Salamu nyingi sana kama mchanga wa pwani zikufikie mahali popote ulipo, hofu na mashaka ni juu yako uliye mbali na upeo wa macho yangu, na baada ya salaam je hujambo.

Madhumuni ya barua yangu ni mengi, lakini nimeona leo niseme kile ambacho macho na masikio ya walio wengi huku kwetu wanasemaje, nimeamua nikudokezee kidogo tena kwa juu juu ili uweze kujua na kuamua ufanye nini.

Nimekuandikia barua hii rasmi leo ili ujue hawa wananchi wako wanasemaje huku Kipatimo kutokana na hali halisi ya maisha ilivyo sasa, maisha yalivyo sasa si yale ambayo sisi tuliishi katika kipindi cha Uhuru, sasa ni maisha ya sayansi na teknolojia, maisha ya kurahisisha kila kitu hata kile kilichokuwa kigumu kwa wakati wetu.

Nakumbuka mengi sana mheshimiwa mkuu wetu wa kaya, nakumbuka uhifadhi wa nyaraka za Serikali na ugumu wake ambao ulikuwa unatokea kama mtu anahitaji taarifa zake ambazo zimehifadhiwa katika faili.

Nakumbuka taabu ya ubashiri wa madaktari wetu ambao ilikuwa nadra sana kufanya makosa ya utabiri wao pamoja na kwamba vifaa vya kisasa walikuwa hawana, hawakuwahi kukosea kubashiri upasuaji wa moyo  kwa mgonjwa wa kichocho, haikuwahi kutokea.

Nakumbuka usalama wa raia ulikuwa katika hali ya juu sana, hatukuwahi kusikia mauaji ya kutisha, kubakwa, uporaji wa mchana, majambazi, majangili na vita ya wakulima na wafugaji  katika nchi ambayo mawasiliano ya haraka yalikuwa yakiunganishiwa Dodoma kwa kupiga namba 900.

Hatukuwahi kusikia mauaji ya watu mashuhuri na viongozi wa Serikali kwa kisingizio cha watu wachache kujinufaisha kwa mali yake, tuliwapenda viongozi wetu kwa kuwa tuliwachagua kwa moyo mmoja na tuliishi nao kwa kufanya nao kazi zote za maendeleo, kwa ufupi walikuwa wenzetu zaidi, hawakuwa wao.

Mheshimiwa ushabiki nchi hii ulikuwa ni ule wa Sunderland na Young Africans, hatukuwahi kusikia ushabiki wa vyama vya siasa na asasi kadhaa za kiraia kwa kisingizio cha maisha bora na haki kwa raia, mikutano ya hadhara ilikuwa ya kuelimishana juu ya kilimo bora, ulinzi na usalama na maendeleo ya ward zetu.

 

Mheshimiwa, nimeamua kuandika ili uangalie Taifa hili linakwenda wapi, kila kitu tunacho siku hizi tena vitu vinavyokwenda na wakati kwa hiyo sayansi yenu lakini mambo ni shaghalabaghala kabisa, teknolojia haitusaidii kabisa kwa kizazi ambacho tunasema ni cha maendeleo ya kisasa.

Taifa unaloongoza lina wasomi, wengine nasikia wamesoma hadi mataifa ya nje yaliyoendelea yanawahitaji kwa utaalamu wao, lakini ndiyo Taifa ambalo linaongoza kwa vituko vya karne ya 19 kwa mambo yake, mathalani tunashindwa kuwabaini wauaji na majambazi yanayofanya uhalifu mchana kweupe pee, why? Pamoja na hao kuwa na wataalamu wote hao?

Tunaishi karne ya 19 isiyo na kompyuta kwa sababu leo hii data muhimu hatuna na kama zipo zitatafutwa taratibu kuliko zamani, utadhani yanatafutwa mafaili katika stoo yenye vumbi wakati ni issue ya kubofya kompyuta yenye kila kitu, jamani hivi ni sisi kweli ama tumelogwa?

Mheshimiwa Kikwete, una vijana ambao wanadhani ukiritimba ni mfumo wa maisha na kwamba bila kufanya hivyo maisha hayaendi. Hebu fikiria kumuona mgonjwa hapo hospitali ya taifa unahitaji kuwa na kitambulisho na unasajiliwa, leo watu wanapanga foleni kujiandikisha kumuona mgonjwa, for what?

Naandika nikiwa najua kuwa kuna tatizo la uozo mkubwa ambao kuufumua  ni kazi kubwa lakini ni bora kujaribu kuanza kuliko kuacha.

Leo Tanzania kuna watu wanavunja sheria mahali popote na wakati wowote bila kuchukuliwa hatua na ukiona sheria inafuata mkondo ujue kuna mkono wa mlokole, vinginevyo mmh! Na huyo mlokole lazima aundiwe genge la majungu ili aondoke kwa kashfa. Tunakwenda wapi?

Naomba ufanyie kazi mambo haya kabla hujatoka Ikulu ili baadaye watu waseme ‘alijaribu lakini alishindwa’ na ndiyo maana leo tunasema Julius alijaribu Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha lakini mmh! yakamshinda lakini alijaribu hadi tone lake la mwisho, aliweza kuthubutu, kwa hiyo naomba uthubutu tuone.

 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri