
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa yeye ndiye yuleyule na hajabadilika kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Amesema bado ni kiongozi anayeamini katika falsafa ya maridhiano kama ilivyokuwa tangu alipochukua uongozi wa nchi.
Ameyabainisha hayo Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea ripoti ya Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025.
Aidha, ameeleza kuwa wakati akifuatilia uwasilishaji wa ripoti hiyo alisikia sentensi inayosema, “Tunamtaka Samia wetu tunayemfahamu,” hali iliyoashiria kana kwamba alipokuwa anaingia madarakani alikuwa tofauti na alivyo sasa.
Pia ameongeza kuwa anawahakikishia Watanzania kuwa yeye ni Samia yuleyule wa falsafa ya maridhiano (4R), na anachohitaji ni ushirikiano wao katika utekelezaji wa falsafa hiyo.
Amesema kuwa “kidole kimoja hakivunji chawa,” akisisitiza kuwa hawezi kufanikisha mambo peke yake bila ushirikiano wa wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa ni muhimu kwa Watanzania kuungana ili kufikia malengo ya pamoja ya taifa.
Pia ameongeza kuwa wananchi wasikubali kurubuniwa au kuchochewa na wanaharakati, wanasiasa pamoja na watu wenye maslahi binafsi katika kuharibu tunu ya amani ya Tanzania.


Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 23 Aprili, 2026.
















