Binadamu ni kiumbe mwenye uwezo wa kutambua mema na mabaya. Ana akili ya kufikiri na kutengeneza jambo au kitu. Lakini hughafilika kila mara, si mkamilifu. Ni mdhaifu katika matendo yake.

Uwezo na akili alizonazo zinampa kiburi kuweza kutengeneza kitu akitakacho kwa faida yake na wenzake katika umoja wao. Uwezo na akili zake zinaishia katika kufikiri, kubuni na kutengeneza, si kuumba. Hana uwezo huo.

Laiti Mwenyezi Mungu (muumba wake) angempa uwezo wa kuumba, leo dunia yetu na sayari nyinginezo zingekuwa shakani kusanifiwa kiumbo na njia zao kuparaganyika na kugongana hewani. Viumbe vingi vingebanana na kuharibu mandhari za sayari.

Mwenyezi Mungu alilijua hilo ndiyo maana hakumpa uwezo na akili ya kuumba. Tazama hiki alichopewa cha kutengeneza na kufikiri, anavyoifanyia dunia na viumbe vingine uharibifu na uchafuzi kama miliki zake. Ilhali si vyake.

Katika hali ya uwezo wa kutengeneza, kufikiri na kubuni binadamu huyu, ameigawa nafsi yake katika mafungu. Fungu la kutenda mema na fungu la kutenda mabaya. Mafungu haya yamo katika miliki yake na anayatumia atakavyo.

Anapotumia fungu la kutenda mema wanadamu wenzake wanafurahi, wanamsifu, wanampongeza na wanamwombea heri na baraka kwa Muumba wake, amzidishie uwezo na akili kutenda mambo mema na hisani.

Nyimbo, mashairi na simulizi zinajaa maneno matamu na mazuri ya kumtukuza na kumtakia afya njema na kumlinda asizongwe na mahasidi. Sifa na habari njema husambazwa duniani. Huyu ndiye binadamu.

Anapotumia fungu la kutenda mabaya, wanadamu hao wanamchukia, wanamsengenya na wanamzogoa na hatimaye wanamlaani. Wanamuhisi si mtu mwema na mpinga maendeleo ya watu. Ni binadamu mwenye choyo.

Kauli zake zinatia kichefuchefu nyoyo za watu na matendo yake kuonekana kinyaa. Ananyimwa sifa ya ubinadamu na kujazwa sifa ya ubaya na uhayawani. Huyu si binadamu.

Mara kwa mara nashuhudia kuona au kusikia binadamu fulani anavyotengeneza husuda kwa binadamu mwenzake aliyepewa au aliyepata kitu. Ni tabia ya kuonea wivu mtu kutokana na mafanikio yake. Ni chuki dhidi ya mtu pamoja na mali yake.

Kwa akili aliyonayo binadamu, wakati fulani anajifanya mwenye huruma, upendo na mtetezi wa watu maskini – wanyonge. Ana uwezo zaidi wa kufanya mazuri kuliko binadamu aliyopo katika uongozi au madaraka. Lakini akipewa nafasi hiyo hufanya kinyume cha matazamio ya wanadamu. Anakuwa mbadhirifu na fisadi.

Binadamu umeumbwa kuwa kiumbe bora kuongoza viumbe vingine kwa njia ya haki na usalama. Unapomwona binadamu mwenzako anafanya vizuri, mkubali, msifu na mpe nafasi atimize mema aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Funzo hili nenda nalo kila siku duniani.

Mutribu mmoja wa taarabu visiwani Zanzibar, ustadhi Hajji Gora katika shairi lake moja anasema: ‘MPEWA HAPOKONYEKI’. Baadhi ya mishororo ya shairi inasema:

Mpewa hapokonyeki, aliyepewa kapewa

Wewe ukifanya chuki, bure unajisumbua

Aliyepewa kapewa, naapa hapokonyeki

Kwa alichojaliwa, walahi hapunguziki

Kwake ukilia ngo, unajipatisha dhiki.

Please follow and like us:
Pin Share