*Asema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kiongozi mbunifu na wa vitendo

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mbunifu, wa vitendo na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania kwa kutoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ikiwemo uboreshwaji wa miundombinu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Aprili 26, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Msimbazi jijini Dar es Salaam baada ya kukagua ujenzi wa Daraja la Mkwajuni pamoja na Daraja la Kigogo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema ujenzi wa madaraja hayo ni ubunifu wa Msheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kumaliza mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwaelekeza wataalam kuandika andiko la kutafuta namna ya kutatua tatizo la mafuriko kwa dhararu ndipo zinapatikana fedha ambazo zimewezesha ujenzi wa jumla ya madaraja 81 nchi nzima ikiwemo barabara ya kwenda Lindi na Mtwara ambayo kipindi cha mvua hugeuka kisiwa.

Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa ofisi zote za umma zipo kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania kwa kutoa majawabu ya kero zinazowakabili, hivyo ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wote wa umma kutumia ofisi hizo ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutoa majibu mazuri kwa wananchi.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Segerea, Agnesta Lambart kupitia Chama cha CHAUMA ameupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utatuzi wa kero za wananchi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao ikiwemo ya afya na miundombinu.

“Kwa haya ninayoyaona ndani ya jimbo la Segerea ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na sasa tunaweka pembeni itikadi za vyama vyetu tunakwenda kuwatumikia Watanzania ambao wanahitaji maendeleo. Mimi ni mpinzani ila si upinzani wa maendeleo.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassam kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ambapo madaraja yanajengwa katika maeneo mengi ya mkoa huo.

Awali, Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mkwajuni lenye urefu wa mita 20 kimo mita 5.5 na barabara unganishi zenye jumla ya urefu wa kilometa 0.660, ambapo mradi huo umefikia asilimia 92 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 11 hadi kukamilika.

Pia, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa Daraja la Kigogo lenye urefu wa mita 50 kimo mita 8.9 na barabara unganishi zenye jumla ya urefu wa kilometa 0.625, ambapo mradi huo umefikia asilimia 82 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 17 hadi kukamilika.