Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum, amewaasa vijana kuwa makini na wazalendo kwa nchi yao, huku akiwasisitiza wasikubali kutumika.

Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Sheikh Profesa Mussa amesema hatua hiyo itasaidia nchi kuendelea kuwa salama kwa sababu hakuna sehemu nyingine ya kwenda.

Amesema siku zote vijana wanapokuwa na jambo lao ambalo linahitaji ufumbuzi ni vizuri wakatumia njia sahihi ya kufikisha ujumbe kwenye mamlaka zinazotambulika kisheria.

“Nawasihi vijana wetu wawe makini, wazalendo na wasikubali kutumika,hii ndiyo nchi yao ambayo wanapaswa kuilinda kwa nguvu zote, hawana mahala pengine pakukimbilia kama mambo yakiharibika, wajifunze kulingana na matukio yaliyotokea siku za nyuma.

“Amani ni maendeleo, ni rasilimali muhimu, si njia ya kutatua matatizo yetu, tunatakiwa kujifunza kwa kilichotokea Oktoba 29, mwaka jana pamoja na ujana wao hawakuweza kufanya chochote katika hali ya hofu lakini vijana hata kama wana changamoto waone naman ya kufikisha changamoto zao sehemu inayostahili.

“Kuharibu nchi au kuvuruga nchi kwa sababau ya changamoto ulizonazo si njia ya kutatua changamoto hizi. Ujana wao si chochote, wasitumike, bali wawe na uzalendo wa kuilinda nchi yao, maana changamoto zitakwisha na utatamani uishi katika nchi uliyoiharibu.

Hivi ukivuruga nchi utakwenda kuishi wapi, wakati umeshaharibu miundombinu ambayo ungekwenda kuitumia, unachoma vituo vya mabasi, majengo ya serikali na vingine, si sahihi hata kidogo,” amesema.

Amesema kutokana na hali hiyo, viongozi wa dini nao wanapaswa kusimama imara kuisaidia serikali kudumisha amani, utulivu na mshikamano kwa sababu wanakutana na makundi ya waumini wao kila wakati.

“Amani maana yake ni kuwa na utulivu wa nafsi ya kila mtu, amani katika mali yake na watu wote wanaomzunguka… kunapokuwa na utulivu maana yake watu wataweza kufanya shughuli za kujipatia maendeleo, kila mtu ataweza kufanya kazi kwa bidii, mwisho wa siku wanaweza kupata maendeleo.

“Kila mtu atapata nafasi ya kumuabudu Mola wake kupitia dini yake, kutakuwa na uhuru wa kuabudu sehemu anayotaka kuabudu, maana yake ni kwamba wananchi wanakuwa huru kufanya ibada.

Inapokosekana amani ni shida.Kwa mfano, Oktoba 29, mwaka jana hakuna mtu aliyetoka nje na taifa zima lilisimama, tuliona mfano mzuri wa amani kuvurugika. Ni wakati mzuri tukajifunza kutokana na makosa,” amesema.

Amesema kinyume cha hapo ni kukosekana kwa utulivu na kuanza kushuhudia vurugu na umwagikaji wa damu, mambo ambayo kamwe hayapaswi kupewa nafasi.

“Kama hakuna amani, hakuna mtu anayeweza kufanya jambo lolote la kuiletea nchi maendeleo. Kufikia malengo ya nchi lazima amani iwepo ili watoto wetu waweze kwenda shuleni, kinyume chake hayo hayawezi kufanyika.

Amesema maandiko matakatifu yanahamasisha amani, hivyo viongozi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kusimamia ipasavyo.

“Madhehebu yote yanahamasisha amani, utulivu, viongozi wa dini tusimamie na kurejesha umoja wetu kama ilivyokuwa siku zote, tuwaache wanasiasa waendelee na siasa zao ili wakikosea sisi tusimame na tuwaonye, tuwaelekeze na kuwakumbusha wajibu wao.

“Viongozi wa dini hatutakiwi kusimama nyuma ya watu wanaovunja umoja wetu kamwe, tusichanganye siasa na mambo ya dini, tusijiingize katika siasa, tuache wanasiasa wakae kule, wakikosea tuwakosoe.

“Tukiingia katika mambo ya siasa, tutawachangaya waumini wetu katika nyumba za ibada, wajibu wetu ni kuhakikisha tunaisaidia serikali iwepo na watu waweze kumuabudu Mungu. Tusipoisaidia serikali maana yake sisi tutakuwa ni mojawapo ya watuwanaovuruga amani, kinyume cha mafundisho tuliyonayo” amesema Mongella

Rais mstaafu wa Bunge la Afrika, Gertrude Mongella, amesema amani inapaswa kudumishwa, licha ya kuwa suala hilo ni pana mno kama mizizi ya mti.

“Suala la amani ni pana kulishughulikia. Ni mti mkubwa wenye mizizi mingi. Hauwezi kuukata kwa kukata mzizi mmoja tu. Siwezi kusema raia, maana kuna vitu vingi. Viongozi ni raia, watoto ni raia, vijana, wazee wote hawa ni raia, usipoweza kuijua jamii, nakumbuka jamii za zamani zilikuwa zinaendeshwa na mila na desturi,” amesema.

Amesema kuna kila sababu ya kuitafakari jamii ya leo, misingi na mizizi inayoendesha jamii ili kupata majibu sahihi.

Kuhusu viongozi wa dini, wanapaswa kujitafakari kwenye taasisi zao.“Ungeniuliza taasisi za kijadi na kimilila zilikuwa na nguvu, siku hizi hata taasisi za kidini inategemeana, siwezi kusema jumla, angalau wao wanakubalika kiimani, ni muhimu wachukue nafasi yao ambayo inawafaa kama watu wa imanni, waijenge ili imani ijengeke.

“Kama Wakristo, tunasema amani iwe nanyi kila Jumapili, kila misa padri anasema amani iwe nanyi, tunamjibu iwe pia nawe. Kama tunaisema kikweli kweli hiyo amani lazima tuisimamie,” amesema