Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta ya viwanda na taasisi binafsi, kwa lengo la kukuza sekta ya elimu ya mafunzo ya ujuzi ili wahitimu waweze kuendana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 23,2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mtaala mpya wa mafunzo kwa wakufunzi na mafundi seremala. Mafunzo hayo yataendeshwa na VETA kwa ushirikiano na kiwanda cha Emirates Aluminium Profile.
Amesema kuwa taifa imara linahitaji kukuza ubunifu, ujuzi na ushindani katika uchumi, hivyo serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha elimu inayozingatia ujuzi. Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila mhitimu anayetoka chuoni anakuwa na uwezo wa kujiajiri na hata kuajiri wengine.
Aidha, Ameir alibainisha kuwa ushirikiano kati ya VETA na Emirates Aluminium Profile unalenga kuimarisha upatikanaji wa rasilimali watu wenye ujuzi na ubunifu, huku akieleza kuwa mtaala huo mpya umeanzishwa kwa wakati muafaka kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
“Niseme kuwa mafanikio ya elimu ya ufundi stadi yanategemea kwa kiwango kikubwa ushirikiano kati ya vyuo vya mafunzo, sekta ya viwanda pamoja na wadau wengine wa maendeleo,” amesema Naibu Waziri.
Mkurugenzi wa kampuni ya Emirates Aluminium, Deogratis Marandu, amepongeza kwa dhati uzinduzi wa mtaala mpya wa mafunzo kwa mafundi, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha taaluma na hadhi ya fani hiyo nchini.
Amesema kuwa hapo awali mafundi walikuwa wakijifunza kwa mfumo wa kufundishana wenyewe kwa wenyewe bila kuwa na vyeti rasmi vya kuwatambua, hali iliyosababisha kukosa uthamini stahiki katika soko la ajira.
Ameeleza kuwa kupitia mtaala huo mpya, mafundi watapata vyeti vitakavyowatambulisha rasmi, kuwapa fursa ya kupata mikopo, pamoja na kushiriki kikamilifu katika zabuni na tenda za ndani na nje ya nchi.
“Nashukuru sana kwa mashirikiano haya kati ya VETA na Emirates Aluminium katika kuwapatia vijana mafunzo na vyeti vitakavyowajengea uwezo na kuwaongezea thamani katika soko la ajira,” amesema Marandu.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mafundi kutoka Emirates Aluminium, Hamidu Mabaraza, amesema kuwa hapo awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa mtaala rasmi wa kufundishia fani ya vioo, jambo lililokuwa linakwamisha maendeleo ya taaluma hiyo.
Amesisitiza kuwa ujio wa mtaala huo ni mwanzo wa mapinduzi ya kiuchumi kwa mafundi, kwani utawajengea ujuzi unaotambulika na kuwawezesha kunufaika zaidi na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiendelea kutoa wahitimu katika fani mbalimbali za ujuzi, hatua inayochangia kuongeza nguvu kazi yenye stadi nchini. Ameeleza kuwa VETA itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, hivyo kuwawezesha kujiajiri na pia kuajiriwa kwa ufanisi.





