……………………………………………

Bohari ya Dawa (MSD) imesema imeendelea kuboresha mfumo wa ununuzi wa bidhaa za afya nchini kwa kutumia mikataba ya muda mrefu (Framework Agreements), hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unakuwa wa uhakika wakati wote.

Akitoa taarifa ya ununuzi wa dawa katika kikao kazi kati ya MSD na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kilichofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki hii, MSD ilieleza kuwa mfumo huo umeongeza ufanisi, uwazi na kasi ya upatikanaji wa bidhaa za afya.

Kwa mujibu wa MSD, mikataba hiyo hufanyika kupitia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST), ambapo wazabuni huchaguliwa na kuthibitishwa sifa zao, masharti pamoja na bei kwa kipindi cha hadi miaka mitatu.

“Tumeimarisha matumizi ya mikataba ya muda mrefu ili kuharakisha mchakato wa ununuzi, ambapo baada ya mikataba kukamilika, tunatoa maagizo ya bidhaa (Call-off Orders) bila kurudia hatua zote za zabuni,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

MSD ilibainisha kuwa mfumo huo unapunguza muda wa upatikanaji wa bidhaa, ambapo kwa bidhaa zenye mikataba huchukua wastani wa miezi mitatu tangu kuagiza hadi kupokelewa, tofauti na zile zisizo na mikataba ambazo huchukua muda mrefu zaidi.

Aidha, ilielezwa kuwa takribani asilimia 80 ya bidhaa za afya huagizwa kutoka nje ya nchi, huku zingine zikipatikana ndani ya nchi kutoka kwa wazalishaji na wasambazaji walioidhinishwa.

Kwa upande wa gharama, MSD ilisema matumizi ya mikataba ya muda mrefu yamepunguza matumizi ya fedha zinazotumika katika matangazo ya zabuni yanayojirudia mara kwa mara, pamoja na kuhakikisha bei zinabaki thabiti kwa kipindi cha mkataba.

“Faida nyingine ni pamoja na kuimarisha upangaji wa bajeti kwa kuwa bei zinakuwa zinajulikana mapema na kudumu kwa muda mrefu, pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa ununuzi,” iliongeza taarifa hiyo.

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, MSD imepanga kuwa na jumla ya bidhaa za afya 1,725 zinazopaswa kupatikana ghalani wakati wote, zikiwemo bidhaa muhimu 1,444, bidhaa za huduma za figo (dialysis) 112 na bidhaa za miradi maalum 169.

Kati ya hizo, bidhaa 1,354 sawa na asilimia 78.5 tayari zina mikataba ya muda mrefu, huku bidhaa 371 zikiwa katika hatua mbalimbali za zabuni ili kuingia kwenye mfumo huo.

Aidha, kati ya bidhaa zenye mikataba, 1,036 zina mikataba ya moja kwa moja na wazalishaji, huku 318 zikiwa chini ya wasambazaji walioidhinishwa na wazalishaji (authorized dealers).

MSD ilifafanua kuwa uwepo wa mikataba zaidi ya mmoja kwa baadhi ya bidhaa husaidia kukabiliana na changamoto za uzalishaji, hususan pale kiwango cha oda kinaposhindwa kufikia kiwango cha chini cha uzalishaji (minimum order quantity).

“Tukiwa na chaguo la wasambazaji walioidhinishwa, tunaweza kupata bidhaa kwa wakati pale wazalishaji wanaposhindwa kukidhi mahitaji kwa sababu mbalimbali,” ilieleza.

Kwa upande wa wazalishaji, MSD imeingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji 1,036, ambapo kati yao 921 ni wa nje ya nchi na 115 ni wazalishaji wa ndani.

MSD imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 pamoja na kanuni zake za mwaka 2024, ili kuhakikisha huduma za afya nchini zinaboreshwa na kuwafikia wananchi kwa wakati.