Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 sinza ilikuwa na wakazi 40,546 lakini idadi hiyo ilipungua hadi kufikia 31,396 mwaka 2022.
Licha ya kupungua kwa idadi ya wakazi bado eneo hilo limeendelea kushuhudia ongezeko la shughuli za biashara na uwekezaji hali inayoashiria mabadiliko ya matumizi ya ardhi kutoka makazi ya kawaida kwenda matumizi mchanganyiko.
SINZA YA ZAMANI

Sinza ilipangwa rasmi mwaka 1973 kupitia mradi wa Site and Services uliotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia huku lengo kuu likiwa ni kutoa makazi kwa wananchi wenye kipato cha chini waliokuwa wakihamishwa kutoka Manzese.
Mpango huo ulihusisha viwanja vya ukubwa wa mita za mraba 288, vilivyokusudiwa kujengwa nyumba za familia moja za ghorofa moja, pamoja na kuwepo kwa maeneo ya wazi yenye huduma za maji na miundombinu ya kijamii.
Hata hivyo kadri miaka ilivyopita mpango huo wa awali ulianza kupoteza uhalisia wake kutokana na ongezeko la watu, ukuaji wa uchumi na mabadiliko ya mahitaji ya makazi. Sinza ilianza kubadilika na kuwa eneo lenye shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Serikali iko katika mpango madhubuti wa kusuka na kulikarabati upya eneo la Sinza lililopo katika Manispaa ya Ubungo ambalo kwa sasa makazi pamoja na maduka yamerundikana katika eneo moja.
Mpango huu unaoratibiwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi una lengo la kufikia mwaka 2046 eneo la sinza liwe na nyumba za ghorofa ambazo zitaanzia ghorofa 8 mpaka 20 kulingana na aina ya udongo uliopo katika eneo husika.
Hii itakuwa sio mara ya kwanza kwa Serikali kunzisha mpango kazi kama huo ambapo mwaka 2011 ulianzishwa katika eneo la Msasani ambapo mpaka sasa utekelezaji wake bado unasuasua huku eneo la kigamboni ambalo mpango huo pia ulianzishwa ukifutwa baadae.
Eneo la Sinza limegawanywa katika mitaa mitano ambayo ni Sinza A, B, C, D na E ambapo kwa sasa inapitia mabadiliko makubwa ya kiuchumi kijamii na kimazingira yanayolifanya kuwa kitovu kipya cha maendeleo ya mijini.
UKUAJI WA MAENEO
Aidha ukuaji wa maeneo jirani kama Mwenge, Ubungo na Mlimani City Mall umeongeza kwa kiasi kikubwa presha ya maendeleo katika eneo la Sinza ambalo limegeuka kuwa kitovu cha biashara kinachohudumia wakazi wa maeneo jirani kama Manzese, Kijitonyama na Ubungo.
Mabadiliko haya yameambatana na kuongezeka kwa majengo ya ghorofa, biashara ndogo ndogo, hoteli, migahawa na huduma mbalimbali. Hata hivyo, maendeleo haya yamekuwa yakifanyika bila mwongozo thabiti, jambo lililosababisha changamoto kadhaa ikiwemo uvamizi wa maeneo ya wazi, matumizi yasiyo sahihi ya ardhi na uhaba wa maegesho.
SINZA YA MPYA

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo imeanzisha Mpango wa Uendelezaji Upya wa Sinza kwa mwaka 2026/2046.Mpango huu unalenga kuweka mfumo madhubuti wa maendeleo utakaoendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Kupitia mpango huu wa uendelezaji upya, Sinza inalengwa kubadilishwa kuwa mji wa kisasa wenye majengo ya ghorofa, matumizi mchanganyiko ya ardhi, miundombinu bora na mazingira safi. Pia inalenga kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji chenye uchumi imara na kinachotoa maisha bora kwa wakazi wake.
Mpango wa Uendelezaji Upya wa Sinza unatoa fursa ya kipekee ya kubadilisha sura ya eneo hili, lakini pia unahitaji usimamizi makini ili kuhakikisha unaleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha kuboresha maisha ya wakazi, kuvutia uwekezaji mpya, kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, pamoja na kukuza uchumi wa eneo. Aidha, Sinza imechaguliwa kutokana na nafasi yake ya ikiwa imeunganishwa na barabara kuu kama Morogoro na Sam Nujoma, pamoja na ukaribu wake na taasisi za elimu kama Chuo kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Ardhi.
Licha ya umuhimu wake Sinza inakabiliwa na changamoto kubwa za miundombinu. Takribani asilimia 86.9 ya barabara zake ni nyembamba na hazina mifereji ya maji wala njia za watembea kwa miguu. Hali hii husababisha msongamano mkubwa wa magari na hatari kwa watumiaji wa barabara.
Usafiri wa umma unategemea zaidi daladala, bodaboda na bajaji huku barabara kuu kama Sam Nujoma na Shekilango zikibeba mzigo mkubwa wa usafiri pamoja ukosefu wa maegesho rasmi unaolazimisha magari mengi kuegeshwa barabarani, jambo linalochangia msongamano na ajali.
Takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya ardhi yamebadilika kwa kiasi kikubwa. Makazi yanachukua asilimia 26.28 ya eneo, taasisi za umma asilimia 17.46, na matumizi mchanganyiko asilimia 9.26. Wakati huo huo, maeneo ya wazi yamepungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 6.8 mwaka 1973 hadi asilimia 0.88 mwaka 2024.
Kupungua huku kwa maeneo ya wazi kunahatarisha ustawi wa mazingira na ubora wa maisha ya wakazi. Aidha, biashara nyingi zimejengwa katikati ya makazi, hali inayosababisha migongano ya matumizi ya ardhi.


