Na Mwandishi wetu,Jamhuri Media Dar es salaam
Wananchi wote wametakiwa kulipia pango la ardhi ndani ya siku 14 kuanzia leo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka agizo hilo.
Agizo hilo limetolewa leo Aprili 24, 2026 jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es salaam,Shukrani Kyando akisisitiza kuwa ulipaji wa kodi wa ardhi ni wajibu wa kila mmiliki wa ardhi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 24(1), kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi, lakini haki hiyo inaambatana na wajibu wa kulipia pango la ardhi kwa mujibu wa sheria.
Aidha, amesema kuwa katika ukaguzi uliofanyika kwa wananchi zaidi ya 600 waliotembelewa, ilibainika kuwa wengi wao hawajalipa kodi ya ardhi kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita licha ya kupewa elimu na kusisitizwa kulipa, bado baadhi yao hawajatekeleza wajibu huo.
Ameonya kuwa kuanzia leo, wananchi wote wanaodaiwa wanapaswa kulipa ndani ya wiki mbili, (siku 14) na baada ya muda huo, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.
“Kisheria, kila anayemiliki ardhi anatakiwa kulipia pango la ardhi hivyo, ni muhimu kwa wananchi kutimiza wajibu huu ili kuepuka hatua za kisheria,” amesisitiza Kamishna
Naye Mratibu wa Kodi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Lihapa, amewataka wananchi wote wanaomiliki viwanja kuhakikisha wanalipa kodi ya ardhi kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
“Ulipaji wa kodi ya ardhi ni wajibu wa kila mmiliki wa kiwanja, na kusisitiza kuwa ni muhimu kutekeleza jukumu hilo kwa hiari na kwa wakati” Amesema Maratibu
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sura ya 113, kifungu cha 35 (a), wananchi wanapaswa kulipa kodi hiyo kama inavyoelekezwa kisheria.
Aidha, ameonya kuwa kwa wale watakaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya ardhi kwa hiari, serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.



