Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai, amethibitisha dhamira ya taasisi hiyo kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ya afya ili kuboresha upatikanaji bidhaa za afya, gharama nafuu, na ubora wa huduma za afya.

Akizungumza jana jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa sekta binafsi ya afya, Tukai alieleza fursa mbalimbali za ushirikiano zinazoweza kuongeza ufanisi katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

Alisisitiza kuwa MSD ingependa kuongeza ushirkiano na sekta binafsi katika maeneo muhimu ikiwemo uzalishaji wa ndani kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Halikadhali, Kwa kuzingatia mafanikio makubwa ambayo MSD imeyapata kwa kushirikiana sekta binafsi hasa katika ununuzi na upatikanaji wa bidhaa, uhifadhi, pamoja na usafirishaji wa vifaa na dawa muhimu.

Bw. Tukai amesema kwamba lengo la MSD kwa sasa ni kuanza kuuza bidhaa moja kwa moja kwenda katika vituo vya afya vya binafsi, hatua ambayo itafikiwa baada ya kukamilisha miongozo ya ndani ya taasisi pamoja na vibali muhimu kutoka kwa mamlaka husika.

Alibainisha kuwa ushirikiano imara kati ya MSD na watoa huduma binafsi utaongeza nguvu ya pamoja katika kufanya majadiliano ya kibiashara, jambo litakalosaidia kupunguza bei na kuboresha upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya.

“Kwa kuunganisha nguvu, tunaweza kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba, bei nafuu, na huduma zinazowafikia wananchi kwa urahisi zaidi,” Alisema Tukai.Aidha, Tukai alisisitiza umuhimu wa kuleta usanifishaji wa vifaa na mahitaji ya afya katika sekta binafsi, akitolea mfano vifaa vya maabara.

Alieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha usimamizi wa vifaa, kuongeza ufanisi na uhakika wa upatikanaji wa vitendanishi (reagents), pamoja na kupunguza gharama.

Kwa mujibu wake, juhudi hizo za pamoja zitaleta huduma zenye ufanisi wa gharama, kuimarisha uhakika wa ubora wa bidhaa, na kuinua viwango vya utoaji huduma za afya kwa ujumla.Mkurugenzi Mkuu huyo alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo imara na endelevu wa huduma za afya unaokidhi mahitaji ya wananchi.

Kongamano hilo lililotamatika leo, liliwaleta pamoja wataalamu na wadau wa sekta binfasi ya afya kujadili namna ya kuimarisha ubora na ufanisi wa hali ya juu katika utoaji wa huduma za afya za sekta binafsi, kuelekea bima ya afya kwa wote.