimenti kuzuru mochwari na kuona namna ya kuweka mazingira ili harufu ya miili isiendelee kuwa kama ilivyo.

MN haamini kama hakuna bajeti ya kupata dawa za kukata harufu hiyo. Anadhani kinachokosekana ni utashi tu wa kuondoa hali hiyo kwa vile imezoeleka kuwa sehemu ya kuhifadhia maiti si sehemu ya kukaguliwa mara kwa mara.

Kwa heshima kubwa, na kwa kutambua mochwari ni kama nyumba ya kulala wageni (haikwepeki), jamani wahusika fikeni hapo mochwari mrekebishe hali. Vinginevyo MN na wenzake wataamini kuwa kwa hali mbaya ya mochwari hiyo ndiyo maana wakubwa wengi siku hizi miili yao inatunzwa kule jeshini. Chonde chonde jamani. Mochwari ya Muhimbili ndiyo mochwari ya taifa. Iwekewe mazingira mazuri ya usafi.

2493 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!